Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafuriko ya ghafla Afghanistan ni tishio kubwa kwa watoto: UNICEF

Nyanya ameketi na wajukuu zake watatu waliojeruhiwa kwa mafuriko ya ghafla yalipopiga kijiji chao katika jimbo la Baghlan, Afghanistan.
© UNICEF/Osman Khayyam
Nyanya ameketi na wajukuu zake watatu waliojeruhiwa kwa mafuriko ya ghafla yalipopiga kijiji chao katika jimbo la Baghlan, Afghanistan.

Mafuriko ya ghafla Afghanistan ni tishio kubwa kwa watoto: UNICEF

Tabianchi na mazingira

Makumi ya maelfu ya watoto nchini Afghanistan wbado wameathiriwa na mafuriko yanayoendelea, hususan katika majimbo ya kaskazini ya Baghlan na Badakhshan na mkoa wa Ghor magharibi mwa Afghanistan, limesema leo shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia watoto UNICEF na kukumbusha kuwa mafuriko katika nchi hiyo ya Asia ya Kati yanasababisha tishio la haraka na la kudumu kwa watoto.

Wakikabiliwa na tishio hilo UNICEF inatoa wito wa kuongezwa kwa uwekezaji katika kujiandaa na majanga na kmnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kwani mafuriko ya hivi karibuni yanatoa onyo kubwa la hatari zinazokuja ambazo zinazowezekana za mabadiliko ya tabianchi.

"Jumuiya ya kimataifa lazima iongeze juhudi na uwekezaji wake ili kusaidia jamii kukabiliana na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa watoto," amesema Dkt. Tajudeen Oyewale, Mwakilishi wa UNICEF nchini Afghanistan akioneza kuwa "Wakati huo huo, UNICEF na jumuiya ya kibinadamu lazima wajitayarishe kwa ukweli mpya, majanga yanayohusiana na tabianchi."

Zaidi ya nyumba 400 ziliharibiwa na mvua kubwa na mafuriko katika mkoa wa Ghor, Afghanistan, na kuacha mamia ya watoto bila nyumba au mali.
© UNICEF/Mark Naftalin
Zaidi ya nyumba 400 ziliharibiwa na mvua kubwa na mafuriko katika mkoa wa Ghor, Afghanistan, na kuacha mamia ya watoto bila nyumba au mali.

Takriban watu 350 wakiwemo makumi ya watoto wamepoteza maisha

UNICEF inasema mafuriko ya hivi karibuni yamegharimu maisha ya watu 350, wakiwemo watoto kumi na wawili. 

Pia zaidi ya nyumba 7,800 ziliharibiwa au kusambaratishwa, zaidi ya familia 5,000 zimelazimika kuyahama makazi yao. 

Dkt. Oyewale amesema "Mvua kubwa haipaswi kusababisha maafa  makuba ya mara moja kwa watoto wa Afghanistan".

Kufuatia mafuriko hayo Afghanista UNICEF mara moja ilisafirisha maji ya kunywa na kusambaza vifaa vya usafi. 

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa pia lilikusanya timu kliniki tembezi na lishe kuwatibu majeruhi na wagonjwa, na kutoa nguo za joto, mablanketi, vifaa vya nyumbani na vifaa vya kupikia kwa familia zilizopoteza mali zao.

UNICEF pia imetoa msaada wa haraka wa kifedha kupitia utaratibu wake wa kukabiliana dharura ili kusaidia familia kujikimu na kukidhi mahitaji yao ya msingi. 

"Lazima tutoe kipaumbele kwa mahitaji maalum ya watoto katika kufanya maamuzi na kushughulikia mahitaji haya sasa ili kuwalinda watoto kutokana na majanga yajayo huku tukiwekeza katika huduma za msingi wanazozitegemea," ameongeza Dkt. Oyewale.

Maandalizi makubwa ya vifaa vya msaada

Hali mbaya ya hewa ambayo hivi karibuni imeikumba Afghanistan ina ishara zote za janga la mabadiliko ya tabianchi linalozidi kuongezekakwani baadhi ya mikoa iliyoathiriwa ilikumbwa na ukame mwaka jana.

Ripoti zinaonyesha kuwa hali mbaya ya hewa nchini humo inaongezeka mara kwa mara na kusababisha hasara ya maisha na uwezo wa watu kuishi pamoja na uharibifu mkubwa wa miundombinu.

Ongezeko la idadi na ukali wa matukio ya hali mbaya ya hewa litahitaji UNICEF na watendaji wengine wa kibinadamu kuchukua hatua kwa kasi zaidi na kwa kiwango kikubwa cha msaada wa kibinadamu.

"Lakini hii inawezekana tu kwa hatua zilizoimarishwa za kujitayarisha, kama vile utangulizi zaidi wa vitu vya msaada wa dharura na uratibu bora." Limesema shirika hilo la Umoja wa Mataifa.

Licha ya kuwa moja ya nchi zinazohusika kidogo na mabadiliko ya tabianchi, Afghanistan inashika nafasi ya 15 kati ya mataifa 163 katika fahirisi ya hatari ya mabadiliko ya tabianchi kwa watoto kwa mujibu wa ripoti ya UNICEF ya 2021.

Hii ina maana kwamba sio tu kwamba majanga ya tabianchi na mazingira yanatawala nchini humo, lakini pia watoto huko wako katika hatari ya athari zake ikilinganishwa na maeneo mengine ya ulimwengu.