Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Yumkini hali si shwari DRC mauaji, ubakaji na vita vyatawanya maelfu: Khehris

Mtoto akiwa katika kami ya wakimizi wa ndani
© UNICEF/Diana Zeyneb Alhindawi
Mtoto akiwa katika kami ya wakimizi wa ndani

Yumkini hali si shwari DRC mauaji, ubakaji na vita vyatawanya maelfu: Khehris

Amani na Usalama

Naibu msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu Ilze Brands Kehris, amehitimisha ziara nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC na kusema alichokishuhudia kinatisha na kusikitisha akihimiza hatua Madhubuti kuchukuliwa kunusuru maisha ya watu hususan Mashariki mwa nchi hiyo. 

Kehris ambaye katika ziara yake alizuru mji mkuu Kinshasa, na miji ya Goma na Bunia Mashariki mwa taifa hilo ameselezea kutiwa hofu na hali mbaya ya usalama inayozidi kuzorota Mashariki mwa DRC ambako makundi mbalimbali yenye silaha yakiwemo M23, Allied Democratic Forces ADF, CODECO na Zaire, yanaendelea kufanya mashambulizi dhidi ya raia. 

Amesema miongoni kwa uasi ambao ni ukiukwaji wa haki za binadamu  unaotekelezwa na makundi hayo na kuorodheshwa na osifi ya haki za binadamu unajumuisha mauaji ya watu wengi, ukeketaji na unyanyasaji wa kingono unaohusiana na migogoro, na kulazimisha maelfu ya watu kuhama makazi yao na kukabiliwa na kiwewe. 

Ngadjole Ngle Jean-Pierre, baba wa watoto wanne. Mke wake aliuawa na waasi katika kituo cha wakimbizi wa ndani cha Plain Savo jimboni Ituri nchini DRC.
UNHCR Video
Ngadjole Ngle Jean-Pierre, baba wa watoto wanne. Mke wake aliuawa na waasi katika kituo cha wakimbizi wa ndani cha Plain Savo jimboni Ituri nchini DRC.

Mashambulizi na ukatili havipaswi kuendelea 

Naibu huyo msaidizi wa Katibu mkuu amesema "Ninalaani vikali mashambulizi ya kutisha nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na naunga mkono wito wa Katibu Mkuu mwishoni mwa juma lililopita wa hatua ya amani barani Afrika. Vurugu lazima zikome. Pia ninahimiza sana mamlaka kuzidisha juhudi zao za kukabiliana na chuki inayoongezeka na kutekeleza mipango inayolengwa ili kukuza uaminifu na mshikamano ndani na kati ya jamii.”   

Ameongeza kuwa kuibuka tena kwa mashambulio ya M23 katika jimbo la Kivu Kaskazini katika miezi ya hivi karibuni kumeathiri vibaya sana maisha ya watu. 

Kutawanywa huko kwa watu Kivu Kaskazini pia kumesababisha kutumwa tena kwa wanajeshi wa Serikali hali ambayo imezua ombwe la usalama katika maeneo mengine yaliyoathiriwa na migogoro, na kuruhusu makundi mengine yenye silaha kupata nafasi na kueneza ugaidi katika miji, vijiji na kambi kwa watu waliokimbia makazi yao.  

“Mazingira haya mabaya yamekuza habari potofu, chuki na matamshi ya chuki dhidi ya baadhi ya makabila na hatari za kuchochea vurugu zaidi.”Ameendelea kusema afisa huyo. 

Ameendelea kusema kwamba "Huko Goma na Bunia, nimeshangazwa na umnepo wa waathiriwa, wawakilishi wa mashirika ya kiraia na jumuiya zilizoathiriwa na migogoro kusaka njia mpya. Nilisikiliza maelezo yao binafsi ya vurugu na mapendekezo ya kuchukuliwa hatua. Na nilisikiliza kwa makini wito wao wa jinsi Umoja wa Mataifa na jumuiya ya kimataifa inavyoweza kusaidia watu wa Congo na serikali kumaliza migogoro na kushughulikia matatizo ya sasa na ya zamani.” 

Wanawake wakirejea katika nyumba zao katika makazi ya wakimbizi wa ndani ya Plain Savo jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
© UNHCR/Hélène Caux
Wanawake wakirejea katika nyumba zao katika makazi ya wakimbizi wa ndani ya Plain Savo jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Mazingira wanamoishi wakimbizi wa ndani Ituri hayaridhishi 

Katika jimbo la Ituri, afisa huyo wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu alihuzunishwa sana na hali ya maisha ya watu waliolazimishwa na mizozo ya kivita kukimbia makazi yao.  

Wanawake wengi, wanaume na watoto katika kambi ya wakimbizi wa ndani, karibu na Bunia, walikuwa na uhitaji mkubwa wa chakula, matibabu na usaidizi wa kisaikolojia.  

Hali ni mbaya zaidi kwa walio hatarini zaidi wale ambao wamekeketwa, wazee na wengine.   

"Katika nchi yinayoshika nafasi ya 3 kwa idadi kubwa ya watu duniani  ambao wamekimbia makazi yao, mara nyingi kukaa kwa miaka mingi katika mazingira hatarishi ni ukumbusho tosha kwamba kukidhi mahitaji ya msingi ya kibinadamu ni suala la haki za binadamu," amesisitiza Brands Kehris. 

 Kwa watoto walioathiriwa na migogoro na kuhama makazi yao, amesema ukosefu wa fursa ya kupata shule peke yake ni ukiukwaji wa haki yao ya elimu, ambayo ina athari ya kudumu katika maisha yao.  

Pia huongeza hatari yao ya kukabiliwa na shughuli za uhalifu na kuwafanya kuwa katika hatari zaidi ya kuandikishwa kwenye vikundi vilivyojihami ambavyo vimeuathiri na kuutia kiwewe utoto wao.   

Familia ya watu waliofurushwa makwao wakiwasili na lori kuishi na familia Beni baada ya kukimbia machafuko Ituri, DRC.
© UNHCR/Ibrahima Diane
Familia ya watu waliofurushwa makwao wakiwasili na lori kuishi na familia Beni baada ya kukimbia machafuko Ituri, DRC.

Mauaji, ubakaji, na ukataji watu viungo unaendelea 

Kwa mujibu wa afisa huyo wa Umoja wa Mataifa mauaji ya watu wengi, ukataji watu viungo na ukatili wa kingono unaohusiana na migogoro unaendelea.  

Walionusurika katika ghasia za kutisha na unyanyasaji mwingine wamemwambia kwamba wanahisi wameachwa na kusahauliwa.  

Akielezea uchungu na kufadhaika kwao, mwathiriwa mmoja amemwambia kwamba jumuiya ya kimataifa haionekani kutambua mateso yao. 

"Katika muktadha huu wenye changamoto, hatua za kijeshi kwa vitisho vya makundi yenye silaha zinapaswa kutanguliza ulinzi wa raia. Kwa kuongeza, kuheshimu haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu kwa nguvu zote DRC sio tu wajibu wao, lakini pia kunafanya kuwa na ufanisi zaidi."    

Brands Kehris amesisitiza kuendelea kuwa tayari kwa ofisi ya kamishna mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu kusaidia katika uanzishaji wa mfumo unaofaa wa kufuata kwa vikosi vya usalama.  

Ameongeza kuwa "Tunatazamia kushirikiana na Jeshi la kikanda la jumuiya ya Afrika Mashariki, lililoidhinishwa na Muungano wa Afrika, kwa uratibu wa karibu na MONUSCO na vikosi vya jeshi vya Congo." 

Katika ziara yake hiyo ya siku 10, msaidizi huyo wa Katibu Mkuu alikutana na  waziri mkuu Sama Lukonde, marais wa bunge na seneti na viongozi wengine wakuu wa Serikali wakiwemo mawaziri wanaohusika na masuala ya sheria, haki za binadamu na ulinzi wa taifa.  

Pia alikutana na magavana wa kijeshi wa majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri, maafisa wakuu wa kijeshi na haki za kiraia, viongozi wa jumuiya na mashirika ya kiraia, ikiwa ni pamoja na vyama vya waathiriwa, wawakilishi wa jumuiya ya kidiplomasia, Jeshi la Kanda la Jumuiya ya Afrika Mashariki na mfumo wa Umoja wa Mataifa, hasa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuleta utulivu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo MONUSCO.