Skip to main content

UN yasikitika Marekani kujitoa makubaliano kuhusu Iran

Mtambo wa nyuklia ulioko Busher nchini Iran.
IAEA/Paolo Contri
Mtambo wa nyuklia ulioko Busher nchini Iran.

UN yasikitika Marekani kujitoa makubaliano kuhusu Iran

Amani na Usalama

Guterres ataka shaka na shuku kwenye JCPOA iondolewe kwa kuzingatia mfumo uliowekwa na si kwa pande husika kujitoa kwenye makubaliano hayo yanayolenga kuwezesha Iran kuachana na nyuklia.

Nimesikitishwa sana na tangazo la Marekani kuwa itajiondoa kwenye mpango wa pamoja wa kudhibiti matumizi ya nyuklia kwa Iran, JCPOA na kuanza kuwekea nchi hiyo vikwazo.

Hiyo ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, aliyotoa leo kupitia msemaji wake baada ya tangazo la Rais wa Marekani Donald Trump.

Guterres amesema kila mara amekuwa akikariri  kuwa mpango huo ni mafanikio makubwa katika kudhibiti nyuklia na umechangia kwa kiasi kikubwa kuleta amani ya kikanda na ya  kimataifa.

JCPOA ni mpango unaojumuisha Iran pamoja na Marekani, China, Urusi, Ufaransa, Uingereza na Muungano wa Ulaya na unachagiza Iran isitishe mipango yake ya nyuklia.

Akimnukuu Katibu Mkuu, msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amewaambia waandishi wa habari mjini New York, Marekani kuwa..

(Sauti ya Stephane Dujarric)

“Ni muhimu shaka na shuku zote kuhusu utekelezaji wa mpango huo vishughulikiwe kupitia mfumo uliowekwa kwenye JCPOA. Hoja zisizohusiana moja kwa moja na JCPOA zinapaswa kushughulikiwa bila chuki ili kuhifadhi makubaliano hayo na mafanikio yake.”

Katibu Mkuu  ametoa wito kwa wanachama wa JCPOA pamoja na mataifa yote wanachama wa Umoja wa Mataifa waunge mkono makubaliano hayo.