Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mfumo wa afya nchini Sudan unaporomoka: WHO

Watoto wakitembea kuelekea kituo cha wakimbizi wa ndani huko El Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini nchini Sudan (Maktaba)
© UNICEF/Shehzad Noorani
Watoto wakitembea kuelekea kituo cha wakimbizi wa ndani huko El Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini nchini Sudan (Maktaba)

Mfumo wa afya nchini Sudan unaporomoka: WHO

Afya

Nchini Sudan katika maeneo ambayo ni magumu kufikiwa, vituo vya afya vimeharibiwa, kuporwa au kukabiliwa na uhaba mkubwa wa wafanyakazi, madawa, chanjo, vifaa na vifaa. Ni asilimia 30 -20 tu ya vituo vya afya vinasalia kufanya kazi, na hata hivyo katika viwango vidogo, ameeleza leo Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, Christina Lindmeier.

 
Bi. Lindmeir amewaeleza waaandishi wa habari jijini Geneva, Uswisi kwamba vifaa tiba nchini Sudan vinakidhi asilimia 25 tu ya mahitaji. Ghala la WHO katika jimbo la Al Gezirah halijaweza kufikiwa tangu Desemba 2023. Baadhi ya majimbo, kama vile Darfur, hayajapokea vifaa vya matibabu kwa mwaka uliopita. Watu wanaougua kisukari, shinikizo la damu, saratani au kushindwa kwa figo wanaweza kupata matatizo au kufa kwa kukosa matibabu.
 
Milipuko ya magonjwa inaongezeka kwa zaidi ya visa milioni 1.3 vya malaria, visa 11,000 vya kipindupindu, zaidi ya visa 4,600 vya surua, na visa 8,500 vya dengue. Milipuko ya malaria, surua, homa ya dengue na Homa ya ini (hepatitis E) pia inaenea katika nchi jirani ya Chad.
 
“WHO imefikia karibu watu milioni 2.5 kupitia usaidizi wa moja kwa moja kwa huduma na utoaji wa vifaa vya dharura. Takriban watu 50,000 wamepata huduma katika kliniki za kuhamahama. Wakimbizi 433,000 wa Sudan walitibiwa katika kliniki zinazohama mashariki mwa Chad.” Amezitaja takwimu.
 
WHO imewasilisha vifaa muhimu vya matibabu kupitia operesheni za kuvuka mpaka kutoka Chad na Sudan Kusini ikiwa ni pamoja na vya kusaidia waliopata kiwewe na vifaa vya upasuaji wa dharura, viuavijasumu (antibiotics), na vipimo vya haraka vya dengue.
 
“Katika miezi michache iliyopita,” anaendelea kueleza kuwa juhudi za WHO na wadau wake zimesababisha kupungua kwa idadi ya visa vya kipindupindu, dengue na malaria. Watu milioni 4.5 walio na umri wa zaidi ya mwaka mmoja walipokea Chanjo ya Kipindupindu ya matone (OCV) katika majimbo 6 yaliyo hatarini zaidi.
 
 “Tumewasilisha vifaa kwa ajili ya matibabu ya watoto 115,000 wanaokabiliwa na utapiamlo mkali wenye matatizo ya kiafya.”