Kenya yapeleka misaada kwa waathirika wa mafuriko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo:WFP

11 Novemba 2019

Kufuatia ombi maalum la serikali ya Kenya helikopta ya shirika la mpango wa chakula duniani WFP imeanza kusafirisha na kufikisha msaada wa chakula wa kuokoa maisha ya mamia ya familia katika kaunti za Mandera, Wajir, Garissa na Tana River zilizokumbwa na mafuriko. 

Msaada huo wa chakula umetolewa na serikali ya Kenya kwa ajili ya maeneo hayo ambayo hayafikiki kufuatia mafuriko makubwa. “

Wakati tumetenga msaada wa kukidhi mahitaji ya familia zilizoathirika na mafuriko , tunakabiliwa na changamoto kubwa ya kuifikisha misaada hiyo kwa sababu ya vikwazo vya usafiri. Hivyo tumeiomba WFP kutusaidia na usafiri wa helkopta ili kutuwezesha kuendelea na shughuli za kupeleka misaada.” Amesema Waziri Eugene Wamalwa kutoka wizara ya serikali za majimbo na maeneo ynayoathirika na ukame.

Ameongeza kuwa tangu kuanza kwa mvua mapema mwezi Oktoba mwaka huu, mafuriko yameharibu madaraja na barabara nyingi kutoweza kutumika hususani maeneo ya Kaskazini Mashariki mwa Kenya, na kusababisha adha kubwa ya usafiri.

Idara ya utabiri wa hali ya hewa nchini Kenya inasema mvua katika maeneo kame na yenye ukame kiasi hadi sasa imekuwa ni mara mbili au tatu ya kiwango cha kawaida na utabiri unaonyesha mvua itakubwa kubwa zaidi katikati ya mwezi Novemba.

Mwakilishi na Mkurugenzi wa WFP nchini Kenya Annalisa Conte amesema “serikali ya Kenya inachukua uongozi imara katika kuwafikia watu ambao maisha yao yameathirika na mafuriko. WFP kwa kutumia uwezo wake wa kimataifa inaandaa usafiri wa anga kusaidia juhudi za misaada ya serikali na kuhakikisha misaada hiyo ya kuokoa maisha inafikishwa kwa walengwa na kwa wakati.

Kwa miaka mingi serikali ya Kenya kupitia wizara ya majimbo wamekuwa wakishirikiana katika ufuatiliaji wa athari za kimazingira na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo majanga ya asili, ukame na mafuriko.

TAGS: WFP, mafuriko, Kenya, misaada

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter