Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa umesisitiza ahadi ya kuujenga upya mji wa Kharkiv Ukraine

Shambulio dhidi ya eneo la makazi ya watu huko Kharkiv nchini Ukraine Jumamosi ya tarehe 25 Mei, 2024
Ujumbe wa Kibinadamu Proliska
Shambulio dhidi ya eneo la makazi ya watu huko Kharkiv nchini Ukraine Jumamosi ya tarehe 25 Mei, 2024

Umoja wa Mataifa umesisitiza ahadi ya kuujenga upya mji wa Kharkiv Ukraine

Amani na Usalama

Mji wa Kharkiv nchini Ukraine umeathiriwa vibaya na vita inayoendelea na unakabiliwa na uharibifu mkubwa wa miundombinu na janga la kibinadamu.

Mkutano wa ujenzi mpya wa Ukraine unaofanyika huko Berlin nchini Ujerumani unasaka kuongeza msaada wa kimataifa kwa ajili ya ujenzi huo mpya na Tume ya kiuchumi ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Ulaya UNECE inaongoza juhudi hizo na ikikadiria kuwa dola bilioni 10 zinahitajika kwa ajili ya ujenzi huo.

Kharkiv ni mji wa pili kuwa na watu wengi nchini Ukraine na uko kilomita 30 tu kutoka mpaka na Urusi, ni miongoni mwa maeneo ya mijini yaliyoathiriwa zaidi na vita huku hivi karibuni ukikumbwa na milipuko mipya ya mabomu.

Meya wa mji huo Ihor Terekhov amebainisha kuwa wakazi 150,000 kati ya milioni 1.3 wa jiji hilo kwa sasa hawana makazi, huku takriban nyumba 9,000 zikiharibiwa vibaya tangu kuanza kwa vita.

Hali baada ya shambulio la Kharkiv Ukraine mwezi Mei (Kutoka Maktaba)
© IOM
Hali baada ya shambulio la Kharkiv Ukraine mwezi Mei (Kutoka Maktaba)

Uharibifu mkubwa huko Kharkiv

Uharibifu huo pia umeathiri vituo 110 vya kulelea watoto wadogo na shule 130, nusu ya taasisi za elimu za jiji hilo, pamoja na mitambo yote ya nishati ya kusha nyumba joto, vituo vya kubadilisha transfoma, taasisi 88 za matibabu na majengo 185 ya huduma za kijamii.

Wakati mzozo ukiendelea kongamano la ujenzi mpya wa Ukraine limewaleta pamoja serikali, watendaji wa kimataifa na wa ndani, na UNECE mjini Berlin katika mkutano utakaomalizika leo ili kurejesha ahadi zao za kumsaidia na kuunga mkono Kharkiv.

Mazungumzo hayo yanalenga kuunganisha juhudi kati ya serikali ya Ukraine, mashirika ya Umoja wa Mataifa na mameya ili kukabiliana na changamoto kubwa za ujenzi na ukarabati wa jiji hilo.

Mtoto mvulana mjini Kharkiv akiwa ameketi katika bango linalosema mabomu ya kutegwa ardhini ni hatari
© UNICEF/Olena Hrom
Mtoto mvulana mjini Kharkiv akiwa ameketi katika bango linalosema mabomu ya kutegwa ardhini ni hatari

Dola bilioni 10 zahitajika kwa ujenzi mpya wa jiji la Kharkiv

Katibu Mtendaji wa UNECE Tatiana Molcean ametangaza upanuzi wa mpango wa UN4UkrainianCities kusaidia ujenzi wa Kharkiv, unaofadhiliwa na Wizara ya Shirikisho la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Ujerumani. 

UNECE, mwanzilishi katika upangaji wa ujenzi mpya wa jiji hilo, umeweka kazi yake kwenye mpango mkuu uliotengenezwa na Wakfu wa Norman Foster.

Juhudi hizi ni pamoja na mpango kamili waujenzi mpya na mpango wa ukarabati wa mji wa Kharkiv, pamoja na mkakati wa kiuchumi uliotayarishwa na wataalamu kutoka vyuo vikuu vya Harvard na Oxford.

Meya Ihor Terekhov anakadiria kuwa karibu dola bilioni 10 za Kimarekani zitahitajika kwa ujenzi mpya wa mji huo.

UNICE inapanua wigo wa msaada katika ngazi ya kitaifa kwa ajili ya kuandaa sheria mpya ya sera ya makazi, ambayo inatarajiwa kuwasilishwa bungeni mwezi Julai mwaka huu 2024. 

Msaada huu pia unahusu maendeleo ya mijini ya Ukraine, kuhamasisha kundi la kimataifa la wataalam katika ushauri.

Muhudumu wa misaada akimsajili mmoja wa wakimbizi wa ndani kupokea msaada wa fedha taslim Kharkiv
© OCHA/Tanya Lyubimova
Muhudumu wa misaada akimsajili mmoja wa wakimbizi wa ndani kupokea msaada wa fedha taslim Kharkiv

Migogoro katika kanda

Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, maelfu ya watu walihamishwa kutoka miji iliyo katika maeneo ya mpaka wa eneo la Kharkiv na mamlaka ya Ukraine kwa msaada wa wahudumu wa kujitolea na mashirika ya kibinadamu.

Wengi wa watu waliohamishwa ambao walilazimika kukimbia makazi yao waliondoka na mali chache tu, na  wako katika hatari kubwaikiwa ni pamoja na wazee na watu wenye ulemavu mdogo au walemavu kabisa ambao hawakuweza kukimbia hapo awali.

Kulingana na wanasaikolojia wanaofanya kazi na UNHCR, watu wengi wanakabiliwa na msongo wa mawazo. 

Ili kupokea na kusaidia watu wengi walio katika hatari kubwa ya kufurishwa makwao, kituo cha usafiri kilianzishwa mara moja katika jiji la Kharkiv na mamlaka na mashirika ya kibinadamu.

Walisajiliwa kama wakimbizi wa ndani, walipokea aina tofauti za msaada wa kibinadamu kama vile misaada ya msingi, msaada wa kisaikolojia na wa kisheria, walijiandikisha kwa usaidizi wa pesa taslimu na walishauriwa juu ya chaguzi zinazopatikana za malazi.

Msaada kwa ajili ya watu waliofurushwa makwao Kharkiv
© UNICEF in Ukraine
Msaada kwa ajili ya watu waliofurushwa makwao Kharkiv

Ukimbizi wa ndani

Wengi wa waliofurushwa makwao walionyesha dhamira ya wazi ya kukaa na wanafamilia au katika makazi ya kukodisha na maeneo ya jumuiya huko Kharkiv na kutosonga mbali zaidi na nyumba zao, ili waweze kurudi wakati hali inaruhusu.

Wakati huo huo, watu zaidi wanaendelea kuzikimbia jumuiya zilizo mstari wa mbele wa vita katika mikoa ya Donetsk, Sumy, Zaporizhzhia na Kherson kuelekea mikoa ya kati na magharibi.

Mamlaka zinazoongoza harakati hizo zinaomba msaada ili kusaidia kupokea na kusaidia wakimbizi wa ndani. 

UNHCR inasema inawezekana kwamba idadi ya watu waliofurushwa makwao na waliohamishwa itaongezeka katika wiki na miezi ijayo ikiwa mashambulizi ya anga yataendelea na kwa kutarajia miezi ya msimu wa baridi.

UNHCR ina wasiwasi hasa kuhusu msimu wa baridi, kwani mahitaji yatakuwa makubwa nchini Ukraine kutokana na uharibifu wa miundombinu ya nishati, pamoja na mashambulizi dhidi ya makazi katika maeneo ya mstari wa mbele na dhidi ya vituo vya makazi ya mijini.