Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Saudi Arabia yasaidia Sudan na Sudan Kusini kupambana na utapiamlo

Mtoto mwenye umri wa mwaka 1 anafanyiwa unchunguzi wa matibabu kama kuna dalili za utapiamlo katika kituo cha mapokezi kwenye mpaka wa Sudan na Sudan Kusini.
© WFP/Hugh Rutherford
Mtoto mwenye umri wa mwaka 1 anafanyiwa unchunguzi wa matibabu kama kuna dalili za utapiamlo katika kituo cha mapokezi kwenye mpaka wa Sudan na Sudan Kusini.

Saudi Arabia yasaidia Sudan na Sudan Kusini kupambana na utapiamlo

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP leo limetia saini mikataba miwili na Saudi Arabia yenye thamani ya dola milioni 1.4 ili kutibu na kuzuia utapiamlo nchini Sudan na Sudan Kusini.

Taarifa ya WFP kutoka Nairobi Kenya na Riyadh Saudi Arabia inaeleaza kuwa fedha hizo zitasaidia zaidi ya watoto 35,000 na wajawazito pamoja na wamama wanaonyonyesha walioathirwa na vita, mtikisiko wa kiuchumu na mabadiliko ya tabianchi. 

Idadi hiyo inajumuisha wasudan 29,000 ambao wameathirika na vita vinavyoendelea pamoja na wa Sudan Kusini 6,000 ambao wameathirika na mgogoro wa misaada ya kibinadamu uliosababishwa na machafuko, kiuchumi na mabadiliko ya tabianchi. 

“Fedha hizi zinakuja katika wakati mahususi, ni takriban mwaka mmoja sasa tangu kuanza kwa vita tangu hapo vimeendelea kuongezekza mpaka kuwa moja ya majanga kabaya ya kidunia” amesema Michael Dunford Mwakilishi wa WFP ukanda wa Afrika Mashariki. 

Mwakilishi huyo amesema tayari wameanza kupokea ripoti za watoto kufa njaa huko nchini Sudan hivyo programu za usaidizi wa lishe ni muhimu zaidi katika kuzuia vido na kuleta mustakabali bora wa baadae wa watoto.

Kwa upande wake Dkt.Abdullah Al Moallem ambaye ni mkurugenzi wa Idara ya Afya ya Mazingira ya Ksrelief ya Saudi Arabia ameeleza kuwa wamejitolea kusaidia kundi hilo ambalo lipo kwenye mazingira magumu ili kukuza mustakabali wenye afya na uthabiti zaidi kwa jamii nzima.

“Mipango hii itawawezesha wale wanaohitaji kupata msaada muhimu wa chakula na matibabu na itatusaidia kupambana na njaa na utapiamlo katika nchi zote mbili,” alisema Dk. Al Moallem.

Nchini Sudan, watoto milioni 4.9 wenye umri wa chini ya miaka mitano na wanawake wajawazito au wale wanaonyonyesha wana utapiamlo, hili likiwa ni ongezeko la asilimia 22 kutoka mwaka uliopita. 

Kati ya hao, watoto 730,000 wanakabiliwa na utapiamlo mkali. 

Nchini Sudan Kusini, watoto milioni 1.6 na wanawake 870,000 wajawazito na wanaonyonyesha wanatarajiwa kukosa lishe bora mwaka huu.