Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ufugaji samaki Tanzania kusongesha sekta ya uvuvi- FAO

Wanafamilia wakivua samaki kutoka katika bwawa lao walimofuga samaki na hii imewezekana kutokana na mfumo wa umwagiliaji maji kutoka mto jirani huko Haiti
UN/Logan Abassi
Wanafamilia wakivua samaki kutoka katika bwawa lao walimofuga samaki na hii imewezekana kutokana na mfumo wa umwagiliaji maji kutoka mto jirani huko Haiti

Ufugaji samaki Tanzania kusongesha sekta ya uvuvi- FAO

Ukuaji wa Kiuchumi

Tanzania imejaliwa  vyanzo vingi vya maji vinavyoweza kupatia wakazi wa nchi hiyo kitoweo cha samaki. Vyanzo hivyo ni pamoja na bahari, maziwa na mito ambapo hata hivyo mabadiliko ya tabianchi yanatishia uwepo wa viumbe hivyo katika vyanzo hivyo vya maji na FAO inachukua hatua.

Shirika la kilimo na chakula, FAO nchini Tanzania kwa kutambua nafasi kubwa ya sekta ya uvuvi katika kukwamua uchumi wa taifa hilo, linasaidia serikali kusimamia vizuri sekta hiyo na pia wakulima kuweza kujipatia samaki kwa ajili ya kitoweo na biashara.

Mwakilishi wa FAO nchini Tanzania Fred Kafeero akihojiwa na Stella Vuzo wa kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa jijini Dar es salaam, amesema kwa serikali wanaisaidia kuandaa mpango kabambe wa usimamizi wa sekta ya samaki na pia ufugaji wa samaki,

“Ili watu wasitegemee tu kuvua samaki kutoka kwenye vyanzo asili vya maji bali watengeneza vyanzo vya maji ambamo watafuga samaki. Huko Zanzibar tunashirikiana na serikali  kwa msaada wa fedha kutoka KOICA tumeanzisha bwawa la kuzalisha mbegu bora za samaki ambazo tunasambaza kwa wakulima ili watengeneza mabwawa na wafuge samaki.”

Bwana Kafeero amesema kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha uhaba wa samaki na uvuvi kupita kiasi, ufugaji wa samaki ndio mwelekeo wa sasa ili kuepusha uvuvi kupita kiasi kwenye baharí, maziwa na mito akisema,

“Katika nchi nyingi hasa barani Asia nchi za kusini Mashariki mwa bara hilo, kiwango kikubwa cha kitoweo cha samaki kinacholiwa eneo hilo na kuuzwa nje ya nchi hutoka katika mabwawa binafsi ya ufugaji, kwa nini isiwezekane Tanzania ambayo ina utajiri wote huu, ufugaji samaki unaweza kusongesha sekta ya uvuvi.”

Kwa mujibu wa Bwana Kafeero, FAO inatambua kilimo kuwa kinajumuisha mazao, uvuvi, mifugo na usimamizi wa rasilimali asili kama vile misitu.