Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Majaji wa ICC watangaza hati za kukamatwa kwa waliokuwa viongozi wawili wa jeshi la Urusi

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC mjini The Hague Uholanzi
UN Photo/Rick Bajornas
Mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC mjini The Hague Uholanzi

Majaji wa ICC watangaza hati za kukamatwa kwa waliokuwa viongozi wawili wa jeshi la Urusi

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Tarehe 24 Juni 2024, Chemba namba mbili ya Utangulizi ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, ilichoundwa na Jaji Rosario Salvatore Aitala, Jaji Sergio Gerardo Ugalde Godínez na Jaji Haykel Ben Mahfoudh, kimetoa hati ya kukamatwa kwa kwa watu wawili, Sergei Kuzhugetovich Shoigu na Valery Vasilyevich Gerasimov, katika muktadha wa hali ya Ukraine kwa madai ya uhalifu wa kimataifa uliofanywa kuanzia tarehe 10 Oktoba 2022 hadi Machi 9, 2023.

Bwana Shoigu, aliyezaliwa tarehe 21 Mei 1955, Waziri wa Ulinzi wa Shirikisho la Urusi wakati wa matukio anayoshitakiwa kwayo, na Bwana Gerasimov, aliyezaliwa Septemba 8, 1955, Mkuu wa Wafanyakazi wa Majeshi ya Urusi ambaye pia alikuwa Naibu Waziri wa Kwanza wa Ulinzi wa Shirikisho la Urusi wakati wa matukio hayo anayotuhumiwa kwako, kila mmoja anadaiwa kuwajibika kwa uhalifu wa kivita wa kuelekeza mashambulizi kwa miundombinu ya kiraia (kifungu cha 8(2)(b)(ii) cha Mkataba wa Roma) na uhalifu wa kivita wa kusababisha madhara makubwa kupita kiasi kwa raia au uharibifu wa miundombinu ya kiraia (kifungu cha 8(2)(b)(iv) cha Mkataba wa Roma), na uhalifu dhidi ya ubinadamu wa vitendo visivyo vya kibinadamu chini ya kifungu cha 7(1)(k) ya Mkataba wa Roma

Hati hizo mbili za kukamatwa zilitolewa kufuatia maombi yaliyowasilishwa na Upande wa Mashtaka. Chemba ya Utangulizi ya II ya mahakama imeona kwamba kuna sababu za kuridhisha za kuamini kwamba watuhumiwa hao wawili wanawajibika kwa mashambulizi ya makombora yaliyofanywa na jeshi la Urusi dhidi ya miundombinu ya umeme ya Ukraine kuanzia angalau tarehe 10 Oktoba 2022 hadi angalau 9 Machi 2023. Katika kipindi hicho mashambulizi mengi dhidi ya mitambo mingi ya umeme na vituo vidogo yalifanywa na vikosi vya jeshi la Urusi katika maeneo mengi nchini Ukraine.