Asante UNICEF kwa kutusaidia wakati huu wa mafuriko:Waathirika Kenya  

31 Agosti 2020

Waathirika wa mafuriko makubwa yanayokumba maeneo mbalimbali ya Mashariki mwa Afrika na kusababisha athari  ikiwemo watu kupoteza kila kitu, hususan  nchini Kenya wamelishukuru shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF kwa kuwasaidia. 

Katika eneo la Bunyala , kaunti ya Busia jimbo la Magharibi mwa Kenya ambako kwa mujibu wa UNICEF  watu 81,000 wameatirika na mafuriko yanayoendelea kwa miezi kadhaa sasa kutokana na mvua kubwa zinazonyesha. 

Watu kutoka kaya zaidi ya 5,000 wametawanywa na kupoteza makazi na sasa wanapatiwa hifadhi katika makazi ya muda kwenye eneo la Namenya jimboni humo. 

Mama huyu kutoka kitongoji cha Namagusi ni miongoni mwa waathirika ,“kwa jina naitwa Hellen Adhiambo, mimi ni mkazi wa Namagusi Kijiji cha Malomba. Na ni mmoja wa wale walioathirika na mafuriko , tulitoka huko tukaja hapa Namenya, na tumekuwa hapa kwa muda wa miezi miwili sasa.” 

UNICEF imekuwa ikiwasaidia waathirika hawa ambao wengine wamepoteza kila kitu. Abdi Hassan ni mtaalam wa masuala ya maji na usafi (WASH) wa UNICEF Kenya, “wakati watu wanapotawanywa hususan kutoka kaya masikini basi watoto wanaweza kuwa katika hatari ya magonjwa yatokanayo na maji kama kuhara, kipindupindu na kwa sasa hata COVID-19, ni kwa sababu mara nyingi hawana fursa ya kupata maji salama na sabuni kwa ajili ya kunawa mikono .” 

Lakini UNICEF imekuwa mkombozi wao wakati huu wa mafuriko kwa kuwagawia vifaa kwa ajili ya huduma za WASH zikiwemo tembe za kusafisha maji. Na kwa msaada huo Hellen kwa niaba ya waathirika wengine anasema asante, “kwa sasa tunalishukuru shirika la UNICEF kwa maana limetusaidia, tumepata madumu na ndoo za maji na hata tembe wametupa sasa tunakunywa maji masafi na salama na hata watu wa kampeni wameweza kuja kututembelea na kutuelimisha kuhusu usafi, kwa hivyo  hata katika hii kambi yetu tunadumisha usafi na tunashukuru.” 

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud