Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO waboresha kitabu cha muongozo wa uzazi wa mpango

Mshauri wa kike anamuonyesha mwanamke njia za kupanga uzazi katika kituo cha afya huko Sulawesi Kusini, Indonesia.
© UNICEF/Shehzad Noorani
Mshauri wa kike anamuonyesha mwanamke njia za kupanga uzazi katika kituo cha afya huko Sulawesi Kusini, Indonesia.

WHO waboresha kitabu cha muongozo wa uzazi wa mpango

Wanawake

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani WHO hii leo limetoa maboresho muhimu kwenye Kitabu chake cha kihistoria cha Uzazi wa mpango, ambacho kinawapa watunga sera na wafanyakazi wa sekta ya afya taarifa mpya za kuweza kufanya machaguo kuhusu dawa za uzazi wa mpango.

Kitabu hicho cha Mwongozo chenye maboresho kimetolewa leo katika mkutano wa Kimataifa wa Uzazi wa Mpango huko Pattaya, Thailand.

Uzalishaji wa kitabu hicho umetolewa kwa ushirikiano wa Shule ya Afya ya Umma katika chuo cha Johns Hopkins Bloomberg na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani USAID.

Dkt. Mary Gaffield, Mwanasayansi na mwandishi mkuu wa Kitabu hicho amesema huduma za uzazi wa mpango zinaweza kutolewa kwa usalama na kwa gharama nafuu ili bila kujali watu hao wanaishi wapi, wanandoa au watu binafsi waweze kuchagua njia salama na bora za kupanga uzazi.

“Mapendekezo yaliyosahihishwa katika Kitabu hiki yanaonesha karibu njia yoyote ya upangaji uzazi inaweza kutumika kwa usalama na wanawake wote. Wanawake wote wanapaswa kupata chaguzi mbalimbali zinazokidhi mahitaji na malengo yao ya kipekee maishani.” Amesema Dkt. Gaffield

 

Walichojifunza kwenye majanga

WHO wameeleza kutokana na mambo waliyojifunza kutokana na milipuko ya hivi karibuni, toleo hili jipya linaeleza hatua zinazoonekana kwa wahudumu wa afya walio mstari wa mbele kulinda upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango wakati wa dharura, kama vile upatikanaji mpana wa vidhibiti mimba vinavyojitegemea na matumizi ya teknolojia ya kidijitali na watoa huduma.

Mkurugenzi wa Afya na Haki za Uzazi wa WHO Dkt. Pascale Allotey anasema kitabu hicho ni nyenzo muhimu, kusaidia wafanyakazi wa afya kusaidia watumiaji wa uzazi wa mpango ulimwenguni kote katika kufanya maamuzi sahihi kuhusu chaguo sahihi za uzazi wa mpango kwao.

“Uzoefu kutoka kwa milipuko ya hivi majuzi unaonesha kuwa huduma za upangaji uzazi zinaweza kuathiriwa sana wakati wa dharura. Wakati wa awamu za awali za janga la COVID-19 mnamo 2020, takriban asilimia 70 ya nchi ziliripoti kukatizwa kwa huduma hizi muhimu na kuongeza hatari za mimba zisizotarajiwa na magonjwa ya zinaa.”

 

Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) linatoa elimu kuhusu upangaji uzazi kwa wakimbizi wa ndani walio katika jimbo la Kasai nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC
© UNFPA DRC
Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) linatoa elimu kuhusu upangaji uzazi kwa wakimbizi wa ndani walio katika jimbo la Kasai nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC

Kujidunga binafsi

Vidhibiti mimba vinavyojitegemea kama vile kondomu, tembe za kuzuia mimba, dawa za kuua manii , chaguo la kujidunga kidhibiti mimba chenye projestini pekee, kiitwacho DMPA, ambacho sasa kinaweza kuwekwa kwa usalama chini ya ngozi badala ya kuingia kwenye misuli ya mwili.

Wanawake wengi wanapendelea uzazi wa mpango wa kibinafsi na usioingiliwa ambao unahitaji hatua tu kama mbili hadi tatu na kufanya chaguo hili kuwa na uwezekano wa kuongeza matumizi

 

Kuhusu UKIMWI

Kwa mara ya kwanza, toleo hili la mwaka 2022 linajumuisha sura maalum ya kuongoza huduma za uzazi wa mpango kwa wanawake na vijana walio katika hatari kubwa ya kuambukizwa UKIMWI VVU, ikiwa ni pamoja na watu wanaoishi katika maeneo yenye maambukizi ya VVU na wale walio na wapenzi wengi wa wanashiriki ngono au ambao mpenzi wao wa kawaida anaishi na VVU.

Ingawa kondomu pekee hulinda dhidi ya VVU na magonjwa mengine ya zinaa, njia zote za uzazi wa mpango isipokuwa tu ya nonoxynol-9 spermicide sasa zinachukuliwa kuwa salama kwa wanawake na vijana walio katika hatari kubwa ya VVU kwa vile hazijapatikana kuongeza hatari ya maambukizi ya VVU.

Kwa wale walio katika hatari kubwa ya kuambukizwa VVU, mwongozo huo unasema kuwa upimaji, ushauri nasaha na utunzaji wa kimatibabu wa kwanza na rufaa zinapaswa kutolewa kama sehemu ya huduma za uzazi wa mpango.

 

Kuhusu Saratani

Kitabu hiki pia kinajumuisha mwongozo wa hivi karibuni wa WHO kuhusu saratani ya shingo ya kizazi na uzuiaji wa mapema wa saratani, uchunguzi na matibabu, ambayo yote yanaweza kutolewa kupitia huduma za kupanga uzazi, udhibiti wa magonjwa ya zinaa; na kupanga uzazi katika utunzaji baada ya kuharibika kwa mimba.

Sasa katika toleo lake la nne, kijitabu hiki ndicho mwongozo wa marejeo unaotumika zaidi juu ya mada hii duniani kote, na zaidi ya nakala milioni moja zimesambazwa au kupakuliwa kutoka mtandaoni hadi sasa.

Kusoma kitabu hicho ambacho kimetengenezewa App yake bofya hapa.