Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Iwapo ulizikosa wiki hii ya 22-26 Julai 2019

mtoto Mwigulu Matonange Magesa mwenye umri wa miaka 16 kutoka Tanzania anayeishi na ualbino.
UN News/Video capture
mtoto Mwigulu Matonange Magesa mwenye umri wa miaka 16 kutoka Tanzania anayeishi na ualbino.

Iwapo ulizikosa wiki hii ya 22-26 Julai 2019

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la nishati ya atomiki duniani, IAEA, Yukia Amano, aaga dunia, siku chache tu kabla ya kuwasilisha barua yake ya kujiuzulu wadhifa huo. Suala la wahamiaji na wakimbizi wanaosaka maisha bora barani Ulaya kupitia Mediteranea lapigiwa chepuo kwa hatua mpya chanya barani humo. Nchini Kenya mradi mpya kwenye pwani ya nchi hiyo washamirisha mikoko na biashara ya hewa ya ukaa. Baa la nzige latishia mustakabali wa chakula kwenye pembe ya Afrika na Yemen, na mtoto Mwigulu ambaye alikatwa mkono kisa tu ni albino azungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa.

Ni pigo kubwa kwetu kuondokewa na Yukiya Amano:IAEA

Yukiya Amani, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA aliyefariki dunia tarehe 22 Julai 2019

Shirika la kimataifa la nguvu za atomiki IAEA, Jumatatu ya tarehe 22 julai 2019 limetangaza kwa masikitoko makubwa kifo cha aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Yukiya Amano.

Amano raia wa Japan na mwanadplomasia aliyekuwa na umri wa miaka 72 ameliongoza shirika la IAEA tangu mwaka 2009 na kabla ya kuwa mkurugenzi mkuu wa shirika hilo alifanya kazi katika utumishi wa umma wa kimataifa kwenye Umoja wa Mataifa katika vitengo mbalimbali .

Uongozi wa IAEA umesema kumpoteza Amano ni pigo kubwa kwani alikuwa mchapa kazi aliyeipenda kazi yake kwa moyo wote,  "na katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, shirika limeleta matokeo halisi ili kufikia lengo la Atomiki kwa ajili ya amani na maendeleo, kutokana na msaada wa nchi wanachama na kujitolea kwa wafanyakazi wa shirika hili. Ninajivunia sana mafanikio yetu, na ninawashukuru nchi wanachama na wafanyakazi wa shirika hili. "

Makubaliano yaliyofikiwa EU kuhusu hali ya Mediteranea yatutia moyo- IOM/UNHCR

Maelfu kadhaa ya wasaka hiafdih na wahamiaji kutoka Syria, Iraq, Ethiopia, Sudan, Pakistan na Afghanistan wanaishi katika  kambi za kuhamahama au mitaani huko Calais nchini Ufaransa.

Viongozi wa mashirika mawili  ya Umoja wa Mataifa wamekaribisha uamuzi uliofikiwa barani Ulaya wenye lengo la kushughulikia hali wahamiaji na wakimbizi kwenye bahari ya Mediteranea na kuzuia vifo nchini Libya.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa IOM António Vitorino na lile la kuhudumia wakimbizi, UNHCR Filippo Grandi wamesema hayo kufuatia makubaliano yaliyotokana na mjadala uliofanyika mjini Paris, Ufaransa miongoni mwa mataifa ya Ulaya.

“Tunakabirisha makubaliano ya leo kuhusu umuhimu wa kumaliza ushikiliaji holela wa wakimbizi na wahamiaji nchini Libya. Kuna umuhimu wa kuwepo kwa mchakato halali wa kuachia watu wanaoshikiliwa kwenye vituo iwe mijini au kuwepo kwa maeneo ya wazi ya kuwawezesha kutembea huru na kupata msaada bila kudhurika,” wamesema viongozi hao kupitia taarifa yao ya pamoja.

Mauzo ya hewa ya ukaa ni ushindi kwa uhifadhi wa mazingira na kipato  Kenya-UN Environment

Mikoko baharini

Shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, UN Environment, halmashauri ya misitu Kenya na taasisi ya utafiti ya viumbe baharí na samaki Kenya na wadau hivi karibuni wamezindua mradi katika pwani ya Kenya kwa ajili ya kukuza biashara ya hewa ya mkaa kufuatia uhifadhi na upanzi wa mikoko. 

Taarifa ya UN Environment iliyotolewa Nairobi, Kenya, inasema kuwa wakati kunapatikana mfumo wa kuhifadhi mazingira na unaopunguza umasikini na kujengea jamii mnepo kiuchumi, kwa kawaida serikali hupiga jeki hatua kama hizo na kwa hiyo ni suluhu ya ushindi kwa pande zote.

Ripoti zinasema kuwa kwa  sasa kuna upungufu wa mikoko kwa sababu ilikuwa inavunwa kupita kiasi kwa ajili ya kuni na mbao za ujenzi, hali ambayo inazua hatari kwani jamii nyingi zinazotegemea uvuvi, huku maeneo ya mikoko yakiwa ni maeneo ya mazalia ya samaki. 

FAO yaonya kuhusu mlipuko wa nzige wa jangwani Yemen na pembe ya Afrika

Nzige hawa ni hatari kwa mazao shambani

Shirika la chakula na kilimo FAO leo limetoa onyo dhidi ya mlipuko wa nzige wa jangwani katika eneo la Pembe ya afrika na Yemen, likisema nzige hao waliochochewa na mvua kubwa wanaweza kuwa tishio kubwa kwa uzalishaji wa kilimo katika miezi mitatu ijayo. 

Kwa mujibu wa shirika hilo maeneo yaliyo hatarini zaidi ni Yemen, Sudan, Eritrea na baadhi ya sehemu za Ethiopia na Kaskazini mwa Somalia. Limeongeza kuwa “hali hiyo inaweza kusababisha athari kubwa katika mazao ya msimu wa kilimo na uchumi wa maeneo hayo kitu ambacho ni tisho la uhakika wa chakula  na maisha ya watu wa nchi husika."

Napenda niwe mchezaji mashuhuri wa mpira wa soka kama Ronaldo- Mwigulu

mtoto Mwigulu Matonange Magesa mwenye umri wa miaka 16 kutoka Tanzania anayeishi na ualbino.

Licha ya kupungua kwa vitendo vya mashambulizi dhidi ya watu wenye ualbino, bado kundi hilo linaishi kwa mashaka na hofu kutokana na madhila wanayopitia katika maisha yao ya kila siku.

Miongoni mwao ni mtoto mtanzania Mwigulu Matonange Magesa ambaye sasa ana umri wa miaka 16, na ambaye mashambulizi dhidi yake yamemsababishia kupoteza mkono wake mmoja katika kisa hiki anachosimulia alipohojiwa na Priscilla Lecomte wakati alipotembelea New York, MArekani hivi karibuni kushiriki mkutano wa kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya watu wenye Ulemavu.