Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya hatua kubwa zilizopigwa Dunia inakabiliwa na dharura ya miundombinu: UN

Wanaume wakipakua magunia ya vitunguu kutoka kwa lori huko Bamako, Mali, nchi inayoendelea isiyo na bandari. Ukosefu wao wa ufikiaji wa moja kwa moja kwa viungo muhimu vya biashara mara nyingi husababisha nchi zisizo na bandari kulipa gharama kubwa za us…
World Bank/Dominic Chavez
Wanaume wakipakua magunia ya vitunguu kutoka kwa lori huko Bamako, Mali, nchi inayoendelea isiyo na bandari. Ukosefu wao wa ufikiaji wa moja kwa moja kwa viungo muhimu vya biashara mara nyingi husababisha nchi zisizo na bandari kulipa gharama kubwa za usafiri na usafirishaji.

Licha ya hatua kubwa zilizopigwa Dunia inakabiliwa na dharura ya miundombinu: UN

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Wiki ya Uendelevu ya Umoja wa Mataifa unaendelea hapa Makao Makuu New York Marekani, leo mkutano ukijikita na mada ya miundombinu endelevu na inayoaminika ambayo Umoja wa Mataifa unasema itazisaidia nchi kuelekea kwenye maendeleo yenye miumbombinu bora, isiyo ya hatari na itakayoongeza kasi ya kufikia malengo ya maendeleo endelevu SDGs.

Ili kufikia hilo Umoja wa Mataifa umesisitiza kuwa uwekezaji utahitajika katika sekta za umma na binafsi hususan katika nchi zenye maendeleo duni, nchi zisizo na bahari na nchi zinazoendelea za visiwa vidogo ambazo zinakabiliwa na changamoto za kijiografia na rasilimali.

Watu milioni 700 hawana umeme duniani

Akizungumza katika mjadala wa kujenga mnepo wa kimataifa na kuchagiza maendeleo endelevu kupitia uunganishwaji wa miundombinu msaidizi wa Katibu Mkuu wa masuala ya kiuchumi na kijamii Li Junhua amesema “Licha ya hatua kubwa zilizopigwa bado dunia inakabiliwa na dharura ya miundombinu.”

Ameongeza kuwa "Zaidi ya watu bilioni 2 kote ulimwenguni wanakosa maji ya kunywa yaliyosimamiwa kwa usalama, na karibu nusu, hawana huduma zilizoboreshwa za usafi wa mazingira na takriban watu milioni 700 duniani kote hawana nishati ya umeme huku karibu theluthi moja ya watu duniani wanasalia nje ya mtandao wa intaneti.”

Hivyo amesema, "Tunaweza na lazima tugeuze dharura ya miundombinu kuwa fursa ya miundombinu. Ni lazima tuzibe pengo hilo kwa kuangalia uwekezaji wa siku zijazo katika miundombinu ambayo inatuweka karibu na malengo yetu ya uendelevu.”

Pengo la miundombinu linaongeza pengo la usawa

Dennis Francis, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa upande wake amesema "Mapengo ya kudumu ya miundombinu yanazidisha kukosekana kwa usawa duniani, kuathiri kusiko na uwiano nchi zilizo katika hali maalum, kama za visiwa vidogo zinazoendelea SIDS, chi za maendeleo duni LDCs na n anchi zisizo na bandari LLDCs ambazo ziko hatarini zaidi kutokana na vikwazo vya kijografia na uhaba wa rasilimali."

Rais wa Jamhuri ya Poland, Andrzej Duda, amesema, "Uwekezaji katika miundombinu ya hali ya juu, inayotegemewa, endelevu na yenye uthabiti ni kipaumbele cha kimataifa."

Mazungumzo hayo yasiyo rasmi yamelenga kuleta msukumo na kuongeza matarajio ya mapendekezo ya kuchangia katika kuimarisha uwekezaji kwenye miundombinu bora, inayotegemewa, endelevu na inayohimili hatari, ikiwa ni pamoja na kuchukua mtazamo wa kukabili hatari kwa maendeleo na usimamizi wa miundombinu.

Pia yamelenga kuunda jukwaa la kushiriki mbinu na mikakati bora ya kuimarisha ushirika na ushirikiano ndani na miongoni mwa kanda na changamoto za kikanda na kuhusisha njia za utekelezaji ikiwa ni pamoja na mbinu za ubunifu za kifedha na ushirikiano ili kusaidia uunganishwaji ulioboreshwa, uthabiti na ubora wa mifumo ya miundombinu.