Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano huu wa asasi za kiraia ni muhimu kwa ajili mustakbali ujao: UN

Washiriki wakikusanyika katika ufunguzi wa mkutano wa Umoja wa Mataifa wa asasi za kiraia, unaofanyika katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa jijini Nairobi, Kenya, kuanzia tarehe 9-10 Mei 2024.
UN Nairobi
Washiriki wakikusanyika katika ufunguzi wa mkutano wa Umoja wa Mataifa wa asasi za kiraia, unaofanyika katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa jijini Nairobi, Kenya, kuanzia tarehe 9-10 Mei 2024.

Mkutano huu wa asasi za kiraia ni muhimu kwa ajili mustakbali ujao: UN

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Leo mkutano wa Umoja wa Mataifa wa asasi za kiraia umeng’oa nanga ukiwaleta pamoja washiriki zaidinya 3000 kutoka kila kona ya dunia wakijumuisha wawakilishi kutoka asasi za kiraia, serikali, maafisa wa Umoja wa Mataifa, vijana waleta mabadiliko, wanazuoni, wadau wengine na vyombo vya habari wakifanya majadiliano ya awali na kutoa takwimu kuelekea mkutano wa wakati ujao utakaofanyika New York Marekani mwezi Septemba mwaka huu.

Mkutano huu ambao umeandaliwa na Idara ya Umoja wa Mataifa ya Mawasiliano ya kimataifa DGC ni wa siku mbili na utafunga pazia kesho. 

Mabadiliko ya tabianchi ni changamoto kwa jamii zote

Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo Maher Nasser mwenyekiti mwenza wa kamati ya mipango ya mkutano wa 2024 wa asasi za kiraia na mkurugenzi wa kitengo cha uhamasishaji cha idara ya DGC amesema “mvua kubwa na mafuriko ya wiki iliyopita vimeacha vifo na uharibifu kote nchini Kenya na nchi jirani, hali mbaya ya hewa kwa mara nyingine tena imeonyesha kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi zimekuwa zikidhuru wale waliohusika kidogo kuchangia changamoto hii”.

Bwana Nasser ametoa salamu za rambirambi kwa waathiriwa, na mshikamano na jamii zilizoathiriwa. 

Amesema Idara ya Mawasiliano ya kimataifa haikuwahi kuandaa mkutano wa ukubwa huu, ambao umevutia watu wa ngazi za juu, katika muda mfupi kama huo. Zaidi ya wawakilishi 3,600 wa mashirika ya kiraia kutoka mashirika 2,750 walikuwa wamejiandikisha, pamoja na wawakilishi karibu 400 wa serikali 64, Mashirika saba ya Kiserikali ya Kimataifa (IGOs), mashirika 37 ya Umoja wa Mataifa na waandishi wa habari zaidi ya 100. 

Ameongeza kuwa asilimia 70 ya waliosajiliwa wametoka Afrika na asilimia 40 ya waliojiandikisha walikuwa vijana, katika kundi la umri wa miaka 18 hadi 34. 

Bwana Nasser amesea alitarajia matarajio ya mkutano huo yatafikiwa.

Maafisa wa Umoja wa Mataifa na viongozi wa mashirika ya kiraia wakiongoza ufunguzi wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Asasi za Kiraia, unaofanyika katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa jijini Nairobi, Kenya, kuanzia tarehe 9-10 Mei 2024.
UN Nairobi
Maafisa wa Umoja wa Mataifa na viongozi wa mashirika ya kiraia wakiongoza ufunguzi wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Asasi za Kiraia, unaofanyika katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa jijini Nairobi, Kenya, kuanzia tarehe 9-10 Mei 2024.

UN na wadau wanafanya kila wawezalo kusaidia

Zainab Hawa Bangura, mkurugenzi mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa Nairobi Kenya UNON, alianza kwa kuwakaribisha wageni Nairobi na kisha kuzungumzia athari ya mafuriko nchini humo ambayo yameharibu Kenya, Bi Bangura ametoa ujumbe wa Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa wa uungaji mkono na rambirambi kwa walioathirika. 

Amesema “Umoja wa Mataifa na washirika wao wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu kushughulikia mahitaji ya kibinadamu. 

Ameongeza kuwa UNON imekuwa makao makuu pekee ya Umoja wa Mataifa kusini mwa dunia, na imepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 69 wa Mashirika ya Kiraia jijini Nairobi, ambao ni mara ya kwanza kufanyika barani Afrika. 

Mkutano huo ambao unatoa fursa ya kipekee kwa mashirika ya kiraia na ushirikiano wa wadau mbalimbali umekuwa ni utangulizi muhimu wa mkutano wa kilele wa viongozi wa dunia wa siku zijazo utakaofanyika mwezi Septemba jijini New York Marekani.

Bi. Bangura amesisitiza kuwa asasi za kiraia zinachukua jukumu la msingi katika kuunda mustakabali, ambao leo zaidi ya hapo awali, unahitaji mbinu za kimataifa. Kama kiongozi wa zamani wa mashirika ya kiraia, Bi. Bangura anaelewa jukumu muhimu la mashirika ya kiraia duniani kote. 

Amewahimiza wajumbe wote kupaza sauti zao akisema UNON inasalia kuwa mshirika mkuu anayesaidia shughuli za Umoja wa Mataifa duniani kote na imekuwa kinara katika kazi endelevu. 

Ameongeza kuwa UNON inapitia mabadiliko ya kihistoria ambayo yanasongesha safari kuelekea nishati safi, kutoegemea upande wowote na bioanuwai. 

“Miradi miwili muhimu ya ujenzi wa mji mkuu, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa majengo sita mapya ya ofisi, na uboreshaji wa vifaa vya mikutano vyenye thamani ya jumla ya dola milioni 340, inawakilisha mradi muhimu zaidi wa miundombinu wa Umoja wa Mataifa barani Afrika. 

Kwa kumalizia, Bi. Bangura amezishukuru nchi wanachama na kutambua ushirikiano unaoendelea wa serikali ya Kenya kuelekea maendeleo ya miundombinu.

Wajumbe katika ufunguzi wa Kongamano la Mashirika ya Kiraia ya Umoja wa Mataifa jijini Nairobi, Kenya. Kwenye skrini, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammad.
UN Nairobi
Wajumbe katika ufunguzi wa Kongamano la Mashirika ya Kiraia ya Umoja wa Mataifa jijini Nairobi, Kenya. Kwenye skrini, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammad.

Machafuko Gaza na duniani kote yakome

Amina Mohammed, Naibu Katibu Mkuu, wa Umoja wa Mataifa  akizungumza kupitia ujumbe wa video, pia ametoa salamu zake za rambirambi kwa wahanga wa mafuriko makubwa nchini Kenya, akisisitiza kuendelea kujitolea kwa Umoja wa Mataifa kuunga mkono Serikali ya Kenya wakati huu wa changamoto. 

Akizungumzia vita inayoendelea Mashariki ya Kati Bi. Mohammed alisisitiza wito wa Katibu Mkuu wa kusitishwa mara moja kwa mapigano huko Gaza, kuachiliwa kwa mateka wote na upatikanaji salama na usiozuiliwa wa misaada ya kibinadamu. 

‘Sisi watu, ufunguzi wenye nguvu wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa, ulikuwa ni dhamira ya kuja pamoja kwa manufaa ya watu wote. Kila siku, mashirika ya kiraia duniani kote yanafanya kazi bila kuchoka kuendeleza malengo ya Umoja wa Mataifa, kupitia mapambano yao ya haki za kimataifa, kijamii, mabadiliko ya tabianchi na kwa ajili ya amani, usawa wa kijinsia na haki za binadamu. 

Ameongeza kuwa “Mkutano huu umekuwa ushuhuda wa sauti dhabiti ya mashirika ya kiraia, licha ya kuongezeka kwa vitisho na kupungua kwa fursa. 

Pia ameongeza inathibitisha kwamba mkutano ujao wa kilele wa “Wakati Ujao” utahitaji kuangazia vipaumbele vyao, wasiwasi wao, na matarajio yao. 

Amesema mkutano wa Septemba utakuwa fursa ya vizazi kurekebisha taasisi za kimataifa na kujenga umoja wa kimataifa unaojumuisha masilahi ya watu wote. Lakini fursa hiyo inaweza tu kuchukuliwa kwa ushiriki hai. 

Kati ya sasa na Septemba, maoni ya mashirika ya kiraia na ushiriki wa dhati unahitajika amesema Bi. Mohammed huku akihimiza mashirika ya kiraia kujihusisha kikamilifu na nchi wanachama na viongozi New York na katika miji mikuu kuunganisha nguvu na wenzao wa asasi za kiraia katika kanda na sababu; kuunganisha mabadiliko yanayohitajika katika mfumo wa kimataifa na mabadiliko ambayo watu wanahitaji kuona katika maisha yao ya kila siku na kufanya sauti zao zijumuishwe.