Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kulipiza kisasi hakufai kutaongeza madhara Mashariki ya Kati - António Guterres

Mvulana mdogo akibembelezwa na timu ya kliniki ya dharura Kaskazini mwa Gaza.
© WHO
Mvulana mdogo akibembelezwa na timu ya kliniki ya dharura Kaskazini mwa Gaza.

Kulipiza kisasi hakufai kutaongeza madhara Mashariki ya Kati - António Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amerudia kusema kwamba ni wakati muafaka kusitisha mzunguko hatari wa kulipiza kisasi katika Mashariki ya Kati.

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake asubuhi hii ya Ijumaa ya tarehe 19 Aprili kwa saa za New York, Marekani, Katibu Mkuu amelaani kitendo chochote cha kulipiza kisasi na anatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kufanya kazi pamoja ili kuzuia uendeleaji wowote zaidi unaoweza kusababisha madhara makubwa kwa eneo zima la mashariki ya kati na kwingineko.

Wito huu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa unakuja baada ya Israel jana usiku wa Aprili 18 kuishambulia Iran kwa kombora katika mji wa Isfahan ulioko katikati mwa nchi.

Duru zinadai shambulio hilo la Israel ni la kulipiza kisasi dhidi ya shambulizi lililotekelezwa na Iran dhidi yake Jumamosi ya Aprili 13 mwaka huu.

Ikumbukwe pia kuwa shambulio hilo la Iran dhidi Israel lilikuwa la kulipiza kisasi baada ya Israel kuwa imeshambulia ubalozi wa Iran mjini Damascus, Syria katika siku ya kwanza ya mwezi huu wa Aprili 2024.

Rafael Mariano Grossi Mkurugenzi mkuu wa shirika la kimataifa la nishati ya atomic IAEA
UN Photo/Loey Felipe
Rafael Mariano Grossi Mkurugenzi mkuu wa shirika la kimataifa la nishati ya atomic IAEA

Hakuna uharibifu Kwenye kinu cha nyuklia cha Iran

Shirika la Umoja wa Mataifa la nguvu ya nishati ya nyuklia IAEA limesema linaweza kuthibitisha kwamba hakuna uharibifu wowote katika maeneo ya kinu cha nyuklia cha Iran, na Mkurugenzi Mkuu wa shirikahilo Rafael Mariano Grossi "anaendelea kutoa wito wa kujizuia kwa hali ya juu kwa kila mtu na kusisitiza kwamba vifaa vya nyuklia haipaswi kulengwa katika migogoro ya kijeshi." Shirika hilo la la Kimataifa la Nishati ya Atomiki limesema hayo kufuatia ripoti za vyombo vya habari ambazo hazijathibitishwa kwamba huenda mashambulizi ya ndege zisizo na rubani yalilenga mkoa wa Isfahan wa Iran, ambao ni nyumbani kwa vituo vya nyuklia na ngome za kijeshi.

Huko Geneva Uswisi, pia, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu, OHCHR, imezitaka pande zote "kuchukua hatua za kukomesha hali hiyo haraka.

"Tunatoa wito kwa Mataifa ya tatu, hasa yale yenye ushawishi, kufanya yote yaliyo katika uwezo wao kuhakikisha hakuna kuzorota zaidi katika hali ambayo tayari ni ya hatari," amesema msemaji wa OHCHR Jeremy Laurence.

Njaa na hofu

Huko Gaza, timu za misaada zimetoa ufahamu mpya juu ya hatari zinazowakabili raia wa Palestina haswa wanawake wajawazito na akina mama wanaonyonyesha  kama matokeo ya "uharibifu mkubwa wa vifaa tiba muhimu na upungufu wa maji mwilini, utapiamlo na hofu miongoni mwa Wapalestina.”

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Dominic Allen, mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya ya uzazi UNFPA kwa ajili ya eneo la Palestina, amesema kuna dalili kwamba idadi ya watoto wanaozaliwa ni karibu mara mbili ya ilivyokuwa kabla ya vita kuzuka.

"Kuna ongezeko la idadi," amesema, akiongeza kuwa kabla ya vita, karibu asilimia 15 ya watoto wanaozaliwa walihitaji aina fulani ya huduma ya dharura ya uzazi. 

Leo, baadhi ya madaktari wameripoti "kuongezeka maradufu kwa matatizo yale waliyokuwa wameshughulikia hapo awali, na hii ni kutokana na utapiamlo, upungufu wa maji mwilini na hofu, ambayo huathiri uwezo wa mwanamke mjamzito kujifungua salama na kubeba mtoto wake hadi muhula kamili kwa usalama," amesema afisa huyo wa UNFPA.

Watoto wakiwa nje ya moja ya majengo yaliyosambaratishwa kwa makombira  Deir Al-Balah Katikati mwa Gaza
© UNRWA
Watoto wakiwa nje ya moja ya majengo yaliyosambaratishwa kwa makombira Deir Al-Balah Katikati mwa Gaza

Uharibifu uliokithiri

Bwana Allen ameelezea dhamira yake ya hivi karibuni huko Gaza kutathmini athari za mashambulizi ya Israel kwenye huduma za afya katika hospitali zinazokabiliwa na mashambulizi katika maeneo ya kaskazini, kati na kusini.

Ilikuwa bayana kwamba hospitali za mwisho zilizosalia katika eneo hilo ikiwa ni pamoja na hospitali ya pili kwa ukubwa, ya Nasser "Ziko katika hatihati ilhali ni njia ya kuokoa maisha ya wanawake wajawazito wa Gaza", Bw.ana Allen amesema kupitia taarifa aliyoitoa kwa njia ya video kutoka Jerusalem. Ameongeza kuwa “Nilichokiona, kinanivunja moyo. Hakielezeki. Tunachoona hapo ni vifaa vya matibabu, vilivyovunjwa kwa makusudi, vipimo vya uchunguzi wa ultrasound  ambavyo utajua ni zana muhimu sana ya kusaidia kuhakikisha uzazi salama kwa nyaya ambazo zimekatwa, skrini za vifaa vya matibabu muhimu kama vile ultrasound na vingine vilivyovunjwa skrini. Kwa hivyo, uharibifu wa makusudi na mbaya umefanyika katika wodi ya wazazi.

Kabla ya mashambulizi makali ya Israel kuanza ili kujibu mashambulizi ya kigaidi yanayoongozwa na Hamas kote kusini mwa Israeli tarehe 7 Oktoba mwaka jana, Hospitali ya Nasser katika mji wa kusini wa Khan Younis ilikuwa na wodi ya wazazi ambayo timu za UNFPA zimesaidia kwa miaka mingi.

Ili kufanya kazi kikamilifu tena, hospitali itahitaji huduma za maji na usafi wa mazingira zilizorekebishwa na ukarabati wa jenereta za umeme zilizoharibika, kwa kiwango cha chini kabisa. “Lakini, nilisimama kando ya ghala ambapo tulipeleka vifaa miezi mingi iliyopita na lilikuwa linawaka linateketea, kuna kazi nyingi na kubwa ya kufanya katika suala la kujaribu kuanzisha upya njia hiyo ya maisha,” amesema Allen.

Watoto karika hospitali ya Al-Shifa Kaskazini mwa Gaza (kutoka Maktaba)
© UNICEF/Eyad El Baba
Watoto karika hospitali ya Al-Shifa Kaskazini mwa Gaza (kutoka Maktaba)

Kutanda kwa hofu

Ujumbe wa UNFPA ulioanza Jumatatu tarehe 8 Aprili na kumalizika Jumatano wiki hii, ulitekelezwa kwa ushirikiano na Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa WHO, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, na shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA.

Lengo lilikuwa kutembelea karibu hospitali 10 huko Gaza, miongoni mwao zikiwemo Hospitali ya Al Aqsa katikati mwa Gaza, ambayo ilikuwa "imezidiwa na wagonjwa wenye kiwewe na haikusaidia huduma ya uzazi.

Katika Hospitali ya Emirati kusini mwa eneo hilo, Bwana Allen alisimulia alipokutana na mkurugenzi wa matibabu wa kituo hicho ambaye alisema kwamba "haoni tena watoto wa kawaida."

Akigeukia Rafah na kuendelea na hofu ya uvamizi wa Israel, afisa huyo wa UNFPA amesisitiza kuwa "hisia kubwa za hofu imewaghubika zaidi ya watu milioni 1.2 wanaojihifadhi huko Rafah. Kuna hofu ya wazi kutoka kwa Wagaza ambao nilizungumza nao wakunga, madaktari, wanawake wajawazito, na wafanyakazi wenzangu, ambao wako Gaz. Hivi sasa ni kimbilio la Wagaza milioni 1.2, si mahali salama, lakini ni kimbilio angalau.”