Urusi yatumia mabomu ya mnyumbuliko kwenye makazi ya rais Ukraine- Bachelet

30 Machi 2022

Taarifa za uhakika zinadokeza kuwa tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine tarehe 24 mwezi uliopita, majeshi ya Urusi yameangusha zaidi ya mara 20 mabomu yanayonyumbulika katika makazi yenye watu wengi, amesema hii leo huko Geneva Uswisi, Michelle Bachelet ambaye ni Kamishna Mkuu wa  Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu.
 

Akihutubia mkutano wa 49 wa Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu, Bi. Bachelet amesema “kwa zaidi ya mwezi mzima sasa maisha ya mamilioni ya raia yako mashakani kwa kuwa wanalazimika kukimbia makazi yao au kujificha kwenye mahandaki na makazi mengineyo salama kwa kuwa miji yao inashambuliwa na kuharibiwa”

Pamoja na ripoti hiyo, Kamisha huyo amesema ofisi yake pia inachunguza madai ya kwamba Ukraine nayo imetumia silaha za aina hiyo.

Wajumbe wa jopo la uchunguzi Ukraine watajwa

Wakati huo huo, Baraza hilo la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu hii leo  limetangaza jopo la watu watatu litakalounda Tume Huru ya kuchunguza madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Ukraine.

Wajumbe hao ni  Erik Møse wa Norway ambaye pia atakuwa Mwenyekiti, Jasminka Džumhur wa Bosnia na Herzegovina na Pablo de Greiff kutoka Colombia.

Jukumu la jopo hilo lililoundwa kufuatia azimio la Baraza hilo tarehe 4 mwezi Machi mwaka huu ni pamoja na kuchunguza madai yote ya ukiukwaji wa haki na unyanyasaji unaofanywa wakati huu wa uvamizi wa kijeshi wa Urusi nchini Ukraine pamoja na uhalifu mwingine unaohusiana nao.

Misafara ya misaada imewasili

Takribani wiki tano tangu kuanza kwa vita nchini Ukraine, shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Ulimwenguni, WFP hii leo mjini Lviv, Ukraine, limeeleza kuwa limewafikishia msaada wa chakula cha kuokoa maisha watu milioni moja nchini humo. 

Shirika hilo limesambaza mikate iliyookwa kwa familia katika mji wa Kharkiv, msaada wa pesa taslimu kwa watu waliokimbia makazi yao mjini Lviv na chakula kilicho tayari kuliwa katika maeneo mbalimbali ya nchi. 

Chakula cha dharura cha WFP pia kimefika katika maeneo yenye migogoro ya Sumy na Kharkiv kupitia misafara miwili ya mashirika ya misaada ya kibinadamu. Mafanikio haya yanakuja licha ya hali tete ya usalama, ugumu wa kupata wadau mashinani wa kushirikiana nao, na changamoto za kuwahudumia watu wanaohamahama.

Malori, treni na mabasi madogo yanatumika hii leo kusambaza vyakula kwa wale walio hatarini zaidi na misafara mingine yenye misaada ya dharura inatarjiwa kuwasili kwenye maeneo hayo, imesema WFP.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter