Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafuriko Kenya: Mgao wa fedha waleta matumaini kwa wakazi wa Kaunti ya Mto Tana- UNICEF

Eva Ghamaharo, mkazi wa Kaunti ya  Mto Tana, mnufaika wa mradi wa dharura wa mgao wa fedha kwa manusura wa mafuriko unaotekelezwa na UNICEF Kenya.
UNICEF/James Ekwam
Eva Ghamaharo, mkazi wa Kaunti ya Mto Tana, mnufaika wa mradi wa dharura wa mgao wa fedha kwa manusura wa mafuriko unaotekelezwa na UNICEF Kenya.

Mafuriko Kenya: Mgao wa fedha waleta matumaini kwa wakazi wa Kaunti ya Mto Tana- UNICEF

Msaada wa Kibinadamu

Wingu kubwa la mvua likiwa limetanda kwenye mji wa Garsen, ulioko kaunti ya Mto Tana nchini Kenya, Eva Ghamaharo, mama wa watoto watatu anarejea nyumbani akitembea na watoto wake wawili mapacha wenye umri wa miaka mitatu baada ya kununua matumizi ya nyumbani kutoka kioski cha jirani. Watoto hawa wawili mapacha wa kike ni Grace na Jane na wanaonekana na furaha kwani angalau leo mama yao ameweza kuwanunulia kila mmoja pakiti ya maziwa na wanakunywa kwa furaha.

Wanaingia nyumbani mwao na mama yao anatoa kwenye mfuko mchele, unga wa kupikia uji, vitunguu na nyanya.

Eva ni mnufaika wa mpango wa mgao wa fedha za dharura kwa familia zilizoathiriwa na mafuriko kwenye kaunti ya mto Tana. Mradi huo unatekelezwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF nchini Kenya kwa ushirikiano na Idara ya Serikali ya Hifadhi ya Jamii na Mamlaka ya Kitaifa ya usimamizi wa Ukame.

Mafuriko yalisomba makazi na mbinu za kujipatia kipato

Mradi unalenga kuwapatia kila mwezi mgao wa fedha taslimu shilingi 2,700 za Kenya sawa na takribani dola 20 za kimarekani. Fedha zinasaidia familia kama ya Eva kujikimu na mahitaji muhimu.

Eva anasema mafuriko ya mweiz Desemba mwaka jana yaliwaletea maafa makubwa kwani yeye kama mzazi pekee kwa watoto wake alikuwa anauza mihogo ya kukaaanga na kushona nguo lakini, mvua ziliponyesha, “maisha yalikuwa magumu kwa sababu mafuriko yaliharibu nyumba na mashamba. Vyakula vilisombwa. Watu wengi waliteseka sana. Maafisa wa kaunti waliona tunateseka, walitembea nyumba kwa nyumba wakisajili majina watu wenye watoto na wajauzito. Nilikuwa nikipata shilingi 2,750.”

Tina Mula, akiwa amesimama nje ya nyumba yake huko mjini Garsen kaunti ya Mto Tana nchini Kenya. Yeye ni mnufaika wa mradi wa mgao wa fedha za dharura kwa manusura wa mafuriko unaotekelezwa na UNICEF, Kenya.
UNICEF/James Ekwam
Tina Mula, akiwa amesimama nje ya nyumba yake huko mjini Garsen kaunti ya Mto Tana nchini Kenya. Yeye ni mnufaika wa mradi wa mgao wa fedha za dharura kwa manusura wa mafuriko unaotekelezwa na UNICEF, Kenya.

Mradi wafikia kaya 1,800 Galole na Garsen

Rachael Wamoto ni afisa kutoka UNICEF Kenya na anafafanua kuhusu usaidizi huo ambao haukulenga tu waathiriwa wa mafuriko bali pia kaya zenye watoto walio na utapiamlo.

Bi. Wamoto anasema, “kwa programu hii tuko katika kaunti sita. Kwa kaunti ya Mto Tana tumeweza kufikia kaya 1,800 katika miji ya Galole na Garsen. Vikundi kazi vya Kaunti ndio vilihusika kwenye kuchagua kaya zenye uhitaji. Hivyo tuliweza kutambua watu walioathiriwa na mafuriko na waliokimbia makwao.”

UNICEF Kenya inashirikiana na serikali na mamlaka ya taifa ya udhibiti wa ukame ushirikiano ambao umewawezesha kutumia orodha yao na hivyo kufikia haraka wahitaji.

Msaada wa fedha taslimu uliofadhiliwa na serikali ya Uingereza, umekuwa na manufaa kwa Eva kwani pamoja na kununua matumizi ya nyumbani, “watoto wangu hawa mapacha niliwaandikisha shule nikawanunulia sare na mabegi ya shule. Nimeshukuru sana UNICEF kwa msaada wao kwa sababu mmetusaidia.”

Kuku wangu wa mayai nao walisombwa na maji

Mita chache kutoka nyumbani kwa Eva, ni makazi ya Tina Mula, mama mjamzito mwenye umri wa miaka 34. Anatarajia kujifungua mtoto wake wa pili. Mafuriko yalipokuja, yeye na familia yake walilazimika kusaka makazi kwenye shule ya jirani.

“Nyumba na mali zao zote vilisombwa pamoja na kuku ambao alikuwa anafuga ili kujipatia kipato baada ya kuuza mayai yao,” inasema UNICEF.

Mgao wa fedha umemwezesha kununua mchele, unga wa mahindi na mafuta ya kupikia. Ameweza pia kumrejesha mwanawe wa kwanza shuleni.

Kwa miaka kadhaa sasa Kaunti ya Mto Tana imekuwa ikiathiriwa na mafuriko kwani mabadiliko ya tabianchi yamebadili mwenendo wa hali ya hewa, hivyo mgao wa fedha kwa familia ya Eva na Tina umeziwezesha familia kurejea angalau katika maisha ya kawaida.

Soma taarifa nzima ya UNICEF hapa.