Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dunia inashindwa kutimiza ahadi ya SDG, yaonya ripoti ya Umoja wa Mataifa

Picha kwenye ukuta katika ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Abuja, Nigeria, linaonyesha SDGs.
UN News/Daniel Dickinson
Picha kwenye ukuta katika ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Abuja, Nigeria, linaonyesha SDGs.

Dunia inashindwa kutimiza ahadi ya SDG, yaonya ripoti ya Umoja wa Mataifa

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Bila uwekezaji mkubwa na kuongeza hatua, kufikiwa kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs kutasalia kuwa mgumu, imeonya Ripoti ya mwaka huu 2024 kuhusu mwenendo wa utekelezaji wa malengo hayo ikiwa imesalia miaka sita pekee kufikia muda ambao ulimwengu ulijiwekea kuwa umeyatimiza malengo yote 17.

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa iliyowekwa wazi leo Juni 28 inafichua kuwa ni asilimia 17 tu ya Malengo ya Maendeleo Endelevu ndio yako katika mwenendo mzuri, huku karibu nusu ikionesha maendeleo madogo au ya wastani, na zaidi ya theluthi moja yamekwama au kurudi nyuma. Athari zinazoendelea za janga la coronavirus">COVID-19, mizozo inayoongezeka, mivutano ya kijiografia na kuongezeka kwa machafuko ya tabianchi kumezuia maendeleo kwa kiasi kikubwa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo asubuhi ya leo kwa saa za New York, Marekani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres anasema,

"kushindwa kwetu kupata amani, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, na kuongeza fedha za kimataifa kunadhoofisha maendeleo. Ni lazima tuharakishe hatua kwa ajili ya Malengo ya Maendeleo Endelevu na hatuna muda wa kupoteza."

Kulingana na ripoti hiyo, watu zaidi ya milioni 23 walisukumwa katika ufukara na zaidi ya watu milioni 100 zaidi walikuwa wakikabiliwa na njaa mwaka wa 2022 ikilinganishwa na mwaka 2019. Idadi ya vifo vya raia katika vita vya kijeshi iliongezeka mwaka jana 2023. Mwaka huo pia ulikuwa wa joto zaidi kuwahi kurekodiwa huku halijoto duniani ikikaribia kiwango cha juu cha nyuzijoto 1.5 za Selsiasi.