Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pande zinazopigana nchini Sudan zatakiwa kusitisha mapigano

Watoto na familia wakikimbia kwa miguu kutoka Wad Madani, jimbo la Al Jazirah kufuatia mapigano ya hivi karibuni.
© UNICEF/UNI492302/Mohamdeen
Watoto na familia wakikimbia kwa miguu kutoka Wad Madani, jimbo la Al Jazirah kufuatia mapigano ya hivi karibuni.

Pande zinazopigana nchini Sudan zatakiwa kusitisha mapigano

Haki za binadamu

Ujumbe wa Kutafuta Ukweli wa Umoja wa Mataifa kuhusu Sudan umesema pande zinazo zozana nchini humo lazima zijitolee kusitisha mapigano na kukomesha mashambulizi dhidi ya raia ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuna upatikanaji wa misaada ya kibinadamu bila vikwazo kwa mamilioni ya watu wenye uhitaji wa misaada ya dharura

Taarifa ya ujumbe huo imetolewa leo jijini Geneva Uswisi na ofisi ya umoja wa mataifa ya haki za binadamu wakati huu ambapo mgogoro huo ukikaribia kuingia mwaka wake wa pili tangu kuanza kwa mapigano kati ya Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka ambavyo vimesababisha mauaji ya maelfu ya raia tangu yalipoanza tarehe 15 Aprili 2023. 

Vita vikomeshwe

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Umoja wa Mataifa zaidi ya watu milioni sita wamelazimika kuyakimbia makazi yao ndani ya nchi huku takriban wakimbizi milioni mbili wakikimbilia nchi jirani. Takriban watu milioni 24 wanahitaji msaada, huku milioni 18 wakiteseka kwa viwango vya uhaba wa chakula.

“Ni zaidi ya wakati kwa vita hivi vikali kukomesha,” alisema Mohamed Chande Othman, mwenyekiti wa Ujumbe Huru wa Kimataifa wa Kutafuta Ukweli kwa nchi ya Sudan. “Pande zinazopigana lazima zikomeshe mara moja unyanyasaji wote, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kingono na kijinsia, na kuwawajibisha wahusika wa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu kwa matendo yao.”

“Vikundi vinavyo pigana Sudan vina wajibu wa kisheria kulinda raia, lakini vimeonesha kujali kidogo kufanya hivyo," Othman alisema. "Sasa tunachunguza ripoti za kutisha za mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya raia na miundombinu ya kiraia, ikiwa ni pamoja na hospitali na shule.”

Mashambulizi dhidi ya misaada ya kibinadamu yaripotiwa

Ujumbe huo wa Kutafuta Ukweli ulisema mashambulizi dhidi ya misafara ya misaada na miundombinu yameripotiwa katika kile kinachoonekana kuwa ni ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa za kibinadamu.

“Mashirika ya misaada yanavumilia ingawa kumekuwa na mashambulizi na uporaji wa misafara ya kibinadamu, wafanyakazi na maghala,” alisema Mona Rishmawi, mjumbe mtaalam wa Ujumbe huo.

“Pia tunachunguza kuzuiwa kwa makusudi msaada wa kibinadamu unaoelekezwa kwa raia wanaoishi katika maeneo yanayodhibitiwa na upande mwingine,” Rishmawi alisema. “Pande kwenye mzozo lazima zihakikishe na kuwezesha ufikiaji salama, huru na usiozuiliwa wa kibinadamu kwa raia walio na uhitaji mkubwa.”

Ujumbe huo wa Kutafuta Ukweli ulizungumzia kuhusu mkutano ujao wa Kimataifa wa Kibinadamu kwa ajili ya nchi ya Sudan na nchi jirani, ambao unatazamiwa kufanyika mjini Paris nchicni Ufaransa tarehe 15 Aprili, 2024. Ujumbe huo unatumaini kuwa upungufu mkubwa wa ufadhili ambao hadi sasa umefikia asilimia sita tu ya makadirio ya dola bilioni 2.7 zinazohitajika kushughulikia mzozo huo, utashughulikiwa mapema iwezekanavyo.