Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gaza: Wakati watu wakiendelea kukimbia Rafah UN yahimiza kufunguliwa upya kwa njia za misaada

Watu waliokimbia makazi yao wanajenga mahema mapya katika eneo la Al-Mawasi katikati mwa Gaza.
UN News / Ziad Taleb
Watu waliokimbia makazi yao wanajenga mahema mapya katika eneo la Al-Mawasi katikati mwa Gaza.

Gaza: Wakati watu wakiendelea kukimbia Rafah UN yahimiza kufunguliwa upya kwa njia za misaada

Amani na Usalama

Bila dalili ya kusitisha operesheni ya kijeshi ya Israel katika mji wa kusini mwa Gaza wa Rafah leo Ijumaa, wahudumu wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa wametoa wito mpya wa kusitishwa kwa mapigano kama "tumaini pekee la kuepusha umwagaji damu zaidi na kurejesha misaada inayohitajika kuliko wakati mwingine wowote”.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA "Wakati mashambulizi ya wanajeshi wa Israel yanapozidi huko Rafah, watu wanaendelea kulazimika kuondoka". 

Katika tarifa hiyo iliyochapishwa kupitia mtandao wa X UNRWA imeongeza kuwa  "Takriban watu 110,000 sasa wamekimbia Rafah kwenda kutafuta usalama. Lakini, hakuna mahali palipo salama katika Ukanda wa Gaza na hali ya maisha ni ya kutisha. Tumaini pekee ni kusitisha mapigano mara moja."

Mbali na tishio la mara moja la hatua za kijeshi zinazoendelea, mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa yameonya kuhusu kuongezeka kwa dharura tangu vifaru vya Israel vilipoingia kwenye kivuko cha mpaka cha Rafah Jumatatu na kwamba operesheni ya kibinadamu katika eneo hilo imelemazwa.

Mratibu Mwandamizi wa Dharura wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF katika Ukanda wa Gaza, Hamish Young amesema "Hali haiwezekani, tena na itakuwa mbaya zaidi ikiwa shughuli za kibinadamu hazitafufuliwa katika saa 48 zijazo." 

UN yashambuliwa

Katika tukio linalohusiana na hilo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amelaani vikali shambulio jipya la waandamanaji kwenye kituo cha UNRWA mjini Jerusalem.

Katika chapisholake kwenye mtandao wa X mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema "Ninalaani shambulio la hivi majuzi kwenye Makao Makuu ya UNRWA huko Jerusalem Mashariki. Kulenga wafanyakazi wa misaada na mali za kibinadamu haikukubaliki, na lazima hali hiyo ikomeshwe.” 

Maoni yake yamesisitiza yale yaliyosemwa na Kamishna Mkuu wa UNRWA Philippe Lazzarini siku ya Alhamisi ambaye aliripoti kwamba wakazi wa Israel "wamechoma moto mara mbili kwenye eneo la makao makuu ya shirika hilo, ikiwa ni mara ya pili UNRWA kulengwa katika wiki moja kati ya wiki za maandamano.

Watu kutawanywa tena

Huko Gaza, picha za hivi karibuni kabisa kutoka Rafah zilizotolewa na UNRWA zinaonyesha msururu wa watu wakiondoka mashariki mwa mji huo wakiwa na magari, pikipiki na mikokoteni ya punda iliyosheheni mali zao kuitikia amri ya kuwahamisha iliyotolewa na wanajeshi wa Israel.

Wengi wa waliokimbia makazi yao wanatafuta usalama huko Khan Younis na Deir Al-Balah. Lakini, maeneo haya yanakosa huduma za msingi zinazohitajika kusaidia raia wanaohitaji chakula, malazi na huduma za afya, timu za misaada zinaendelea.

Barabara kuelekea ukanda wa pwani wa Al Mawasi, ambako wananchi wa Gaza wameagizwa kuhamia, "zimekwama", amesema Bwana Young wa UNICEF. Akizungumza na waandishi wa habari kutoka Rafah kupitia njia ya video Geneva Uswisi, ameelezea matukio ya kukatisha tamaa wakati familia zinaondolewa tena, na "mamia mengi ya malori, mabasi, magari na mikokoteni ya punda iliyopakia watu na mali ikiendelea kutoka nje ya jiji hilo la Kusini”. 

Ameongeza kuwa "Watu ninaozungumza nao wananiambia wamechoka, wana hofu na wanajua maisha ya Al Mawasi yatakuwa magumu tena. Familia hazina vifaa vya usafi, maji ya kunywa na makazi. Watu wanatengeneza vyoo vilivyoboreshwa kwa kuchimba mashimo ardhini kuzunguka vikundi vya mahema. Kujisaidia haja kubwa katika maeneo ya wazi kunaongezeka na ni hali inayoleta hofu ya kuzuka magonjwa.”

Amesema “Baba mmoja aliniambia hakuwa na chochote isipokuwa chaguzi mbaya za kuchagua. Na alipokuwa ananiambia anaenda wapi, alianza kulia. Kisha watoto wake wakaanza kulia na kuanza kuniuliza nifanye nini. Ni hali ya kusikitisha na hakuna mahali popote salama kwa watoto huko Gaza."