Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hakuna sekta inafikia utalii katika kukwamua jamii – UN

Lemurs ni kivutio kikuu cha utalii nchini Madagaska.
UN News/Daniel Dickinson
Lemurs ni kivutio kikuu cha utalii nchini Madagaska.

Hakuna sekta inafikia utalii katika kukwamua jamii – UN

Ukuaji wa Kiuchumi

Wiki ya uendelevu kwenye Umoja wa Mataifa imeingia siku ya pili hii leo ambapo mawaziri kutoka nchi mbali mbali wanachama wa Umoja wa Mataifa wamejinasibu ni kwa vipi sekta hiyo inaweza kuchochea mafanikio ya malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Balozi Dennis Francis ambaye ndiye mwenyeji wa wiki hii, amewaeleza wajumbe kuwa  utalii ni moja ya sekta zinazoongoza katika kufanikisha uchumi wa dunia kwani mwaka 2023 ilichangia asilimia 3 ya pato la ndani la kimataifa, huku ikiajiri mtu 1 katika kila watu 10 duniani. 

Utalii ni sekta thabiti ya kumwezesha mwanamke

“Wanawake wakiwa wanashikilia asilimia 54 ya ajira hizo ikilinganishwa na asilimia 39 kwenye sekta nyingine za kiuchumi, utalii ni chombo thabiti na bora kwa ajili ya uwezeshaji wanawake,” amesema Balozi Francis. 

Hata hivyo amemulika hatari ambazo sekta hiyo inaweza kukumbwa nazo ikiwemo madhara ya mabadiliko ya tabianchi, milipuko ya magonjwa, na ukosefu wa utulivu wa kisiasa na ndipo akasisitiza umuhimu wa kuweka mifumo ya mnepo ili kuhimili na kukabili changamoto hizo zinapotokea, sambamba na kulinda mifumo ya asili ya bayonuai na jamii. 

Kwa ujumla, Balozi Francis amesihi washiriki wasake mbinu za kuona ni kwa jinsi gani utalii unaweza kuchangia kwa ufanisi kwenye kusongesha SDGs, ikiwemo kutokomeza umaskini na kuhakikisha ujumuishi. 

Visiwa vya Perhentian huko Terengganu, Malaysia.
© Unsplash/Hongbin
Visiwa vya Perhentian huko Terengganu, Malaysia.

Utalii ni nuru ya matumaini kwenye kiza

Hotuba ya Katibu Mkuu Antonio Guterres ilisomwa kwa niaba  yake na Katibu Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii duniani, UNWTO, Zurab Pololikashvili. 

Guterres amesema madhara ya mizozo yanafika hata nje ya ukanda wa vita, lakini hata kwenye kiza, tunahitaji kusaka nuru ya matumaini.

Amesema utalii unatupatia matumaini hayo. “Mwaka 2023, licha ya changamoto zote, tuliona jinsi gani sekta hii ilikwamuka kwa kiasi kikubwa. Kukwamuka huko lazima kuwe kichocheo kwa hatua za kijasiri na mabadiliko dhahiri.”

Amemnukuu Katibu Mkuu wa UNWTO ya kwamba “mwaka huu lazima turejelee azma yetu ya kutekeleza lengo letu. Rasimu ya makubaliano ya mustakabali ni fursa ya kurejea kwenye njia sahihi. Ni mwanzo wa kuelea kupitishwa kwa makubaliano kabla ya Mkutano wa zama zijazo mwezi Septemba mwaka huu.”

Guterres amesisitiza kuwa utalii unaweza na ni lazima uwe sehemu ya mpango wa mustakabali bora kwa wote.

Idadi ya watalii wa kimataifa imeongezeka

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa anasema sekta ya utalii ina tofauti kubwa kati ya mwaka 2022 na sasa. “Sekta yetu ilikwamuka kutoka janga kubwa la kihistoria la coronavirus">COVID-19. Mwaka jana watalii wa kimataifa walifikia takribani asilimia 90 kabla ya janga la coronavirus">COVID-19. Tunatarajia kukwamuka kikamilifu ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.”

Waziri wa Utalii na sekta ya Ukarimu nchini Zimbabwe, Barbara Rwodzi akihutubia mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu utalii.
UN Video

Zimbabwe: Utalii unazingatia uhifadhi na uendelevu 

Akihutubia mkutano huo, Waziri wa Utalii na sekta ya Ukarimu nchini Zimbabwe, Barbara Rwodzi amesema utalii unachangia asilimia 5.7 ya pato la ndani la taifa, GDP na ndio  maana inapatiwa kipaumbele kwa kuhakikisha maeneo ya utalii yanafikika, yana malazi bora na yana miradi ya kuboresha huduma kwa watalii.

“Sisi kama nchi tunapatia kipaumbele kwenye vipengele hivyo vitatu ili kuweka mazingira ya watalii kupenda kutembelea, na azma yetu hiyo ni kwenye msingi kwamba  kila dola inayotumika inachangia uendelevu wa sekta ya utalii na ukarimu.” amesema Waziri Rwodzi akisema wakati wote wa kufanya hivyo wanazingatia uhifadhi.

Kipato kitokanacho na utalii pia kimefikia dola trilioni 1.6 za kimarekani mwaka jana. Hii ni sawa na takribani asilimia 95 ya dola trilioni 1.7 za mwaka 2019.

Kwa nchi ndogo za visiwa, utalii unachangia zaidi ya asilimia 20 ya pato la ndani la taifa, GDP. Na ndio maana Katibu Mkuu amesema hakuna sekta inayokaribia hii ya utalii katika uwezeshaji wa wananchi. Na utalii unazidi kukua kama msingi wa fursa kwa vijana na wanawake.

Hata hivyo amesisitiza umuhimu wa mnepo kwenye sekta hiyo kwa kuweka mipango awali badala ya kusubiri janga ndipo kuchukua  hatua.