Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mauaji ya raia Burkina Faso yamefurutu ada lazima yakome: OHCHR

Watoto walio chini ya umri wa miaka mitano ni miongoni mwa watu walioathiriwa na migogoro nchini Burkina Faso ambao wananufaika na utunzaji wa lishe na kisaikolojia.
© Doctors of the World/Olympia
Watoto walio chini ya umri wa miaka mitano ni miongoni mwa watu walioathiriwa na migogoro nchini Burkina Faso ambao wananufaika na utunzaji wa lishe na kisaikolojia.

Mauaji ya raia Burkina Faso yamefurutu ada lazima yakome: OHCHR

Amani na Usalama

Kamishina Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk leo ameelezea wasiwasi mkubwa kufuatia ongezeko la hivi karibuni la mauaji ya raia nchini Burkina Faso, huku kukiwa na madai pande zote, makundi yenye silaha na serikali kuhusika na mauaji hayo.

Kwa mujibu wa tarifa ya ofisi ya Kamishina Mkuu wa haki za binadamu OHCHR kati ya Novemba 2023 na Aprili mwaka huu 2024 imepokea madai ya ukiukwaji wa haki na ukatili unaokiuka sheria za kimataifa za haki za binadamu ukiwaathiri takriban watu 2732 hili likiwa ni ongezeko la asilimia 71 ya visa vya ukiukwaji wa haki za binadamu ukilinganisha na miezi sita iliyopita.

Taarifa inasema watu 1794 ay asilimia 65 miongoni mwa watu hao ni waathirika wa mauaji ya kinyume cha sheria.

Ofisi hiyo ya haki za binadamu imesema Makundi yenye silaha, kama vile Jamāʿat nuṣrat al-islām wal-muslimīn, Kundi kubwa la Kiislamu katika Jangwa la Sahara na makundi mengine yanayofanana na hayo, yamezidisha mashambulizi yao dhidi ya raia, ikiwa ni pamoja na dhidi ya wakimbizi wa ndani. 

Kwa mujibu wa Bwana Türk "Wakati makundi yenye silaha yanadaiwa kuhusika na idadi kubwa ya matukio na waathirika, na yanapaswa kuwajibika, pia ninasikitishwa sana kwamba vikosi vya usalama na ulinzi na wasaidizi wao ambao ni watu waliojitolea kwa ulinzi wan chi yao wanadaiwa kutekeleza mauaji ya kiholela, ikiwa ni pamoja na kunyongwa,”

Awali mkuu huyo wa haki za binadamu alizungumzia masuala haya na Kapteni Ibrahim Traoré, Rais wa Burkina Faso, wakati wa ziara yake nchini humo Machi mwaka huu.

Türk ameongeza kuwa "Ninatambua kikamilifu vitisho tata vya usalama ambavyo Burkina Faso inakabiliana nayo. Jawabu dhidi ya vitisho hivi litafaulu tu ikiwa sheria za kimataifa zitaheshimiwa kikamilifu kote nchini. Kwa hivyo narudia wito wangu kwa mamlaka nchini Burkina Faso kuchukua hatua zote zinazowezekana ili kuhakikisha ulinzi wa raia.” 

Kamishna Mkuu ametoa wito kwa Serikali ya Burkina Faso kuunga mkono uchunguzi wa kina, huru na wa uwazi kuhusu tuhuma zote za ukiukaji wa haki na ukiukwaji wa sheria za kimataifa, na kuhakikisha kuwa wahalifu wanafikishwa mahakamani, katika kesi zinazokidhi viwango vya kimataifa, ili kuhakikisha haki ya kweli kwa waathirika na fidia.

Amesisitiza kwamba ni “Lazima kuweka na haki na uwajibikaji endapo mamlaka inataka kweli kuihakikishia jamii inarejesha mshikamano wa kijamii na kujenga upya uaminifu kati ya raia na vikosi vya usalama."