Habari njema ni kwamba ajenda ya 2030 sasa inahuishwa japo kibarua bado kipo:Guterres

Safari ya malengo ya maendeleo endelevu au SDGs alianza mwaka 2015 na kila mtu anajua wapi ni mwisho wa safari yetu, kutokomeza umasikini na njaa, usawa kwa wanawake na wasichana , kuwawezesha vijana, kupunguza hewa ukaa, kuwa na uchumi wa kukabili mabadiliko ya tabianchi, ajira zenye hadi na mafanikio ya pamoja, jamii zenye amani na haki, haki za binadamu kwa wote na kuheshimu utawala wa sheria. Pia fursa kwa wote za kuishi katika dunia bora.
Kauli hiyo imetolewa leo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza kwenye jukwaa la ngazi ya juu la kisiasa kuhusu SDGs na kuongeza kuwa “ Kwa kifupi tumejiwekea malengo ya kuwa na usawa katika utandawazi na habari njema ni kwamba ajenda ya 2030 sasa inahuishwa. Serikali kuanzia Kaskazini hadi Kusini zimeanza kujumisha malengo ya SDG’s katika miakakati yao na mipango ya kitaifa. Sekta binafsi nazo zimeanza kuelewa kwamba biashara inayojali mazingira ndio biashara bora.Miji, makampuni ya biashara, sekta ya kimataifa ya fedha, asasi za kiraia , vijana na wengineo wanachukua hatua na tunapiga hatua katika mchakato huo.”
Katibu Mkuu amesema miongoni mwa hatua zilizopigwa katika utekelezaji wa malengo hayo 17 ya maendeleo, kiwango cha umasikini uliokithiri au ufukara kinapungua huku fursa za kupata nishati safi na ajira zenye hadhi zinaongezeka na hii inadhihirisha kwamba ajenda ya mwaka 2030 haikuwa kosa kuiweka.
Hata hivyo amesisitiza kuwa “hebu tuwe wazi tuko mbali sana kufika pale tunapotaka na tunapotea njia kwani tumetawaliwa na vita vinavyokatili maisha ya watu wengi, mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi, ukatili wa kijinsia na kuendelea kwa kutokuwepo na usawa kunaathiri juhudi za utimizaji wa malengo hayo ya SDGs.”
Guterres amesema nusu ya utajiri wote duniani unamilikiwa na watu wachache ambao wanaweza kutosha kwenye meza moja ya mduara ya mikutano.Kuna ukuaji wa uchumi usio sawia, kuongezeka kwa mzigo wa madeni, na mivutano ya kimataifa ya kibiashara ambayo inaongeza vikwazo vya utekelezaji wa malengo hayo.
Katibu Mkuu ameainisha kwamba tatizo la ajira kwa vijana linaongezeka katika viwango vya kutisha huku tatizo la njaa kimataifa likiongezeka pia.”hakuna nchi ambayo iko katika mwelekeo unaotakiwa kutimiza lengo la usawa wa kijinsia ambalo bila hilo malengo mengine hayataweza kufikiwa.Ukweli ni kwamba pengo la usawa linazindi kupanuka.”
Kuhusu mabadiliko ya tabianchi na mazingira Guterres amesema viumbe aina milioni moja viko hatarini kutoweka na kwa kasi ya sasa takribani watu milioni 500 watasalia kwenye umasikini uliokithiri ifikapo mwaka 2030. Kwa mantiki hiyo “Ni lazima tuongeze juhudi zetu sasa, ni lazima turudishe tena uaminifu kwa watu na kushughulikia mtazamo na uzoefu wa kuwatenga watu na hali ya kutojiweza inayotokana na mfumo wa sasa wa utamdawazi. Tuna suluhu bora lkatika ajenda ya 2030 ambao ni muongozo wa kuwa na utandawazi ulio sawia, na ni lazima tubadili uchumi wetu na kuingia kwenye uchumi usiozalisha hewa chafuzi ifikapo 2050.”
Katibu mkuu amesisitiza kwamba ni lazima kupiga jeki matarajio ya maendeleo nchi zisizojiweza duniani na makundi ya watu waliotengwa. Na tunapaswa kuangalia ajenda ya mwaka 2030 sio kupitia kioo cha uchumi wa muongo uliopita , bali uchumi wa muongo ujao tukichukua fursa ya uwezekano wa mapunduzi ya nne ya viwanda na kuyalinda dhidi ya hatari zilizopo. Nan dio maana leo hii kama nilivyoombwa na azimio lenu la kisiasa natoa wito wa kimatifa kwa ajili ya muongo wa khatua za kutimiza ahadi ya SDGs ifikapo mwaka 2030.
Katibu Mkuu amesema wito huo umegawanyika katika sehemu kuu tatu na sehemu ya kwanza ni “hatua za kimataifa” kwani sasa ndio wakati wa kuonyesha uongozi imara wa binafsi na wa pamoja. Tunahitaji kukomesha vita vinavyoendelea na kuzuia vingine visitokee, tunahitaji ongezeko la ufadhili, ili kusaidia mifiumo bunifu na kuongeza fursa za teknolojia na ufadhili unaojali mazingira kwa nchi zilizo katika hatari. Wakati huohuo tunahitaji kuongeza uwekezaji wa muda mrefu wa sekta binafsi kwa ajili ya malengo ya maendeleo endelevu.
Amesema pili ni “hatua kitaifa”, akihimiza kwamba nchi zinahitaji kuongeza kazi ya hatua za kitaifa ili kuleta mabadiliko ambako yanahitajika -kwenye maisha ya watu.Hii inajumuisha sera pbora na kuchukua hatua ya utimizaji ajenda ya 2030, kuweka mifumo imara na jumuishi ya kitaifa ya fedha, kuwezesha mfumo wa utekelezaji , kuwa na takwimu jumuishi, mfumo wa utawala na kutekeleza mipango dhidi ya mabadikiko ya tabianchi mwaka 2020.
Na tatu Guterres amesema ni “hatua za watu”ambapo ametoa wito kwa asasi za kiraia , mashirika ya mashinani, vyombo vya habari, sekta binafsi, vyanma vya ushirika, wanazuoni, na wengineo kuhakikisha ushirikiano ambao haujawahi kushuhudiwa.
Pia ametoa wito kwa ulimwengu wa sayansi, utafiti, na teknolojia kuhakikisha kwamba teknolojia mpya inaziba pengo la kidijitali na kupanua wigo wa teknolojia katika kuelekea kwenye lengo zuri la pamoja likizingatia mapendekezo ya jopo la ngazi ya juu la Umoja wa Mataifa kuhusu mwasuala ya kidijitali Amewataka pia vijana na asasi za kiraia kuwawajibisha viongozi wao. “Tunahitaji kila mtu kuchakarika, tunahitaji kusonga kwa pamoja na kutomuacha yeyote nyuma. Tutumie fursa ya wiki hii na mikutano hii kuchochea hama yetu ya pamoha ya kusonga mbele”