Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO na wadau wawakutanisha wadau wa kilimo na chakula Tanzania

Picha ya pamoja ya kikundi cha Washirika wa Maendeleo ya Kilimo na Lishe, wakulima, sekta binafsi, na watafiti na Taasisi za kitaaluma mjini Morogoro Tanzania.
UN News
Picha ya pamoja ya kikundi cha Washirika wa Maendeleo ya Kilimo na Lishe, wakulima, sekta binafsi, na watafiti na Taasisi za kitaaluma mjini Morogoro Tanzania.

FAO na wadau wawakutanisha wadau wa kilimo na chakula Tanzania

Ukuaji wa Kiuchumi

Nchini Tanzania, kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) na wadau wake kama Kitovu cha Kuratibu Mifumo ya Chakula cha Umoja wa Mataifa, Kikundi cha Washirika wa Maendeleo ya Kilimo na Lishe, wakulima, sekta binafsi, na watafiti na Taasisi za kitaaluma wamekutana mjini Morogoro ili kupitia na kuboresha vipaumbele na ramani ya mifumo ya chakula iliyoanzishwa mwaka 2021.

Ulikuwa mkutano wa siku mbili kuanzia jana Mei 23 na umehitimishwa leo Mei 24. Nimepata fursa ya kuzungumza na baadhi ya wadau na huyu hapa ni Mkurugenzi wa masoko na usalama wa chakula kutoka Wizara ya Kilimo ya Tanzania, Gugu Mibavu anaeleza zaidi kuhusu dhamira kuu ya mkutano huu. 

Mkurugenzi wa masoko na usalama wa chakula kutoka Wizara ya Kilimo ya Tanzania, Gugu Mibavu.
UN News
Mkurugenzi wa masoko na usalama wa chakula kutoka Wizara ya Kilimo ya Tanzania, Gugu Mibavu.

“Dhamira kubwa ya mkutano huu ni kupitia ule mkutano wa wadau (Mkutano wa mifumo ya chakula uliofanyuka mwaka 2021), kujadili kilichopo na mabadiliko yake ni yapi hadi sasa tukiwa na takribani zaidi ya miaka mitatu imepita, kwa kuwa kuna mambo mengi yametokea na sisi wizara tumeendelea kuboresha masuala mengi yanayohusiana na uendelezaji wa sekta ya Kilimo, kwahivyo, tunachotaka kuona kama kweli kilichopo bado kinaakisi mambo ambayo tunaendelea kuyafanya kama wizara, lakini vilevile kujua maeneo gani mapya ambayo tunaweza kuyaingiza, nilizungumzia masuala ya uratibu na utawala bora, ukiangalia vipaumbele vyetu utaona kama haviko sawasawa, na ndio maana nikasisitiza kwamba hizi jitihada zinazofanywa na taasisi mbalimbali, bila ya kuziratibu na kuziwekea mipango thabiti tutajikuta kila mtu anarudia mipango ambayo inafanya na mwingine, suala ambalo linapoteza rasilimali na muda”

Mkutano huu umefungamanishwa na Malengo ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo Endelevu, SDGs, Gugu Mibavu anafafanua

“SDG’s ni malengo ya maendeleo endelevu ambayo tuliwekeana kwa kukubaliana ifikapo Mwaka 2030, mfano mmoja hatutakuwa na njaa, sasa ukiangalia miaka iliyobakia ni Sita tu ili kutoa matokeo ya yale ambayo tumewaahidi watu kwamba ikifika mwaka 2030, kutakuwa hakuna njaa”

Mkuu wa Divisheni ya sera katika Wizara ya Kilimo, umwagiliaji, maliasili na mifugo Zanzibar, Sihaba Haji Vuai.
UN News
Mkuu wa Divisheni ya sera katika Wizara ya Kilimo, umwagiliaji, maliasili na mifugo Zanzibar, Sihaba Haji Vuai.

Kutoka upande wa Tanzania Visiwani, Mkuu wa Divisheni ya sera katika Wizara ya Kilimo, umwagiliaji, maliasili na mifugo Zanzibar, Sihaba Haji Vuai ameeleza maboresho waliyonayo yanayoendana na vipaumbele ili kuzitekeleza kikamilifu SDGs.

“Tuko sambamba na vipaumbele vilivyopo katika mifumo ya chakula, jitihada zetu katika kufanya mageuzi ya kilimo tumekuwa na vipaumbele sita kwenye mazao ya kilimo, mazao ya matunda, mazao ya viungo na tuna mazao ya mifugo, kwahivyo, katika kuendana na vipaumbele vilivyopo tumejikita zaidi kuimarisha miundombinu ya uzalishaji katika Sekta ya Kilimo kwa ujumla wake na kilimo cha umwagiliaji kwenye mpunga, lakini pia kuna Kilimo cha umwagiliaji kwenye mbogamboga, pia tunajikita katika kuhakikisha mazao yanayozalishwa, yanachakatwa kiasi kwamba yaweze kutumika kwa kuwafikia walaji moja kwa moja kwa usalama zaidi, kwahivyo, mageuzi haya tumelenga kuwa na vituo vya uchakataji wa mazao ya kilimo kwa kila wilaya”

Miongoni mwa vipambele sita vilivyojadiliwa katika mkutano wa mfumo ya chakula mwaka 2021, ambayo ufanikishwaji wake ndio umejadiliwa katika mkutano huu, ni pamoja na uzalishaji wenye tija katika sekta ndogo za mazao, mifugo na uvuvi, ufadhili wa kilimo na ushiriki wa sekta binafsi katika mfumo wa chakula, kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, kukabiliana na hali na ulinzi wa bayonuai.