Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatutawaacha raia wa Gaza waliosaka hifadhi Rafah- UNRWA

Madhara ya mashmbulizi Rafah yanaweza kusambaratisha watu milioni 1.4 walioko  Rafah, yaonya UN.
UNRWA
Madhara ya mashmbulizi Rafah yanaweza kusambaratisha watu milioni 1.4 walioko Rafah, yaonya UN.

Hatutawaacha raia wa Gaza waliosaka hifadhi Rafah- UNRWA

Amani na Usalama

Huku kukiwa na ripoti ya kwamba wapalestina 100,00 wameamriwa kuhama Rafah kusini mwa Gaza kabla ya operesheni ya kijeshi inayotarajiwa kufanywa na jeshi la Israel, mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayotoa huduma za kibinadamu yameonya kuwa hayana nia ya kuondoka mji huo muhimu zaidi wenye misaada ya kiutu,

“Shambulio ya Israel dhidi ya Rafah, litamaanisha kuwa raia zaidi watapata machungu na kufa, Madhara yake yatakuwa makubwa na ya kutisha kwa watu milioni 1.4 walioko eneo hilo,” limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA kupitia ukurasa wake wa X, zamani Twitter.

Shirika hilo limesema halitaondoka Rafah, bali litaendelea kuweko eneo hilo kwa kadri inavyowezekana na litaendelea kusambaza misaada ya kiutu ya kuokoa maisha ya watu.

“Shambulio ya Israel dhidi ya Rafah, litamaanisha kuwa raia zaidi watapata machungu na kufa, Madhara yake yatakuwa makubwa na ya kutisha kwa watu milioni 1.4 walioko eneo hilo,” limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA kupitia ukurasa wake wa X, zamani Twitter.

Shirika hilo limesema halitaondoka Rafah, bali litaendelea kuweko eneo hilo kwa kadri inavyowezekana na litaendelea kusambaza misaada ya kiutu ya kuokoa maisha ya watu.

Raia wengi wa Gaza sasa wanaishi kwenye mahema huko Rafah, mji wa kusini zaidi ukanda wa Gaza.
© UNICEF/Eyad El Baba
Raia wengi wa Gaza sasa wanaishi kwenye mahema huko Rafah, mji wa kusini zaidi ukanda wa Gaza.

GAZA: Watoto walioko Rafah wasihamishwe kwani tayari wako taabani- UNICEF

Kauli ya janga linaloweza kutokea Rafah limepatiwa msisitizo pia na shirika la  Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF ambalo linaonya kuwa kuzingirwa kijeshi kwa eneo hilo sambamba na operesheni za ardhini za kijeshi huko Rafah kutasababisha janga kubwa kwa watoto 600,000 waliosaka hifadhi kwenye eneo hilo. 

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo mjini New York, Marekani inakumbusha kuwa amri ya kuhamia Rafah, kusini mwa Gaza iliyotolewa mwezi Oktoba mwaka jana na Israel imefanya eneo hilo sasa kuhifadhi watu wapatao milioi 1.2, nusu yao wakiwa ni watoto wakiishi kwenye mahema au nyumba zisizo kamilifu.

Kwa kuzingatia mlundikano wa watoto, wakiwemo wengi walio hatarini wakihaha kuishi, pamoja na ukubwa wa ghasia zinazoendelea na njia za kutumia kukimbia zikiwa na vilipuzi au hakuna njia kabisa , UNICEF inaonya madhila zaidi kwa watoto na operesheni za kijeshi vitaongeza vifo zaidi vya raia na miundombinu ya huduma za msingi iliyosalia kusambaratishwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Catherine Russell amesema zaidi ya siku 200 za vita zimekuwa ‘mwiba’ kwa watoto na Rafah hivi sasa ni mji wa watoto wasio na pahala salama pa kukimbilia Gaza. Iwapo operesheni kubwa za kijeshi zikianza, watoto sio tu watakuwa hatarini na ghasia, bali pia vurugu na kiwewe wakati ambapo hali zao kimwili na kiakili zimeshadhoofishwa.

Hivyo UNICEF inasisitiza wito wa Kamati ya Mashirika ya UN kwa Israel ya kuzingatia wajibu wake kwa mujibu wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu na haki za binadamu ya kupatia chakula na matibabu watoto na kuwezesha operesheni za kugawa misaada na kwa viongozi wa dunia kuzuia janga zaidi kwa watoto Gaza sambamba na sitisho la mapigano.

Baa la njaa Gaza Kaskazini- UNICEF

Wakati huo huo, mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula, Cindy McCain siku ya Jumapili alisema kuwa eneo la Gaza kaskazini sasa linakabiliwa na baa la njaa ambalo sasa linaelekea kusini.

Bi. McCain amepazia sauti hofu kubwa na inayoelezwa mara kwa mara kutoka kwa maafisa waandamizi wa Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa kuhusu vikwazo vya kufikisha misaada pamoja na ucheleweshaji unaowekwa na mamlaka za Israel.

“Mamlaka za Israel zinaendelea kunyima Umoja wa Mataifa kibali cha kufikisha misaada yakiutu,” amesisitiza Philippe Lazzarini, Mkuu wa UNRWA.

“Wiki mbili zilizopita tu, tumerekodi matukio 10 ya mashambulizi dhidi ya misafara ya misaada ya kiutu, kukamatwa kwa watumishi wa Umoja wa Mataifa, kufanyiwa uonevu, kuvuliwa nguo na kuachwa uchi, vitisho kwa kutumia silaha na uchelewashaji wa muda mrefu kwenye vituo vya ukaguzi vikilazimisha misafara kusafiri usiku au kuacha kusafiri,” amesema Jumapili Bwana Lazarrini kupitia mtandao wa X.

Kamishna Mkuu huyo wa UNRWA amelaani pia mashambulizi ya makombora kwenye kivuko cha Kerem Shalom, mashambulizi yaliyosababisha vifo vya askari watatu wa Israel na hivyo kufanya kivuko kufungwa. Kivuko hicho ni lango muhimu na kuu la kupitishia misaada ya kibinadamu.

Louise Wateridge, Afisa kutoka UNRWA akiwa mji wa Rafah, kusini mwa Gaza.
UNRWA/Louise Wateridge
Louise Wateridge, Afisa kutoka UNRWA akiwa mji wa Rafah, kusini mwa Gaza.

‘Al Mawasi si salama’

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, vipeperushwa vilivyoangushwa kutoka angani na jeshi la Israel linashauri jamii kuhamia ukanda salama wa Al Mawasi, magharibi mwa Rafah karibu na bahari ya Mediteranea.

Mashiirika ya Umoja wa MAtaifa ya kutoa misaada ya kibinadamu awali yalikataa mipango hiyo ya kuhamisha raia inayofanywa na jeshi la Israel kwa misingi kwamba ni sawa na kulazimisha watu kuhama makwao.

“Huko Al Mawasi kuna ukosefu mkubwa wa miundombinu ikiewemo maji, na hapafai kupatia misaada makumi ya maelfu ya wakimbizi eneo hilo,” amesema msemaji wa UNRWA huko Gaza, Louise Wateridge akizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa.

Tangu Oktoba 7, 2023, wakati mashambulizi ya Hamas dhidi ya eneo la kusini mwa Israel yalipochochea Israel kuanza mashambulizi ya makombora na operesheni za ardhini dhidi ya Gaza, takribani wapalestina 34,680 wameuawa, wakiwemo watoto zaidi ya 14,000 na watu wengine zaidi ya 78,000 wamejeruhiwa, imesema mamlaka za afya za Gaza.