Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICJ yaamua Urusi ikomeshe operesheni zake za kijeshi Ukraine

Ndani mwa mahakama ya kimataifa ya ICJ
UN Photo/ICJ-CIJ/Frank van Beek
Ndani mwa mahakama ya kimataifa ya ICJ

ICJ yaamua Urusi ikomeshe operesheni zake za kijeshi Ukraine

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Urusi isitishe operesheni zake za kijeshi nchini Ukraine, imesema Mahakama ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki, ICJ katika uamuzi wake iliyotoa leo huko The Hague, nchini Uholanzi.

 

Majaji 13 kati ya 15 wa mahakama hiyo waliunga mkono ombi la Ukraine kutaka Urusi isitishe operesheni zake ilhali majaji wawili, Makamu wa Rais wa ICJ Kirill Gevorgian ambaye ni Mrusi na Jaji Xue Hanging  kutoka China wakipinga ombi hilo.

Uamuzi huu wa Mahakama, wa kwanza kutolewa na mahakama hiyo ya kimataifa tangu Urusi ivamie Ukraine tarehe 24 mwezi uliopita wa Februari, unafuatia ombi la Ukraine la tarehe 27 mwezi uliopita kwa mahakama hiyo ya kimataifa ya haki ya kushutumu Urusi kutumia kisingizio cha mauaji ya kimbari kuhalalisha uvamizi wake wa kijeshi.

Ijapokuwa uamuzi wa ICJ una mashiko, ripoti zinahoji iwapo Urusi itazingatia uamuzi huo, na Mahakama hiyo haina njia ya moja kwa moja ya kuutekeleza.

Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Umoja wa Mataifa, Joan E. Donoghue ambaye amesoma leo hukumu ya ICJ ya shauri la Ukraine dhidi ya Urusi.
UN /ICJ-CIJ/Frank van Beek
Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Umoja wa Mataifa, Joan E. Donoghue ambaye amesoma leo hukumu ya ICJ ya shauri la Ukraine dhidi ya Urusi.

Mwenendo wa kesi

Mahakama ilianza kwa kurejelea kuwa tarehe 26 mwezi Februari 2022, Ukraine iliwasilisha ombi dhidi ya Urusi kuhusu hoja  ya tafsiri, matumizi na kukidhi matakwa ya Mkataba wa kimataifa kuhusu mauaji ya kimbari.

Ukraine ilieleza kuwa baada ya madai ya uongo ya vitendo vya mauaji ya kimbari dhid iya wakazi wa maeneo ya Luhansk na Donetsk , Urusi imetangaza na kutekeleza operesheni maalum za kijeshi ili kuzuia adhabu dhidi ya madai yake hayo.

ICJ ilitaka Urusi kusitisha mara moja mashambulizi yake na kuacha operesheni zote za kijeshi kwa kuwa yalizingatia malengo yake misingi yake ni kuzuia au kuadhibu Ukraine kwa kutekeleza mauaji ya kimbari.

Mahakama pia imesema kuwa Urusi imekataa kushiriki kwenye mchakato wa kesi hiyo na baadaye iliwasilisha nyaraka kuwa kwa kesi hiyo , ICJ inakosa mamlaka na uhalali wa kuisikiliza na hivyo kuitaka mahakama ijizuie kushiriki katika kutoa uamuzi wowote na hivyo iondoe shauri hilo mahakamani.

Vigezo vimekidhi

Akiwasilisha uamuzi wa mahakama, Rais wa ICJ Jaji Joan E. Donoghue kutoka Marekani alisema mazingira sahihi yalikidhi kuipatia Mahakama mamlaka ya kutoa uamuzi; Haki zilizosisitizwa na Ukraine zina mashiko; hakuna mauaji ya kimbari yaliyotekelezwa.

“Bila shaka, operesheni yoyote ya kijeshi, hususan ila inayofanyika katika kiwango kinachotekelezwa na Urusi kwenye eneo la Ukraine, linasababisha vifo, linaleta madhara ya mwili na akili, na inaharibu mali na mazingira,” amesema Rais huyo wa ICJ.

Amesema ICJ inaona kuwa wananchi wanaoathiriwa na vita vya sasa ni wale walio hatarini zaidi na kwamba “uvamizi wa Urusi umesababisha vifo vya mamia ya rai ana wengine wamejeruhiwa, mali zimeharibiwa ikiwemo uharibifu wa majengo na miundombinu.”

Kwa kauli moja hata hivyo majaji walikubaliana kuwa pande zote kwenye mzozo huo zijizuie kufanya kitendo chochote kinachoweza kuchochea zaidi mzozo wa sasa au kufanya hali kuwa ngumu zaidi kupata suluhisho.

Pata muhtasari wa uamuzi wa mahakama hapa.