Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

GAZA: Hospitali ya Al-Shifa yafananishwa na eneo la umwagaji damu

Wafanyakazi wa WHO walishiriki katika msafara wa pamoja wa UN kwenye hosptali ya Al-Shifa kwa ajili ya kupeleka vifaa ya matibabu na kuona hali halisi.
WHO
Wafanyakazi wa WHO walishiriki katika msafara wa pamoja wa UN kwenye hosptali ya Al-Shifa kwa ajili ya kupeleka vifaa ya matibabu na kuona hali halisi.

GAZA: Hospitali ya Al-Shifa yafananishwa na eneo la umwagaji damu

Amani na Usalama

Wafanyakaizi wa Umoja wa Mataifa waliopeleka vifaa vya matibabu kwenye hospitali ya Al-Shifa huko kaskazini mwa Gaza siku ya Jumamosi wamefananisha Wodi ya Dharura kwenye hospitali hiyo na eneo la umwagaji damu ambako kumefurika mamia ya majeruhi, huku kila wakati wagonjwa wapya wakiingia.

Kwa mujibu wa timu hiyo, wagonjwa waliokumbwa na kiwewe wamelazwa kwenye sakafu, hospitali haina dawa yoyote ya kupunguza maumivu, na idara hiyo ya dharura imejaa kiasi kwamba wafanyakazi wanakuwa makini ili wasikanyage wagonjwa waliolala sakafuni.

Hospitali ya Al-Shifa, zamani ikiwa ndio hospitali muhimu zaidi na kubwa ya rufaa huko Gaza, hivi sasa ni kama haifanyi kazi kama ilivyokuwa: vyumba vya upasuaji na huduma nyingine kubwa hazifanyi kazi kutokana na ukosefu wa Oksijeni, madaktari bingwa na vifaa vya matibabu.

Kwa sasa hospitali hiyo ina uwezo wa kutoa huduma za msingi kwa waliokumbwa na kiwewe kutokana na mapigano yanayoendelea kwenye eneo hilo kati ya Israeli na wanamgambo wa kipalestina wa Hamas. Hospitali haina damu ya kupatia wagonjwa.

Wagonjwa wachache walioko pamoja na wauguzi na wafanyakazi 70 wa kujitolea, wanafanya kazi chini ya kile ambacho shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni , WHO linasema “mazingira magumu ya kipekee,” kwenye hospitali “ambayo inahitaji kukwamuliwa.

Kupitia taarifa yake iliyotolewa leo, WHO inasema katika wiki chache zijazo imejizatiti kuimarisha hospitali ya Al-Shifa ili iweze kurejea katika angalau uwezo wa kutoa huduma za msingi, kama vile huduma za kuokoa maisha, na kusadia watu walionaswa kwenye mzunguko wa kifo, uharibifu, njaa na magonjwa.

Vitu vinavyohitajika

Kwa sasa madaktari bingwa, wauguzi na wafanyakazi wa usaidizi wanahitajika, ikiwemo pia watoa huduma idara ya dharura. Halikadhalika mahitaji ya msingi ya kibinadamu: Makumi ya maelfu ya watu waliofurushwa makwao wamesaka hifadhi kwenye hospitali hiyo, ambayo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji safi na chakula.

Kwa sasa, hospitali ya Al-Ahli Arab imesalia kuwa hospitali ambayo angalau inatoa huduma kaskazini mwa Gaza, sambamba na hospitali nyingine za Al-Shifa, Al Awda na Al Sahaba. Kabla ya kuanza kwa mapigano Oktoba 7, kulikuwa na jumla ya hospitali 24 zinazofanya kazi.

Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa katika hospitali ya Al-Shifa walikuwa kwenye ziara ya pamoja ya UN ikileta watendaji kutoka WHO, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa misaada ya dharura, OCHA, Idara ya Umoja wa Mataifa ya Usalama na Ulinzi, UNDCC, na Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na mabomu ya kutegwa ardhini, UNMAS. Timu hiyo ilipeleka hospitali hapo vifaa vya matibabu na upasuaji, mathalani upasuaji wa mifupa na dawa za usingizi zinazotumika wakati wa upasuaji wa wagonjwa.