Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa waondolewa nchini Sudan

Moshi ukiongezeka kufuatia shambulio la bomu katika kitongoji cha Al-Tayif mjini Khartoum, Sudan.
Open Source
Moshi ukiongezeka kufuatia shambulio la bomu katika kitongoji cha Al-Tayif mjini Khartoum, Sudan.

Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa waondolewa nchini Sudan

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekaribisha taarifa za kuhamishwa kwa muda mamia ya wafanyakazi na wategemezi wa Umoja wa Mataifa kutoka katika mji wa Khartoum na maeneo mengine nchini Sudan.

Taarifa iliyotolewa mapema hii leo jijini New York Marekani na Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu Farhan Haq imesema Guterres ameshukuru ushirikiano uliotolewa na pande zote nchini Sudan kuruhusu operesheni hiyo ifanyike bila ya tukio lolote.

“Katibu Mkuu amesisitiza wito wake kwa pande husika kusitisha mapigano mara moja na kuruhusu raia wote kuhama kutoka katika maeneo yaliyoathiriwa na mapigano hayo.” Amesema Haq 

Naibu Msemaji huyo ameongeza kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amethibitisha kuendelea kujitolea kwa shirika hilo kusimama pamoja na kufanya kazi kwa ajili ya watu wa Sudan, kuunga mkono kikamilifu matakwa yao ya mustakabali wenye amani, usalama na kurejea kwenye kipindi cha mpito cha kidemokrasia. Umoja wa Mataifa utafanya kazi yake na wafanyakazi wake, ndani na nje ya Sudan. 

Amehitimisha taarifa yake kwa kueleza kuwa Katibu Mkuu ataendelea kutumia ofisi zake kuratibu kwa karibu na wadau wake, kupunguza mivutano na kuweka usitishaji wa kudumu wa vita. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu Kudumisha Amani na Usalama wa Kimataifa.
UN Photo/Eskinder Debebe
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu Kudumisha Amani na Usalama wa Kimataifa.

Kuwaondoa wafanyakazi wa kimataifa

Umoja wa Mataifa nchini Sudan una wafanyakazi 877 wa kimataifa na wafanyakazi 3,272 wa kitaifa, jumla ni 4,149.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuratibu kipindi cha mpito Sudan, UNITAMS walio hamshwa ni wafanyakazi wake walioajiriwa kimataifa ambao wametolewa Kahrtoum kwenda Bandari ya Sudan ambapo hapo watahamishwa kwenda nchi jirani.

UNITAMS wamesema mchakato wa kuwaondoa ni kupunguza hatari kwa usalama wa wafanyakazi wake lakini wafanyakazi hao wataendelea na kazi wakiwa katika nchi hizo za jirani ili kuhakikisha wanawapatia msaada wananchi wa Sudan.

Mpaka sasa kuna takriban watu 700 kutoka mashirika ya Umoja wa Mataifa, mashirika ya kimataifa yasiyo ya kiserikali (INGOs) na wafanyakazi wa ubalozi pamoja na wategemezi wao wamefika Bandari ya Sudan kwa njia ya barabara.

Kati yao kuna wafanyakazi 43 wa Umoja wa Mataifa walioajiriwa kimataifa na wafanyakazi 29 wa INGOs tayari wamehamishwa kutoka El Geneina (Darfur Magharibi) na Zalingei (Darfur ya Kati) hadi nchini Chad huku shughuli nyingine zikiendelea au kupangwa kuendelea.

Mkuu wa UN Sudan asalia na wafanyakazi wengine

Kutakuwa na idadi ndogo ya wafanyakazi walioajiriwa kimataifa, akiwemo Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu Volker Perthes, watasalia nchini Sudan na wataendelea kufanyia kazi utatuzi wa mgogoro uliopo na kurejea kwenye majukumu yaliyoagizwa na Umoja wa Mataifa.

“Uwepo wetu hapa mashinani umerekebishwa kwa kuzingatia hali ya usalama lakini niwahakikishie kwamba hakuna mpango au mawazo ya Umoja wa Mataifa kuondoka Sudan,” amesema Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu (SRSG) nchini Sudan Volker Perthes.

Umoja wa Mataifa pia unachukua hatua zinazohitajika kuwalinda wafanyakazi wa Sudan na familia zao na inatafuta kila njia iwezekanayo kuwasaidia.

“Tumejitolea kusalia Sudan na kusaidia watu wa Sudan kwa kila njia iwezekanavyo. Tutafanya kila tuwezalo kuokoa maisha huku tukilinda usalama wa wafanyikazi wetu” Amesema Perthes

SRSG Perthes ataendelea kutumia ofisi yake kuratibu kwa karibu na wadau wengine ili kupunguza mvutano na kumaliza uhasama nchini Sudan.