Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wiki ya Uendelevu ya UN yaanza kwa kujadili mzigo wa madeni

Katibu Mkuu António Guterres akihutubia mjadala wa Jukwa la ngazi ya juu kuhusu uendelevu na usawa wa kijamii na kiuchumi kwa wote.
UN Photo/Rick Bajornas
Katibu Mkuu António Guterres akihutubia mjadala wa Jukwa la ngazi ya juu kuhusu uendelevu na usawa wa kijamii na kiuchumi kwa wote.

Wiki ya Uendelevu ya UN yaanza kwa kujadili mzigo wa madeni

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Jumatatu wameongoza wito wa haraka wa kufanyia mabadiliko mfumo wa kimataifa wa kifedha, hususani jinsi gani ya kukabiliana na upunguzaji wa madeni kwa niaba ya mabilioni ya raia wanaoishi katika nchi zinazoendelea.

Dennis Francis, Rais wa kikao cha 78 cha Baraza Kuu amesisitiza kuhusu pengo linalopanuka la kutokuwepo usawa baina ya nchi tajiri na masikini.

Amesema “Mgogoro wa madeni kwa hakika ni mgogoro unaoendelea na unaoziathiri zaidi nchi za Kusini mwa Ulimwengu.”

Ameongeza kuwa “Madeni ya umma yameongezeka haraka katika nchi zinazoendelea kuliko katika nchi zilizoendelea huku mzigo wa madeni ya nje kwa nchi zinazoendelea ukifikia dola trilioni 11.4”

Rais huyo wa Baraza Kuu amesisitiza kwamba “Hatimaye kufikia usawa endelevu katika suala la madeni na usawa wa kuchumi na kijamii kunahitaji uratibu mzuri, juhudi za kimataifa za kubadili na kurekebisha mfumo wa kimataifa wa kifedha hususan taasisi za kimataifa za kifedha ili ziweze kusaidia ipasavyo na kuwezesha maendeleo endelevu katika eneo la Kusini mwa ulimwengu.”

Umuhimu wa msaada wa kujikwamua na madeni

Katibu Mkuu António Guterres kwa upande wake amesisitiza haja ya kuwepo nyenzo ya msaada maalum ili nchi zinazoendelea ziweze kujikwamua kutoka Kwenye dimbwi la madeni.

Guterres amesema “Kwa nchi zinazoendelea Ulimwengu wa madeni unamaanisha ni Ulimwengu wa maumivu. Wanahaha kupanda ngazi ya maendeleo huku mkono wao mmoja ukiwa umefungwa nyuma yao.”

Katibu Mkuu ameainisha kwamba “Uchumi wa dunia unasuasua katika kiwango cha chini cha mapato ya mwaka katika kipindi cha miaka mitano ya mdororo tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990 na wakati wa janga la coronavirus">COVID-19 na vita ya Ukraine vimezidisha kudumaza ukuaji wa uchumi na kuathiri hali ya kifedha.”

Ameongeza kuwa kabla ya nchi zinazoendelea kupata afuweni mgogoro wa dunia wa kujikimu kimaisha athari za janga la COVID-19 viko dhahiri.”

Guterres amesema taasisi za Bretton Woods “Ziliundwa na nchi Tajiri na zinaendelewa kudhibitiwa na nchi hizo” na amesisitiza kwamba leo hii nchi nyingi zinazoendelea zimekwama katika mfumo wa Bretton Woods bila kuwa na ramani ya kuwaongoza.”

Mapendekezo ya fungu la SDGs yanapaswa kuanza kutekelezwa

Katibu Mkuu ajmeziambia nchi wanachama kwamba mapendekezo ya fungu la msaada wa SDG’s aliyoyatoa mwezi Februari mwaka jana lazima yaanze kuhuishwa sasa.

Fungu hilo la msaada linadhamiria kukusanya dola bilioni 500 kila mwaka za ufadhili wa ziada kutoka kwenye mataifa tajiri ili kufikia ajenda ya mwaka 2030 ya malengo ya maendeleo endelevu.