Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Misaada ya kibinadamu Gaza haitoshi kabisa: UN

Mwanamume amebeba kifurushi cha biskuti ambazo zimeingia hivi karibuni kupitia baharini.
© WFP/Jaber Badwan
Mwanamume amebeba kifurushi cha biskuti ambazo zimeingia hivi karibuni kupitia baharini.

Misaada ya kibinadamu Gaza haitoshi kabisa: UN

Amani na Usalama

Wakati jeshi la Israel likiendelea na mashambulizi yake ya anga na mashambulizi ya ardhini huko Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza, wakazi wa eneo la Palestina linalokaliwa wanapokea msaada kidogo sana kiasi kwamba watoto zaidi na zaidi wanakufa kwa njaa, yameonya leo mshirika ya misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu na Misaada ya Dharura OCHA, “wananchi wa Gaza hakika hawapokei kiasi wanachohitaji sana cha msaada ili kuepusha baa la njaa, ili kuepuka maovu yote tunayoyaona na kuna pesa kidogo sana zinazozunguka kwa sasa." 

Tahadhari hii imetolewa leo na Jens Laerke, msemaji wa OCHA, katika mkutano wa Umoja wa Mataifa na waandishi wa habari huko Geneva Uswisi.

Tahadhari hii ya OCHA inakuja huku mashirika mengi zaidi yakionya juu ya matokeo ya vikwazo vinavyoendelea vya kupata misaada huko Gaza. 

Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO limesema , watoto wanakufa kwa njaa kutokana na vikwazo hivyo.

Mtoto akipokea chakula katika jiko linaloungwa mkono na WFP huko Khan Younis, Gaza.
© WFP/Ali Jadallah
Mtoto akipokea chakula katika jiko linaloungwa mkono na WFP huko Khan Younis, Gaza.

Asilimia 85 ya watoto hawakula kwa siku nzima

Utafiti wa hivi karibuni wa Umoja wa Mataifa umeonyesha kuwa asilimia 95 ya watoto wenye umri wa miezi sita hadi 23 yaani, hasa wale walio chini ya umri wa miaka mitano hula makundi mawili au machache tofauti ya chakula kwa siku. "Lakini kinachonishangaza zaidi ni kwamba asilimia 85 ya watoto hawakula kwa siku nzima angalau mara moja katika siku tatu kabla ya utafiti," huo amesema Dkt. Margaret Harris, msemaji wa utafiti huo wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO.

"Huu ni uchunguzi wa papo kwa papo, waliangalia suala hilo na hawa ni watoto wa chini ya umri wa miaka mitano ambao hawajala kutwa nzima, na hii katika siku tatu zilizopita kabla ya uchunguzi. Kwa hivyo tunaweza kujiuliza endapo chakula kinasambazwa vizuri , jibu ni hapana, watoto wana njaa."

Ikikabiliwa na hali hii, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharira OCHA imeendelea kusisitiza kuwa wajibu wa mamlaka ya Israel kuwezesha utoaji wa misaada hauishii mpakani.

Msemaji wa ofisi hiyo jens Laerk amesema "Wajibu wao hauishii mzigo unaposhuka mpakani, umbali wa mita chache tu, na kuendesha gari ili kuwaacha wahudumu wa kibinadamu kuvuka maeneo ya mapigano ambayo hawawezi kufanya lolote kwenda kupata msaada. Kwa hivyo, misaada inayowasili haifikii idadi yote ya watu,” 

Mashambulizi ya mabomu ya Israel yameharibu majengo na miundombinu huko Gaza.
UNOCHA/Samar Elouf
Mashambulizi ya mabomu ya Israel yameharibu majengo na miundombinu huko Gaza.

OCHA inataka vivuko zaidi vya ardhini

Katika kujibu swali kuhusu mchango wa daraja linaloelea linalosimamiwa na jeshi la Marekani, OCHA imekumbusha kuwa njia zote za kutoa misaada zinakaribishwa. "Kwa hivyo wakati ukweli huo haufanyi kazi, bila shaka ni habari mbayá."

Ili kusistiza hilo OCHA inasema ingawa haikuwahi kupangwa, wala kuwa na uhalisia, wa kufanya daraja linaloelea kuwa njia kuu ya kutoa misaada. "Inaweza kuwa nyongeza muhimu na tunaendelea kusisitiza hilo."

Kwa Shirika hilo la Umoja wa Mataifa, njia pekee ya kutoa misaada kwa kiwango kikubwa na kwa kasi kubwa ni kupitia maeneo ya kivuko cha ardhini. "Na hapo ndipo tunapoingia kwenye shida hizi."

Kulingana na OCHA, wasaidizi wa kibinadamu wanahitaji zaidi sehemu hizi za kuvuka ardhini. 

"Tunazihitaji ziwe wazi na tunahitaji ziwe salama kuzitumia kuchukua misaada inaposhushwa."

UNRWA yaonya dhidi ya kuenea kwa magonjwa

Akirejelea wasi wasi huu, mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina UNRWA, Philippe Lazzarini, jana Alhamisi alidokeza kwamba vita ya Gaza imesababisha "kupuuzwa kwa wazi kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na mashambulio ya kutisha dhidi ya wafanyakazi wa UNRWA, vituo na shughuli zake".

Huku Wapalestina waliokimbia makazi yao, ambao wengi wao walikimbia ghasia mara nne au tano wakati wa vita, wanatatizika kuishi katika makazi yenye watu wengi ambako vifaa vya usafi ni haba, UNRWA imeonya kuhusu kusambaa kwa magonjwa na ukosefu wa dawa.

Makazi yaliyofurika watu wengi na ukosefu wa usafi ni hatarishi kwa kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza huko Gaza, limeonya shirika la Umoja wa Mataifa likibainisha kuwa hakuna chanjo au dawa za kutosha kukidhi mahitaji ya wakazi.

“Timu za UNRWA zinaendelea kutoa huduma za afya kwa watu walio katika mazingira magumu, wakiwemo watoto na wazee. Lakini chanjo na dawa hazitoshi kabisa. Tunahitaji ufikiaji salama na usio na kikomo wa huduma za afya," limeandisha shirika la UNRWA kwenye mtandao wake wa kijamii wa X.

Maelfu ya familia za Gaza zinakimbia mji wa Rafah baada ya mashambulizi ya anga ya Israel.
© WFP/Ali Jadallah
Maelfu ya familia za Gaza zinakimbia mji wa Rafah baada ya mashambulizi ya anga ya Israel.

Migogoro na vitisho vinadhoofisha kazi za NGOs za Palestina

Katika suala jingine, Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu imeeleza wasi wasi wake mkubwa kuhusu athari kwa mashirika ya kiraia ya Palestina kutokana na kuongezeka kwa operesheni za kijeshi za Israel huko Gaza, pamoja na vitisho kutoka Israel vinavyoendelea kukabili mashirika hayo au NGOs.

Huko Gaza, wafanyikazi kadhaa wa ndani wa NGOs wameuawa, kujeruhiwa au kuwekwa kizuizini, na wafanyikazi wengi wamehamishwa mara kadhaa, ikiwa ni pamoja na nje ya Ukanda huo tangu Oktoba 7 mwaka 2023.

Katika eneo linalokaliwa la Palestina, wafanyikazi wa mashirika ya kiraia wako katika hatari ya mara kwa mara ya kunyanyaswa, kukamatwa, kuwekwa kizuizini kiholela, kudhulumiwa, na hata kufukuzwa kwa kazi zao ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Palestina na mamlaka ya Hamas.

Mwaka 2021, NGOs sita maarufu za haki za binadamu za Palestina zilitengwa na kuchukuliwa na Israeli kama "mashirika ya kigaidi bila ushahidi, na tuhuma dhidi yao bado hazijathibitishwa.”

Athari mbaya za kutengwa kwa mashirika hayo ya kiraia ya Palestina zimekuwa kubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa usaidizi wa wafadhili, kupoteza wafanyakazi, hofu ya kufanyia kazi masuala muhimu ya haki za binadamu, na ari ya wafanyakazi," imeangazia tarifa ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk.