Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Simulizi ya Jacqueline: Kuacha shule, kupata ujauzito, kupata fistula na kupona

Jacqueline alipata fistula ya uzazi alipojifungua akiwa na umri wa miaka 16.
© UNFPA Malawi
Jacqueline alipata fistula ya uzazi alipojifungua akiwa na umri wa miaka 16.

Simulizi ya Jacqueline: Kuacha shule, kupata ujauzito, kupata fistula na kupona

Afya

Binti Jacqueline, raia wa nchini Malawi alikuwa na umri wa miaka 15 alipozama kwenye dimbi la mapenzi na kijana kutoka kijiji kingine. Wawili hao walitoroka nyumbani na kwenda kuishi kinyumba badala ya kufunga ndoa rasmi. 

Mama yake Jacqueline Margaret Kumwenda alikuwa hafahamu lolote kuhusu uhusiano huo kutokana na kufichwa na binti yake japokuwa alikuwa na wasiwasi kutokana na tabia ya binti yake kubadilika na kuwa anatoweka mara kwa mara. 

Bi.Kumwenda alipopata habari za kutoroshwa kwa binti yake alikasirika, alienda kituo cha polisi kuomba wamchukulie hatua kijana aliyemtorosha binti yake. "Waliniambia kwamba alikuwa bado mtoto, na walichoweza kufanya ni kumshauri yeye na Jacqueline," alisema wakati anazungumza na shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na afya ya uzazi na idadi ya watu UNFPA.

Ushauri huo ulifanya kazi kwa muda. Jacqueline, ambaye sikuzote alikuwa mwanafunzi mwenye bidii, alirejea kuweka mkazo kwenye masomo. Na mama yake alitarajia bintiye angemaliza elimu yake kabla ya kujitumbukiza kwenye masuala ya mahusiano.

Maisha ya kijijini

Katika kijiji anachoishi Jacqueline kiwango cha wanafunzi kuacha shule ni kikubwa na miongoni mwa sababu ni umbali wa shule ilipo, madhalani Jacqueline hutumia mwendo wa saa moja kwenda shuleni. 

Suala jingine ni ndoa za utotoni ambazo zimekuwa ni suala la kawaida kwa wasichana barubaru ambao huwa na taarifa kidogo hukusu afya ya uzazi na ngono pamoja na haki zao. 

Bila ya kuwa na matumaini ya maisha tofauti ya baadaye, Jacqueline, pia, aliamua kuacha shule. 

Siku moja alifunga vitu vyake na kukimbia na mumewe na kuhamia Wilaya ya Mzimba nchini humo Malawi.

"Tulijaribu kumtafuta, lakini hatukufanikiwa," Mama yake Bi. Kumwenda alisema.

Maumivu ya kujifungua na kutelekezwa

Baada ya kuanza maisha mapya huko wilayani Mzimba, Jacqueline alipata ujauzito na, akiwa na umri wa miaka 16, alipata uchungu wa kujifungua na kwenda katika kituo cha afya kilichopo eneo alilokuwa akiishi.

Hali haikuwa nzuri, alishindwa kujifungua kwa haraka, uchungu ilikuwa wa muda mrefu, na kumsababishia fistula ya uzazi - jeraha la kiwewe la kuzaa ambalo shimo limepasuka kwenye njia ya uzazi. 

Wasichana hususan barubaru, wako katika hatari ya kupata changamoto wakati wa kujifungua kwa kupata uchungu wa muda mrefu pamoja na fistula ya uzazi.

Hatimaye Jacqueline alijifungua mtoto wa kike. Mtoto huyo alikuwa na hali njema siku zilizofuata, lakini Jacqueline hakuwa sawa. Kama ilivyo kwa waathirika wengi wa fistula, alianza kuvuja kinyesi na mkojo, na majeraha yake yakashindwa kupona.

“Maisha yangu yalikuwa ya upweke kwani sikuweza kutoka nje ya nyumba kwa sababu nilikuwa najilowesha," Jacqueline aliwasimulia UNFPA. 

Hali iliendelea kuwa hivyo, kwa miezi kadhaa alitengwa, alikuwa anakaa ndani tu kutokana na jeraha la Fistula.

Siku moja, mume wake aliamua kumfukuza. Cha kusikitisha ni kwamba, kuachwa na mke au mume au familia ni jambo la kawaida miongoni mwa waathirika wa fistula. 

Kwa kuogopa kuwasiliana na mama yake Jacqueline Bi Kumwenda moja kwa moja, mvulana huyo alituma ujumbe kama mtu asiyejulikana kwa njia ya sauti: Binti yako hayuko sawa na anataka kurudi nyumbani.

Kuungana ten ana binti yake lilikuwa suala la uchungu sana kwa Bi.Kumwenda. Alifarijika kuwa na binti yake nyumbani, na alifurahi sana pia kukutana na mjukuu. Wakati huo huo, hali ya binti yake ilimhuzunisha.

“Sikujua la kufanya,” alisema Bi Kumwenda.

Margaret Kumwenda (kushoto) hakukata tamaa kwa bintiye.
© UNFPA Malawi
Margaret Kumwenda (kushoto) hakukata tamaa kwa bintiye.

Haki za binadamu ziko hatarini

Fistula ya uzazi sio tu suala la afya, bali pia ni suala la haki za binadamu.

Fistula isiyotibiwa inaweza kusababisha magonjwa makubwa ya kimwili na pia maambukizi ya mara kwa mara na mama aliyepata Fistula ana uwezekano wa kutokuwa na uwezo wa kuzaa tena. 

Katika sehemu nyingi za dunia, fistula ya uzazi inaweza kuzuilika kwa kupata huduma ya dharura ya uzazi kwa kawaida sehemu ya upasuaji.

Kwa sasa hali hii inawaathiri wanawake na wasichana walio katika mazingira magumu zaidi: wale ambao hawana uwezo mdogo wa kupata elimu ya kina ya kujamiiana ambayo itawawezesha kuzuia mimba za utotoni, wale wanaopata ndoa za utotoni, na wale ambao hawana huduma ya mkunga mwenye ujuzi na hali ya dharura, huduma wakati wa kujifungua.

Athari za ugonjwa wa fistula zinazidisha ugumu wa maisha ya wanawake na wasichana. Wanapata unyanyapaa, ubaguzi kutoka kwa jamii, familia na waajiri, na mara nyingi madhara ya kudumu ya kisaikolojia.

Sportlight imerudisha matumaini kwa Jacqueline 

Waswahili husema uchungu wa mwana aujuae mamaye na hivyo hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Bi kumwenda hakutaka kukata tamaa. “Nilikumbuka kwamba kulikuwa na mwanamke katika jumuiya yetu ambaye alizungumza kila mara kuhusu hali kama hiyo, na jinsi anavyoweza kusaidia kutibiwa,”.

Mwanamke huyo alikuwa balozi wa fistula wa Spotlight Initiative, - ambao ni mpango wa usawa wa kijinsia unaofadhiliwa na Muungano wa Ulaya na kutekelezwa na UNFPA na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa. “Alikubali kuja nyumbani kwetu siku iliyofuata,” Bi. Kumwenda alisema.

Mara moja binti yake Jacqueline alipewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Wilaya ya Nkhata Bay, na kutoka hapo alipangiwa kufanyiwa upasuaji katika kituo cha afya cha wilaya, kinachofadhiliwa na Mpango wa Spotlight.

“Sijui ni nini kingetokea kama nisingekuja hapa,” alisema Jacqueline alipokuwa hospitalini, baada ya kufanyiwa upasuaji na kukarabatiwa jeraha lake la fistula.

UNFPA na Spotlight pia zinafanya kazi na jumuiya ya eneo hilo kushughulikia sababu kuu za fistula ya uzazi. Kwa pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Nkhata Bay, wanawawezesha wanawake na wasichana kupata uelewa kuhusu afya ya uzazi na haki za uzazi.

Kuhusu Jacqueline, sasa amepona na anaweza kufikiria kuhusu maisha yake ya baadaye na ya binti yake wa miaka miwili - na ana mifano mingine mipya yenye nguvu. "Ninawashukuru wale walionisaidia kupona tena," alisema.