Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN na wadau wazindua ombi la dola bilioni 2.8 kwa ajili ya Gaza na Ukingo wa Magharibi

Gari lililosheheni mali na vifaa vya nyumbani linapita kwenye mitaa ya Khan Younis.
© UNOCHA/Themba Linden
Gari lililosheheni mali na vifaa vya nyumbani linapita kwenye mitaa ya Khan Younis.

UN na wadau wazindua ombi la dola bilioni 2.8 kwa ajili ya Gaza na Ukingo wa Magharibi

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa na mashirika wadau leo wamesisitiza kwamba "mabadiliko muhimu yanahitajika ili kuboresha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu huko Gaza, wakati walizindua ombi la dola bilioni 2.8 kutoa msaada wa dharura kwa watu zaidi ya milioni 3 katika eneo hilo lililoharibiwa, lakini pia katika Ukingo wa Magharibi, ambapo Wapalestina wamekuwa wakilengwa na kuongezeka kwa vurugu za walowezi wa Kiyahudi”.

Haya yanajiri huku kukiwa na ripoti za mashambulizi ya Israel yanayoendelea katika Ukanda wa Gaza ikiwa ni pamoja na katika mji wa Gaza kaskazini, Rafah kusini mwa Gaza na Gaza ya kati, ambapo zaidi ya watu 10 wanaaminika kufariki Dunia katika shambulio la kombora lililotokea kwenye kambi ya wakimbizi jana Jumanne.

Picha za video zinazoripotiwa kutoka hospitali ya Al-Aqsa huko Deir Al-Balah zilionyesha waathirika waliojeruhiwa na waliokufa wakiwemo watoto baada ya shambulio kwenye kambi ya wakimbizi ya Maghazi katikati mwa eneo hilo.

Hatari ya njaa

Ombi hilo lililotolewa leo linalenga kushushughulikia msaada wa kibinadamu kwa  watu milioni 3.1 kati ya sasa na mwisho wa mwaka huu wa 2024.

Linatazamia kusaidia watu milioni 2.3 katika Ukanda wa Gaza ambapo wataalam wa kutokuwa na uhakika wa chakula wameonya kwamba njaa inakaribia kaskazini baada ya zaidi ya miezi sita ya mashambulizi makali ya Israel na mashambulizi ya ardhini, yaliyoanzishwa kujibu mashambulizi ya Hamas yaliyofanywa kusini mwa Israeli Oktoba 7 mwaka jana. 

Mjini Gaza watoto wakisubiri kupokea chakula wakati mashambulizi ya Israel yakiendelea
© UNDP PAPP/Abed Zagout
Mjini Gaza watoto wakisubiri kupokea chakula wakati mashambulizi ya Israel yakiendelea

Watoto wageuka wachuuzi mitaani

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA, “Njaa imekaribia katika majimbo ya kaskazini na inakadiriwa kutokea wakati wowote kati ya sasa na Mei 2024 wakati zaidi ya nusu ya wakazi wa Gaza wanakabiliwa na viwango vya janga la njaa.” 

Shirika hilo limeongeza kuwa masoko yanakosa bidhaa za msingi za chakula na hutegemea wasambazaji wasio rasmi wanaotoa mgao wa misaada.

"Mwenendo wa kutoa hofu uliobainika ni kuongezeka kwa uuzaji wa misaada ya kibinadamu katika masoko, hasa wachuuzi wasio rasmi wa mitaani, ambao wengi wao ni watoto wadogo."limesema shirika hilo

Ikiongoza ombi hilo, OCHA imebainisha kuwa ombi hilo la ufadhili linashughulikia mahitaji ya shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, ambalo linaendelea kuwa mhimili wa hatua za msaada wa kibinadamu huko Gaza na Ukingo wa Magharibi.

Jukumu muhimu la UNRWA

"Theluthi mbili ya wakazi wa Gaza ambao ni sawa na watu milioni 1.6 ni wakimbizi wa Kipalestina waliosajiliwa na UNRWA," OCHA imesema, na kuongeza kuwa karibu milioni moja kati ya watu milioni 1.7 waliokimbia makazi yao sasa wanapata hifadhi katika makazi UNRWA 450 na makazi ya umma, au karibu na Umoja wa Mataifa limeongeza Shirika hilo la Umoja wa Mataifa.

Pia OCHA imesema kuwa UNRWA ina wafanyakazi zaidi ya 13,000 huko Gaza, huku zaidi ya 3,500 wakishiriki katika operesheni ya misaada. 

"Wakati wa dharura, msaada wa UNRWA unaongezwa kwa idadi kubwa ya watu," limesema shirika hilo likiongeza kuwa shirika hilo la Umoja wa Mataifa la UNRWA pia linahudumia wakimbizi wa Kipalestina milioni 1.1 na watu wengine waliosajiliwa katika Ukingo wa Magharibi, ambapoo 890,000 ni wakimbizi.

Wapalestina wakiwa kwenye foleni ya kutafuta maji huko Gaza.
© WHO/Ahmed Zakot
Wapalestina wakiwa kwenye foleni ya kutafuta maji huko Gaza.

Changamoto ya maji

Ukosefu wa maji safi unaendelea kuwa tatizo kubwa la kibinadamu, limebainisha shirika la OCHA, huku bomba moja tu kati ya matatu ya maji linalotoka Israel ndilo bado linafanya kazi kwa asilimia 47 pekee.

Pia kuna visima chini ya 20 vya maji ya chini ya ardhi ambavyo hufanya kazi tu "wakati mafuta yanapatikana na hakuna mifumo kamili ya kusafisha maji machafu.”

OCHA, imeongeza kuwa kufurika kwa maji taka kumetokea "katika maeneo mengi na kuongeza hatari ya afya ya umma kote Gaza".

Hofu juu ya Rafah 

Ikinukuu tathmini ya hivi karibuni ya huduma za usafi wa mazingira na kujisafi yaani WASH iliyoongozwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, OCHA imesema imegundua kuwa ndani ya maeneo 75 yaliyotathminiwa huko Rafah yanayojumuisha idadi ya takriban watu 750,000 thuluthi moja ilikuwa na vyanzo vya maji ambavyo havikuwa salama kwa kunywa.

Hii ilijumuisha asilimia 68 ya vituo vya pamoja vya UNRWA, na wastani wa upatikanaji wa maji ulikuwa ni lita tatu tu kwa kila mtu kwa siku.

Kufuatia kuondoka kwa vikosi vya Israel kutoka kusini mwa Gaza mapema mwezi huu, wasaidizi wa kibinadamu wameelezea wasiwasi wao mara kwa mara kuhusu operesheni ya kijeshi dhidi ya tawi la kijeshi la Hamas inayofanywa na Vikosi vya ulinzi vya Israel katika mji wa Rafah unaopakana na Misri na ambako zaidi ya watu milioni moja wanahifadhiwa kwa sasa.

Mahitaji yanasalia kuwa mabaya zaidi kaskazini mwa Gaza huku kukiwa na vikwazo vinavyoendelea vya misaada ikiwa ni pamoja na malaka ya Israel kukataa kutoa ruhusa ya kuingia kwa operesheni za kibinadamu.

Wagonjwa wakipatiwa huduma katika hospitali ya Al-Shifa Gaza (Kutoka Maktaba)
© UNRWA
Wagonjwa wakipatiwa huduma katika hospitali ya Al-Shifa Gaza (Kutoka Maktaba)

Wasiwasi wa mkuu wa WHO Dkt. Tedros 

Katika chapisho lake kwenye mtandao wa kijamii wa X hii leo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus ameangazia jinsi ujumbe wa shirika hilo Jumatatu kwenye mji wa Gaza akisema "ulicheleweshwa sana, na kuacha muda mchache wa kutathmini uharibifu na mahitaji katika Hospitali iliyoharibiwa ya Al-Shifa na Hospitali ya Indonesia.”

Dkt. Tedross ameongeza kuwa "Uondoaji wa maiti katika hospital ya Al-Shifa bado unaendelea. Idara ya dharura inasafishwa na wahudumu wa afya na vitanda vilivyoungua vimeondolewa. Usalama wa majengo yaliyobaki bado unahitaji tathmini ya kina ya uhandisi.”

Hospitali ya Indonesia sasa haina mtu lakini juhudi zinaendelea kuifungua tena, amesema Tedros.

Kituo cha matibabu cha Jumuiya y amsaada wa kitabibu cha Palestina kinapokea wagonjwa waliopatwa na kiwewe lakini bado "kina uhitaji mkubwa wa mafuta na vifaa vya matibabu", ambayo mkuu huyo wa WHO aliahidi kuwasilisha.

“Kiwango cha uharibifu wa hospitali za Gaza kinasikitisha. Tunatoa wito tena kwa hospitali kulindwa, sio kushambuliwa au kutumiwa kijeshi.

Takwimu za hivi punde kutoka kwa mamlaka ya afya ya eneo hilo zinaonyesha kuwa Wapalestina 33,800 wameuawa na zaidi ya 76,500 wamejeruhiwa huko Gaza tangu Oktoba 7 mwka jana. 

Idadi ya vifo nchini Israel kutokana na mashambulizi ya Hamas ya Oktoba 7 imefikia 1,139 na makumi ya watu bado wanazuiliwa mateka huko Gaza.

Wanajeshi 259 wa Israel wameuawa katika operesheni za ardhini katika eneo hilo huku zaidi ya 1,570 wakijeruhiwa, kulingana na ofisi ya OCHA.

Hatua za kibinadamu

Ombi hilo la leo Jumatano litachukua nafasi ya ombi la awali la pesa lililotolewa Oktoba 2023 ambalo lilisahihishwa mwezi Novemba na kuongezwa hadi Machi 2024.

Kiasi cha dola bilioni 2.8 kinawakilisha sehemu tu ya karibu dola bilioni 4.1 ambazo Umoja wa Mataifa na washirika wanakadiria zinahitajika ili kukidhi mahitaji ya walio hatarini zaidi lakini inaonyesha kile ambacho timu za misaada zinaamini kinaweza kutekelezeka katika kipindi cha miezi tisa ijayo.

Baadaye mchana wa le Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kujadili hali inayoendelea kuzorota kwa kasi Mashariki ya Kati, na kutafanyika mkutano na waandishi wa habari wa Kamishna Mkuu wa UNRWA Philippe Lazzarini.