Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mazungumzo kuhusu Sudan yaanza huko Jeddah, Saudi Arabia

Wakimbizi kutoka Sudan wakisubiri kuchukua vitu vya msaada katika kijiji cha mpakani nchini Chad.
© UNICEF/Donaig Le Du
Wakimbizi kutoka Sudan wakisubiri kuchukua vitu vya msaada katika kijiji cha mpakani nchini Chad.

Mazungumzo kuhusu Sudan yaanza huko Jeddah, Saudi Arabia

Amani na Usalama

Ikiwa ni miezi sita tangu kuzuka kwa mapigano nchini Sudan hii leo mazungumzo ya Jeddah yameanza rasmi ambapo Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, Martin Griffiths amesema mazungumzo hayo yamekuja wakati muafaka kwani maafa ya kibinadamu nchini humo yanaendelea kushuhudiwa bila kusitishwa

Katika taarifa yake kutoka Jeddah nchini Saudi Arabia, Griffiths ametoa picha ya madhila yanayowasibu wananchi wa Sudan 

  • Maelfu ya watu wameuawa au kujeruhiwa. 
  • Mtu mmoja kati ya tisa amekimbia makazi yao. 
  • Karibu theluthi moja ya watu wanaweza kuwa na uhaba wa chakula hivi karibuni.
  • Mfumo wa afya uko katika hali mbaya, huku hofu ya milipuko ya magonjwa, ikiwa ni pamoja na kipindupindu, imetanda.
  • Watoto wapo hatarini kukosa elimu kamili.
  • OCHA wamepungukiwa na mabilioni ya dola ya ufadhili twanayohitaji ili kuhudumia wenye uhitaji. 

 

Ameeleza kuwa pamoja na changamoto hizo jumuiya ya kibinadamu imefanya kila iwezalo kukidhi mahitaji hayo yanayozidi kuongezeka kila mara. 

“Tangu katikati ya mwezi Aprili, tumefikia watu milioni 3.6 kwa kutoa a aina fulani ya misaada, lakini hii ni asilimia 20 tu ya watu tunaotarajia kuwasaidia.”

Ameeleza kuwa wafanyakazi wa misaada wamekatishwa tamaa na mapigano pamoja na ukosefu wa usalama, na kufanya mazingira ya utendaji kazi nchini Sudan kuwa na changamoto kubwa.

“Hii ndiyo sababu mazungumzo haya ya Jeddah ni muhimu: Tunahitaji Vikosi vinavyopigana nchini Sudan kuvunja msongamano wa ukiritimba. Tunawahitaji kuzingatia kikamilifu sheria za kimataifa za kibinadamu. Tunahitaji usalama ili tuweze kuwafikia wahitaji na iwe endelevu na tusizuiliwe kuwafikia wenye uhitaji, iwe ni Darfur, Khartoum au Kordofans.” Alisema Mkuu huyo wa OCHA.

Kwa kuzingatia mzozo mkubwa wa kibinadamu nchini Sudan, amesema ofisi yake itawezesha ufuatiliaji wa kibinadamu wa mazungumzo haya.” Ninakaribisha kuanzishwa tena kwa mazungumzo haya na ninashukuru Ufalme wa Saudi Arabia na Marekani kwa kuwa mwenyeji pamoja.” 

Amehitimisha taarifa yake kwa kueleza kuwa mazungumzo haya ni “fursa madhubuti ya kuwafahamisha watu wa Sudan kwamba hawajasahaulika, kwamba tunachukua majukumu yetu ya kimataifa kwa uzito, na kwamba tumejitolea kuhakikisha wanapata matunzo, ulinzi na usaidizi wa kuokoa maisha wanaohitaji.”