Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNFPA: Waliopona Fistula nchini Burundi wasaidia kuelimisha wengine

Donavine Ndayikengurukiye, mwanamke mwenye umri wa miaka 23, alikuwa na umri wa miaka 19 wakati ujauzito wake ulisababisha fistula ya uzazi.
© UNFPA Burundi
Donavine Ndayikengurukiye, mwanamke mwenye umri wa miaka 23, alikuwa na umri wa miaka 19 wakati ujauzito wake ulisababisha fistula ya uzazi.

UNFPA: Waliopona Fistula nchini Burundi wasaidia kuelimisha wengine

Afya

“Nilipopata uchungu wa kujifungua, mama mkwe wangu na mama yangu mzazi walikataa kuniruhusu niende kujifungulia katika kituo cha afya” Gloriose Mbonimpa ameliambia Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya afya ya uzazi na idadi ya watu duniani UNFPA.

Bi. Mbonimpa ambaye enzi za ujana wake alikumbwa na tatizo la Fistula ya uzazi anaeleza kuwa alihisi kifo kinakaribia siku aliyoshikwa na uchungu wa kujifungua, alipiga kelele kuita majirani zake kwa msaada, walijaribu kumpeleka kwenye kituo cha matibabu lakini haikuwa heri kwake, alijifungulia njiani mtoto akiwa amefariki, na kupata fistula ya uzazi katika mchakato huo.

Fistula ya uzazi ni majeraha ya kujifungua ambayo husababishwa hasa na uzazi uliokwamishwa kwa muda mrefu. 

Duniani kote, majeraha haya huathiri karibu nusu milioni ya wanawake na wasichana hasa wale ambao wanakosa upatikanaji wa haraka na wenye ubora wa juu wa huduma ya msaada matibabu.

Matokeo ya ugonjwa wa fistula kwa mhanga yanaweza kuwa mabaya kwani mara nyingi hawaheshimiki katika jamii na hutengwa pamoja na kuwa na umasikini wa kiwango cha juu.

Unyanyapaa

“Wanawake katika wodi ya uzazi waliniomba niondolewe katika wodi hiyo kwasababu nilikuwa nikilowanisha kitanda, mbali na maumivu ya kupoteza mtoto, nilikuwa sielewi nini kinanitokea katika Maisha yangu” Donavine Ndayikengurukiye, mwanamke mwingine aliyepona fistula, aliliambia UNFPA.

Kutokana na aibu aliyoipata kutokana na Fistula, mume wa Bi. Mbonimpa alimtelekeza kwa sababu ya kushindwa kuvumilia hali hiyo. “Nilikuwa natoa harufu isiyovumilika, hakuna anayestahili kupitia haya” alisema Bi. Mbonimpa

Fistula inatibika, licha ya hayo, utafiti unaonesha kuwa wahanga wengi hawajui kuwa upasuaji unaweza kusaidia kuponya majeraha hayo.

Mwanzoni, Bi. Ndayikengurukiye alikuwa mmoja wao, lakini kugundua kwake kuwa anaweza kupona ikaleta tabasamu mpya usoni mwake.

Nchini Burundi, kituo kimoja cha afya, kituo cha Urumuri kilichoko katika mji mkuu wa Burundi, Bujumbura, kina vifaa vya kushughulikia wagonjwa wa fistula. 

Kati ya mwaka 2010 na 2023, wanawake takribani 3,000 walifanyiwa upasuaji wa kurekebisha hali zao kituoni hapo. Bi. Mbonimpa alikuwa mmoja wao. 

Mwaka 2022, alitafuta matibabu katika kituo hicho wakati wa kampeni iliyoungwa mkono na UNFPA iliyotoa fursa ya huduma bure kwa wahanga wa ugonjwa wa fistula.

Wanawake walio katika umri wa kubalehe wanaweza kuwa katika hatari ya kupata fistula, kwani mifupa yao ya nyonga haijakomaa vya kutosha kwaajili ya kujifungua.

“Nadhani nilipata hii fistula kwasababu nilijifungua nilipokuwa mdogo sana” Bi. Ndayikengurukiye aliliambia UNFPA

Ni miaka 23 sasa Bi. Ndayikengurukiye anaishi bila fistula, akiwa ni mama wa msichana mdogo ambaye alizaliwa baada ya kupona kwake, tangu wakati huo, yeye na mumewe wamekubali kufuata huduma ya uzazi wa mpango.

“Mume wangu na mimi tulichagua uzazi wa mpango ili mwili wangu upate kupumzika kutoka katika hatari ya kupata fistula ya uzazi nyingine, na kusubiri msichana wetu mdogo aweze kukua kidogo”