Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kwa watu wa Ukraine, mwaka mpya ulianza kwa hasara, maumivu, na uchungu

Mji wa bandari wa Bahari Nyeusi wa Odesa kusini mwa Ukraine unalengwa na mashambulizi mapya ya makombora.
© UNOCHA/Alina Basiuk
Mji wa bandari wa Bahari Nyeusi wa Odesa kusini mwa Ukraine unalengwa na mashambulizi mapya ya makombora.

Kwa watu wa Ukraine, mwaka mpya ulianza kwa hasara, maumivu, na uchungu

Amani na Usalama

Mashambulizi makubwa ya angani yaliyosababisha vifo vingi na uharibifu wa makazi na miundombinu ya raia yameikumba nchi ya Ukraine katika siku za mwanzo za mwaka 2024 kutokana na mashambulizi mapya yaliyo tekelezwa na Urusi.

Hayo yapo kwenye taarifa iliyotolewa hii leo na Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Denise Brown ambaye amelaani vikali mashambulio hayo yaliyolenga zaidi miji. ” Kwa watu wa Ukraine, mwaka mpya ulianza kwa hasara, maumivu, na uchungu. Kwa siku ya tatu mfululizo, mashambulizi makubwa ya angani ya Urusi yamesababisha vifo - ikiwa ni pamoja na watoto kadhaa - na uharibifu wa nyumba”, Bi. Brown alisema.

Alisisitiza kuwa hali ni ya kutisha sana kwani maeneo mengi ya mji mkuu, Kyiv, yameachwa bila umeme au maji, jambo ambalo ni hatari sana kwani hali ya joto inatabiriwa kushuka hadi nyuzi joto -20 baadaye wiki hii.

Bibi Brown kwa mara nyingine tena ameikumbusha Urusi kwamba ‘mashambulizi ya kiholela dhidi ya raia na miundombinu ya kiraia yamepigwa marufuku kabisa chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu’.

 

Msaada kwa Ukraine

Mgogoro wa kibinadamu ni mkali vile vile katika Mkoa wa Donetsk, ambapo uhasama umewaacha mamia ya maelfu ya watu bila umeme, na hivyo kuzidisha hali mbaya ambayo tayari ilikuwepo.

Katika kukabiliana na uharibifu huu, Bi Brown alisisitiza hitaji la kuendelea kusaidia watu wa Ukraine.

“Leo, mawazo yangu yapo kwa familia na marafiki wa waliouawa au kujeruhiwa, na wale wanaohofia kupotea,” Bi. Brown pia a;osema na kusisitiza haja ya kuwasaidia wale “wanaoteseka na uharibifu uliosababishwa na uvamizi wa Urusi.”

Katika ujumbe wao kupitia mtandano wa x (Twitter), Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limechapisha kuwa watoto wengi katika mji mkuu walilazimika kulala usiku kucha katika vituo vya treni vya jiji hilo.

 

Mji wa Kirusi ulipigwa

Wakati wa mkutano wa mwisho wa Baraza la Usalama kwa mwaka 2023 - ulioitishwa kwa ombi la Urusi - afisa mkuu wa masuala ya kisiasa wa Umoja wa Mataifa alilaani mashambulizi dhidi ya mji wa Urusi wa Belgorod, ulio karibu na mpaka wa Ukraine.

Takriban raia 18 waliuawa na zaidi ya 100 kujeruhiwa, alisema Khaled Khiari, Msaidizi wa Katibu Mkuu katika Idara ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Siasa na Kujenga Amani.