Mazingira yenye usawa katika uchaguzi ujao DRC ni muhimu: Zerrougui

26 Julai 2018

 Uchaguzi mkuu nchini Jamhuri ya kidemoksrasia ya Congo (DRC)  unajongea na hadi sasa matayarisho yanakwenda vizuri japo kuna changamoto ambazo zinaweza kuufanya uchaguzi huo uwe na dosari.

Hayo yamesemwa na mwakilishi  maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa   na mkuu wa  kikosi  cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini DRC (MONUSCO) Leila Zerrougui,  wakati akitoa taarifa kuhusu hali ya taifa hilo kwenye baraza la Usalama hii leo , mjini New York Marekani.

Bi. Zerrougui amesema japo matayarisho yanaendelea ana wasiwasi kutokana na kuongezeka kwa visa vya ukiukwaji wa haki za binadamu pamoja na haki zingine za kimsingi na kutoa picha mbaya ya hali ya kidemokrasia akitolea mfano kuzuiwa kwa baadhi ya  maandamano ya amani

 (SAUTI YA LEILA ZERROUGUI)

Hali  ya kuhakikisha kuna mazingira ya usawa kwa wote bado haipo.”

 Ameongeza kuwa hali ya kutoaminiana imetawala kati ya walio wengi, upande wa upinzani na tume huru ya uchaguzi  nchini  humo CENI.

 Kwa mujibu wa Bi. Zerrougui mpaka sasa haijajulikana bayana ni wagombea wangapi waliojiandikisha kushiriki viti mbali mbali kwa sababu orodha kamili haijachapishwa rasmi na tume huru ya uchaguzi, ingawa ameongeza

(SAUTI YA LEILA ZERROUGUI)

“Dalili za mwanzo zinaonyeasha kuwa idadi ya wanawake inafikia zaidi ya asiliamia 12 ya wagombea wote  wa viti waliosajiliawa.”

Ameweka bayana kwamba , DRC kwa sasa iko njia panda na ndio maana anachukua nafasi hii kuomba wadau wote  katika uchaguzi huo kukubali kujumuisha kila mtu  ili uchaguzi mkuu  uwe huru, wa haki na wenye kuaminika.

Ameongeza kuwa uchaguzi huo mkuu uliopangwa kufanyika 23 mwezi Disemba mwaka huu una fursa kubwa ya kubadili hali na kuifanya nchi hiyo kuwa tulivu kwa manufaa ya raia wote  wakiwemo wanawake.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter