Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raia wa Sudan Kusini walikatiliwa na kuuawa Zaidi mwaka 2022 ikilinganishwa na 2021: UNMISS

Mlinzi wa amani wa UNMISS nchini Sudan Kusini akishika doroa kwenye jimbo la Equatorial
UN Photo/Isaac Billy
Mlinzi wa amani wa UNMISS nchini Sudan Kusini akishika doroa kwenye jimbo la Equatorial

Raia wa Sudan Kusini walikatiliwa na kuuawa Zaidi mwaka 2022 ikilinganishwa na 2021: UNMISS

Amani na Usalama

Mpango wa umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini UNMISS leo umetoa taarifa ya kila mwaka ya haki za binadamu na ukatili unaoatjiri raia ambayo inaonyesha kuna ongezeko la asilimia 2 la idadi ya raia waliokatiliwa nchini humo mwaka 2022, licha ya kupungua kwa vitendo vya ukatili kwa ujumla kwa asilimia 27 mwaka 2022 ikilinganisha na mwaka 2021.

Kwa mwaka 2022 kulikuwa na matukio ya ukatili 714 wakati mwaka 2021 kulikuwa na matukio ya ukatili 982.

Ripoti iyo inayohusu kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba 2022, “ilisajili takriban waathirika 3,469 wa mauaji, kujeruhiwa, utekaji nyara na unyanyasaji wa kingono unaohusiana na migogoro.”

Pia inaonyesha kwamba wakati idadi ya matukio ya ukatili yaliyotokana na wahusika katika mgogoro yalipungua kwa asilimia 37 ikilinganishwa na mwaka 2021, idadi ya waathirika iliongezeka kwa asilimia 58 kutoka watu 1,057 mwaka 2021 hadi watu 1,674 mwaka 2022.

Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini inaendelea kuorodhesha ukiukaji wa haki za binadamu.
UN Photo/Isaac Billy
Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini inaendelea kuorodhesha ukiukaji wa haki za binadamu.

Vurugu za makundi yenye silaha

Kuhusu matukio ya vurugu yanayohusishwa na wanamgambo wa kijamii waliojihami au vikundi vya ulinzi wa raia, idadi ya matukio ilipungua kwa asilimia 27 kutoka matukio 531 hadi 387 na idadi ya waathirika ilipungua kwa asilimia 28 kutoka  watu 2,279 hadi 1,642 kwa ikilinganishwa na 2021.

Ripoti hiyo ya UNIMISS inasema  mwaka 2022 uliadhimishwa na ongezeko la machafuko matatu tofauti ambayo ni kati ya Aprili na Mei, katika jimbo la Unity Kusini,  kati ya Julai na Septemba, katika jimbo la Warrap na kati ya Agosti na Desemba, katika eneo la Greater Upper Nile.

Kijiografia, asilimia 42 ya Wasudan Kusini waliokumbwa na vita vikali walikuwa katika majimbo ya Upper Nile na Warrap, huku majimbo ya Jonglei, Unity, Equatoria Mashariki na Equatoria ya Kati kwa pamoja yakichukua takriban asilimia 50 ya waathirika.

Wakimbizi wa ndani katika jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini.
UNMISS
Wakimbizi wa ndani katika jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini.

Majimbo yaliyoathirika zaidi

Kulingana na ripoti hiyo, majimbo ya Equatoria Mashariki, Jonglei na Warrap ndiyo yaliyoathiriwa zaidi na ghasia zilizohusisha wanamgambo wa kijamii au vikundi vya ulinzi wa raia.

Majimbo ya Upper Nile na Unity, kwa upande wao, yameathiriwa na wahusika kwenye mzozo huo na wawakilishi wao au vikundi vya wanamgambo washirika. Jimbo la Ikweta ya Kati lilikumbwa na ghasia kati ya jamii katika kaunti za Juba na Terekeka, na wahusika kwenye mzozo wa Yei, Morobo na Lainya.

Kinachotia wasiwasi zaidi UNIMISS inasema “ni ongezeko la asilimia 96 la unyanyasaji wa kingono unaohusiana na migogoro dhidi ya wanawake na wasichana ikilinganishwa na 2021.”

Nicholas Haysom, mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na mkuu wa UNMISS ametoa wito kwa Serikali ya Sudan Kusini kuonyesha nia ya kisiasa na kuongeza juhudi dhidi ya ukwepaji wa sheria na watu kutoadhibiwa, kuchunguza ukiukaji wa haki za binadamu na unyanyasaji na kuwawajibisha wahalifu, hasa kutokana na kwamba ghasia mbaya bado ni suala linalotia wasiwasi mkubwa katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo. “

UNMISS pia inazitaka pande zote za Sudan Kusini kuzingatia matarajio ya amani endelevu, usalama, na uchaguzi wa amani, haki na shirikishi.