Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UN ashiriki futari na wakimbizi wa Sudan nchini Misri 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (kulia) akishiriki Iftar na wakimbizi wa Sudan huko Cairo, Misri.
UN Photo/Mark Garten
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (kulia) akishiriki Iftar na wakimbizi wa Sudan huko Cairo, Misri.

Mkuu wa UN ashiriki futari na wakimbizi wa Sudan nchini Misri 

Wahamiaji na Wakimbizi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amekutana na kundi la wakimbizi wa Sudan, waliokimbia machafuko nchini mwao hivi karibini na kukimbilia kusaka hifadhi nchini Misri. 

Mkuu huyo wa UN amekutana nao na kushiriki katika futari siku ya jumamosi jioni 23 Machi,2024 ambapo katika mazungumzo yao alisisitiza umuhimu wa amani na utulivu, hasa wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, na kuzitaka pande zote kwenye mzozo wa Sudan kuzingatia usitishaji wa uhasama.

“Katika wakati huu, jumuiya ya kimataifa lazima ielezee watu wa Sudan mshikamano uleule ambao Wasudan wamekuwa wakiutoa kila mara kwa wale wanaotafuta hifadhi ndani ya Sudan,” Guterres alisema.

Kabla ya mzozo huo, Sudan ilikuwa mwenyeji wa zaidi ya wakimbizi milioni moja, wengi wao walilazimika kurejea katika nchi zao kabla ya wakati. Vita hivyo hadi sasa vimewalazimu zaidi ya watu milioni 1.5 kukimbilia nchi jirani ambazo rasilimali zao tayari zilikuwa zimezidiwa, ikiwemo Misri.

Takriban mwaka mmoja wa mzozo

Ziara ya Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa imekuja wiki chache kabla mzozo wa Sudan kuadhimisha mwaka wake wa kwanza.

Hadi kufikia tarehe 17 Machi 2024, kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri, zaidi ya watu 500,000 wa Sudan walikimbia mzozo wa Sudan kwenda kusaka hifadhi nchini Misri, na kuifanya Misri kuwa mwenyeji wa pili kwa ukubwa wa watu wa Sudan wanaokimbia mzozo wa hivi karibuni, ikifuatiwa na nchi ya Chad.

Katika muda wa miezi 11, idadi ya wakimbizi wa Sudan waliosajiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumiwa wakimbizi UNHCR nchini Misri iliongezeka kwa karibu mara tano. UNHCR inawapa hati, huduma za ulinzi pamoja na huduma ya afya, elimu na usaidizi wa pesa taslimu kwa walio hatarini zaidi. Hata hivyo, kwa asilimia 22 pekee ya ufadhili iliyofikiwa hadi sasa, uendelevu wa huduma hizi uko hatarini.

“Msaada wa ziada kwa UNHCR na kwa Serikali ya Misri, katika ngazi ya serikali kuu na mitaa, bado ni muhimu, hasa kuendelea kuhakikisha upatikanaji wa huduma za umma kwa wote. Mzozo unaoendelea nchini Sudan hauwezi kusahaulika,” alisema Dk. Hanan Hamdan, Mwakilishi wa UNHCR katika Serikali ya Misri na Umoja wa Mataifa ya Kiarabu.

Utamaduni wa Guterres

Ziara ya Guterres nchini Misri inakuja kama sehemu ya utamaduni aliouanzisha alipokuwa Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Wakimbizi ili kuangazia jamii za Waislamu zilizo katika dhiki. 

Katika ziara yake ya siku mbili, alikariri akirejea wito wake wa dharura wa kusitishwa kwa mapigano kwa sababu za kibinadamu na kukomesha ghasia, haswa huko Gaza na Sudan.