Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dunia inawaangusha kwa mengi watoto wa kike: Guterres

Kuwapa wasichana fursa kuongoza kwa kuwafanya kitovu cha mabadiliko ni njia mojawapo ya kuwekeza katika kuamini uwezo wa wasichana
© UNFPA Burkina Faso/Théo
Kuwapa wasichana fursa kuongoza kwa kuwafanya kitovu cha mabadiliko ni njia mojawapo ya kuwekeza katika kuamini uwezo wa wasichana

Dunia inawaangusha kwa mengi watoto wa kike: Guterres

Wanawake

Muda wa utekelezaji wa ajeda ya Umoja wa Mataifa ya maendeleo ya 2030 ukiwa umefika katikati Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema dunia inawaangusha kwa mengi watoto wa kike.

Kupitia ujumbe wake wa siku ya kimataifa yam toto wa kike inayoadhimishwa leo Oktoba 11 Antonio Guterres amesema “Kwa mwelekeo wa sasa, mwisho wa ndoa za utotoni umesaliza miaka 300. Ikiwa hakuna kitakachobadilika, kufikia 2030, wanawake na wasichana milioni 110 ambao wanapaswa kuwa katika madarasa, hawatakuwa madarasani. Na wanawake na wasichana milioni 340 bado watavumilia magumu ya umaskini uliokithiri.”

Ameongeza kuwa na aina za zamani za ubaguzi dhidi ya wasichana zinaendelea na katika baadhi ya kesi zinazidi kuwa mbaya. 

Mathalani amesema wasichana nchini Afghanistan hawawezi kutumia haki zao za msingi na uhuru, wakiwa wamezuiliwa majumbani mwao bila matumaini ya elimu au uhuru wa kiuchumi.

Kuibuka kwa mifumo mipya ya pengo la usawa

Guterres amesema aina mpya za upendeleo na ukosefu wa usawa zinaibuka. Mgawanyiko wa kidijitali unamaanisha kuwa wasichana wengi hawajumuishwi kwenye ulimwengu wa mtandao. 

Algorithms kulingana na uzoefu wa wanaume na wavulana ni mfumo wa kidijitali unao kukuza ubaguzi wa kijinsia.

Hata hivyo duniani kote, wasichana wanapambana kukabiliana na ubaguzi wa kijinsia, kupinga ubaguzi na kuleta mabadiliko, kwenye viwanja vya soka, shuleni, na katika uwanja wa umma, hivyo ni lazima tusimame nao. Amesisitiza Katibu Mkuu.

Pendekezo langu la Kichocheo cha  malengo ya maendeleo endelevu SDG ili kurejesha malengo kwenye mstari linazidi kupata nguvu. Na lazima tuwekeze katika uongozi wa wasichana .

kaulimbiu ya siku ya kimataifa ya Mtoto wa Kike mwaka huu ni kusaidia wasichana kufikia malengo yao na kuimarisha usawa wa kijinsia. 

Kwani amesema Wanawake na wasichana wanapoongoza wanaweza kubadilisha mitazamo, kuunda mabadiliko, na kuendeleza sera na masuluhisho ambayo yanashughulikia mahitaji yao.

Amehitimisha ujumbe wake kwa kusema kuwa Wanawake na wasichana wanaweza kutuongoza kwenye mustakabali mzuri zaidi. Katika siku hii ya kimataifa ya Mtoto wa Kike, hebu tuimarishe sauti za wasichana, na tujitoe tena kufanya kazi pamoja ili kujenga ulimwengu ambapo kila msichana anaweza kuongoza na kustawi.