Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukiukwaji wa haki ya afya ya uzazi kwa wanawake wachangia vifo vinavyoweza kuzuilika: UNFPA

Amani huko Upper Nile nchini SUdan Kusini itasaidia wazazi kama aonekanavyo pichani kuweza kupata huduma bora kwake yeye na mtoto. Pichani ni kituo kinachosaidiwa na UNICEF mjini Malakal
UNICEF
Amani huko Upper Nile nchini SUdan Kusini itasaidia wazazi kama aonekanavyo pichani kuweza kupata huduma bora kwake yeye na mtoto. Pichani ni kituo kinachosaidiwa na UNICEF mjini Malakal

Ukiukwaji wa haki ya afya ya uzazi kwa wanawake wachangia vifo vinavyoweza kuzuilika: UNFPA

Wanawake

Wanawake wa Kiafrika wana uwezekano wa kufa mara 130 zaidi kutokana na ujauzito au matatizo ya uzazi kuliko wanawake wa Ulaya na Amerika Kaskazini, kwa mujibu wa ripoti mpya iliyochapishwa leo na Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ya uzazi UNFPA.

Ripoti hiyo “Maisha Yaliyounganishwa, Mizizi ya Matumaini: Kukomesha kukosekana kwa usawa katika afya na haki za ngono na uzazi”, inaonyesha kuwa zaidi ya nusu ya vifo vya uzazi vinavyoweza kuzuilika hutokea katika nchi ambazo ziko katika hali ya shida au changamoto.

Pia inaangazia jukumu ambalo ubaguzi wa rangi, ubaguzi wa kijinsia na aina nyingine za ubaguzi huchukua katika kuzuia maendeleo kwenye masuala ya ngono na afya ya uzazi.

Kulingana na matokeo ya utafiti wa ripoti hiyo “Wanawake na wasichana waliokwama katika umaskini wana uwezekano mkubwa wa kufa mapema kutokana na ukosefu wa huduma za afya za kutosha kama wanatoka katika makundi ya wachache au wamekwama katika mazingira ya migogoro.”

Kwa ujumla, ripoti inasema kumekuwa na maendeleo makubwa katika afya ya ngono na uzazi ikawa kipaumbele cha maendeleo endelevu miongo mitatu iliyopita.

Akizindua ripoti hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Natalia Kanem amesema "Katika nafasi ya kizazi kimoja, tumepunguza kiwango cha mimba zisizotarajiwa kwa karibu theluthi moja, kupunguza kiwango cha vifo vya uzazi kwa theluthi moja, na kupata sheria dhidi ya unyanyasaji wa majumbani katika zaidi ya nchi 160."

Mchakato uliokwama

Bi. Kanem ameongeza kuwa lakini maendeleo yanapungua au kukwama katika maeneo kadhaa muhimu. 

“Katika ulimwengu ambapo robo ya wanawake hawawezi kukataa kufanya ngono na wapenzi wao na karibu mmoja kati ya 10 hawana sauti kuhusu uzazi wa mpango, wanawake 800 wanakufa kila siku wakijifungua idadi ya kutatanisha ambayo haijabadilika tangu 2016.”

Ameendelea kusema kuwa takriban vifo 500 kati ya hivyo vinavyoweza kuzuilika vinatokea kwa siku katika nchi zinazoishi zikipitia majanga ya kibinadamu na migogoro.

"Ulimwengu haujapiga hatua katika kuokoa wanawake kutokana na vifo vinavyoweza kuzuilika wakati wa ujauzito na kujifungua," amesema Bi. Kanem, akiongeza kuwa kwa mara ya kwanza, takwimu zimekusanywa kuhusu endapo uhuru wa mwili wa wanawake unaimarika kwa wakati.

Amesema “Katika asilimia 40 ya nchi ambako taarifa zimepatikana, uhuru unadhoofika kutokana na kushindwa kuwafikia walio nyuma zaidi".

Ripoti imebainisha kuwa kuna tofauti ya wazi kati ya mataifa ya Kaskazini na Kusini, Magharibi na Mashariki, linapokuja suala la uzazi wa mpango, huduma za uzazi salama, utunzaji wa heshima ya uzazi, na huduma zingine muhimu.

Ajnur Demir akiwa katika picha ya pamoja na familia yake wakati akihudhuria warsha ya ukosefu wa uraia iliyoungwa mkono na UNHCR huko Skopje, Macedonia Kaskazini. (Maktaba)
© UNHCR/Roger Arnold
Ajnur Demir akiwa katika picha ya pamoja na familia yake wakati akihudhuria warsha ya ukosefu wa uraia iliyoungwa mkono na UNHCR huko Skopje, Macedonia Kaskazini. (Maktaba)

Suala la usawa

Hata hivyo, hata ndani ya mataifa hayo kuna "mapengo ya ukosefu wa usawa", ripoti inasisitiza. 

Wanawake wenye asili ya Kiafrika katika bara la Amerika wanakabiliwa na viwango vya juu vya vifo vya uzazi ikilinganishwa na wanawake weupe, jambo ambalo linadhihirika hasa nchini Marekani ambako ni mara tatu ya wastani wa kitaifa.

Watu wa jamii za asili na makabila madogo pia wanakabiliwa na hatari kubwa zinazohusiana na ujauzito na kujukifungua.

Ndani ya bara Ulaya, nchini Albania, kwa mfano, ripoti inasema zaidi ya asilimia 90 ya wanawake wa Kiromania kutoka makundi yaliyotengwa zaidi kiuchumi na kijamii walikuwa na matatizo makubwa katika kupata huduma za afya ikilinganishwa na asilimia 5 tu ya wanawake wa kabila la Kialbania kutoka tabaka zilizobahatika zaidi.

Zaidi ya hayo, wanawake wenye ulemavu wana uwezekano wa kufikia mara 10 zaidi wa kukabiliwa na unyanyasaji wa kijinsia, na watu wenye mwelekeo tofauti wa kijinsia na kujieleza kijinsia hukumbana na ukatili mkubwa na vikwazo vya kupata huduma.

Mwanamke akiwa na mtoto wake mchanga akiwasikiliza wafanyakazi wa UNFPA katika kikao cha kuongeza uelewa kuhusu ukatili wa kijinsia katika Kituo cha One Stop katika Hospitali ya Sominé Dolo.
© UNFPA Mali/Amadou Maiga
Mwanamke akiwa na mtoto wake mchanga akiwasikiliza wafanyakazi wa UNFPA katika kikao cha kuongeza uelewa kuhusu ukatili wa kijinsia katika Kituo cha One Stop katika Hospitali ya Sominé Dolo.

Hakuna suluhu moja inayokidhi haja zote 

Ripoti pia inaangazia umuhimu wa kuandaa programu kulingana na mahitaji ya jamii na kuwawezesha wanawake na wasichana kuunda na kutekeleza suluhu za kibunifu.

Pia inakokotoa kwamba ikiwa dola bilioni 79 za ziada zitawekezwa katika nchi za kipato cha chini na cha kati ifikapo mwaka 2030, mimba zisizopangwa milioni 400 zinaweza kuepukwa, maisha milioni moja yataokolewa na dola bilioni 660 katika faida za kiuchumi zinaweza kuzalishwa.

Uwezo wa kupata haki za afya ya uzazi, Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Bi. Kanem anaamini, ni changamoto nyingine kubwa akisema "Kwa hakika ni wajibu wa wanaume kuwa mabingwa wa haki za uzazi za wanawake, wa haki za uzazi za kila mtu."