Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafuriko yasababisha maafa Malawi, Katibu Mkuu UN atuma salamu.

Malawi imekabiliwa na mafuriko makubwa mara kwa mara
PICHA: EU/ECHO Jacqueline Chinoera
Malawi imekabiliwa na mafuriko makubwa mara kwa mara

Mafuriko yasababisha maafa Malawi, Katibu Mkuu UN atuma salamu.

Tabianchi na mazingira

Kwa mara nyingine Malawi imekumwa na mafuriko makubwa yaliyokatili maisha ya watu, kusababisha uharibifu mkubwa na kuwafungisha virago mamia ya watu ambao sasa wanahitaji msaada umesema Umoja wa Mataifa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutrerres, amsekitishwa na vifo pamoja na uharibifu mkubwa kwa makazi na mali vilivyosababishwa na mafuriko kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini Malawi.

Kupitia taarifa aliyoitoa mjini New York Marekani na msemaji wake, Bwana Guterres ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza maisha, kwa serikali na watu wote wa Malawi.

“Umoja wa Mataifa uko pamoja na mamalaka za Malawi na uko tayari kuwasaidia wakati huu ambapo wanatoa misaada ya mahitaji muhimu kwa waathirika wa mafuriko hayo” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Vyombo vya habari vinasema kuwa watu waliopoteza maisha katika mafuriko hayo yaliyosababishwa na mvua kubwa vimefikia 30 na kuwajeruhi watu wengine 377.

Aidha vyombo mbalimbali vya habari vimeeleza kuwa nyumba 93,730 zimesambaratishwa na mafuriko hayo na kuwaacha watu 6,341 bila  makazi huku familia nyingi sasa zikiishi kwenye kambi.