Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukraine: Hofu yangu ni mume wangu- Nataliia

Nataliia Vladimirova na binti yake Oleksandra au Sasha kwenye umri wa miaka 4 wakiwa mjini Lisbon ,Ureno ambako waliwasili tarehe 14 Machi 2022 wakikimbia vita nchini mwao Ukraine
UN News/Leda Letra.
Nataliia Vladimirova na binti yake Oleksandra au Sasha kwenye umri wa miaka 4 wakiwa mjini Lisbon ,Ureno ambako waliwasili tarehe 14 Machi 2022 wakikimbia vita nchini mwao Ukraine

Ukraine: Hofu yangu ni mume wangu- Nataliia

Msaada wa Kibinadamu

Nataliia Vladimirova alikimbia nyumbani kwake Kharkiv, Ukraine, siku ya kwanza tu Urusi  ilipovamia nchi yao tarehe 24 mwezi Februari, 2022, akiambatana na binti yake Oleksandra mwenye umri wa miaka 4 pamoja na mama mkwe wake. Wao ni miongoni mwa maelfu ya wakimbizi wa Ukraine waliopata hifadhi ya muda nchini Ureno . Akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa huko Ureno, Nataliia al maaruf Natasha, anasimulia simulizi wa yale aliyopitia ikiwemo kugawanyika kwa familia sambamba na kupoteza wengine. 
 

“Natoka Kharkiv, mji ambao hivi sasa ni hatari sana. Ni kitovu cha vita inayoendelea Ukraine. Leo ni siku yenye hisia sana kwangu, kwa sababu ni mwezi mmoja tangu nimeondoka nyumbani. Bado napata taswira ya nyumba yet una vitu vyetu tulivyoviacha.”

Kabla vita kuanza, nilipendekeza tuondoke nyumbani, lakini mume wangu alisema, “hapana! Hii ni karne ya 21 inawezekana vipi vita kutokea?”  Lakini penginepo nikawaza, nikaandaa nyaraka zetu. Kisha tarehe 24 mwezi Februari, mume wangu aliniamsha na kusema, “imeanza!”

Tulipoondoka mjini, hatukimbia kabisa Ukraine, kwa sababu tulidhania kuwa tungaliweza kurejea ndani ya siku chache.

Tuliishia kuhamahama kutoka mji mmoja hadi mwingine ndani ya Ukraine, ambako watu wengi walitusaidia. Kituo cha kwanza kilikuwa Dnipro, ambako wafanyakazi wenzake na mume wangu walituruhusu tuishi kwenye nyumba yao. Lakini tulisikia ving’ora baada tu ya siku ya kwanza, hivyo tukaamua kuendelea na safari.

Mume wangu alielezwa kuwa haruhusiwi kuondoka Ukraine, na hivyo aliniomba niondoke bila yeye. Nilimweleza kuwa nampenda na siwezi kumwacha nyuma. Hii ilikuwa ni Kryvyi Rih, na bado  yuko huko.

Nataliia Vladimirova na familia yake waliishi kwenye vituo kadhaa vya malazi huko Ukraine na Romania kabla ya kuingia Ureno.
Picha: Nataliia Vladimirova Personal Files.
Nataliia Vladimirova na familia yake waliishi kwenye vituo kadhaa vya malazi huko Ukraine na Romania kabla ya kuingia Ureno.

Faraja kusaidiwa na asiowafahamu

Lakini ilibidi niondoke. Nilimweleza kuwa amjulishe mama yake aondoke Kharkiv ili atukute Kryvyi Rih, kicha tulipanga kuondoka nchini Ukraine nikiambatana na mwanangu Oleksandra na mama mkwe wangu.

Kabla ya kuondoka Ureno, tuliendesha gari hadi mpakani mwa Ukraine na Romania na tukaingia Romania. Hatukumfahamu mtu yeyote pale na hivyo tukaomba chama cha msalaba mwekundu watusaidie.Wao walitupatia pahala pa kulala.

Walitusafirisha kwa gari hadi mji mkuu Bucharest, ambako walituandalia usafiri na wakimbizi wengine kutoka Ukraine tusafiri kwa ndege za huduma za kibinadamu hadi Ureno.

Tumesaidiwa na wafanyakazi wengi wa kujitolea njiani kote tulikopita. Nchini Romania, walituandalia staftahi, bila hata kudai malipo yoyote. Hapa Ureno, wafanyakazi wa kujitolea walitulaki uwanja wa ndege na kutusaidia kupata pahala pa kuishi.

Mwenyeji wetu mjini Lisbon, Ureno, Maria ni mtu mzuri na mwema sana. Ametuelezea yote kuhusu Ureno, na kile tunapaswa kufanya ili kupata shule kwa ajili ya binti yangu na pia jinsi ya mimi kupata ajira. Marafiki zake pia wametupatia nguo.

Ijapokuwa ana umri wa miaka minne tu, binti yangu anatambua kuwa kuna vita kubwa inaendelea nyumbani, yaani kuna ufyatuaji wa risasi. Amemuuliza nyanya yake, kwa nini babu hayuko hapa. Anaseba Babu lazima aje UReno kwa kuwa kinachoendelea Kharkiv ni hatari kubwa.

Hofu yangu kubwa zaidi ni kwamba sitaweza kumuona tena mume wangu.”