Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rais wa Baraza Kuu atangaza uzinduzi wa kwanza wa Wiki ya Uendelevu

Maandalizi ya mkutano wa Baraza Kuu la UN kuhusu malengo ya maendeleo endelevu, SDGs au Ajenda 2030
UN/Manuel Elias
Maandalizi ya mkutano wa Baraza Kuu la UN kuhusu malengo ya maendeleo endelevu, SDGs au Ajenda 2030

Rais wa Baraza Kuu atangaza uzinduzi wa kwanza wa Wiki ya Uendelevu

Masuala ya UM

Rais wa Baraza Kuu  la Umoja wa Mataifa leo ametangaza uzinduzi wa Wiki ya Uendelevu ya shirika la Umoja wa Mataifa, ikijumuisha mfululizo wa mijadala na mipango ya ngazi ya juu inayolenga kuhimiza utekelezaji wa mazoea endelevu na kushughulikia changamoto zinazoikabili dunia.

Rais huyo wa Baraza Kuu Dennis Francis amesema wiki hiyo itafanyika kuanzia tarehe 15 hadi 19 Aprili, na mpango mkuu utakaojumuisha nada mbalimbali zilizoaririwa ndani ya wiki hiyo ya umoja, yenye matokeo ya kusongesha sekta muhimu kama vile utalii, miundombinu, nishati na usafiri.

Bwana Francis amewaambia waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Msrekani kwamba "Mpango wa Wiki ya Uendelevu kimsingi umeundwa ili kuchochea kasi katika uendelevu kwa njia ambayo inasaidia kutekeleza Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu," 

Ameongeza kuwa ushiriki wa hali ya juu unatarajiwa kutoka kwa wakuu wa nchi na serikali, mawaziri mahususi wa sekta na maafisa wakuu wa Umoja wa Mataifa.

Watoto kutoka mji wa Xochimilco wakiwa wamebeba mabango ya malengo ya maendeleo endelevu SDGs
UNIC Mexico/Antonio Nieto
Watoto kutoka mji wa Xochimilco wakiwa wamebeba mabango ya malengo ya maendeleo endelevu SDGs

Yatakayojiri katika Wiki ya Uendelevu

Tarehe 15 Aprili: Mjadala wa mada ya ngazi ya juu kuhusu uendelevu wa madeni na usawa wa kijamii na kiuchumi, ukiangazia athari za kuongezeka kwa madeni kwenye mwelekeo wa maendeleo ya nchi.

Tarehe 16 Aprili: Mjadala wa ngazi ya juu kuhusu utalii, kushughulikia mazoea yasiyo endelevu katika sekta hii na kuzindua mfumo wa takwimu wa kupima uendelevu.

Tarehe 17 Aprili: Mkutano wa ngazi ya juu kuhusu usafiri endelevu, ukisisitiza umuhimu wake katika kufikia Malengo kadhaa ya Maendeleo Endelevu (SDGs)

Tarehe 18 Aprili: Mazungumzo yasiyo rasmi kuhusu kujenga uthabiti wa kimataifa na kukuza maendeleo endelevu kupitia uunganishwaji wa miundombinu

• Tarehe 19 Aprili: Uainishaji wa kimataifa kuhusu nishati endelevu, zikiakisi maendeleo na mapungufu katika Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Nishati Endelevu kwa Wote 2014-2024 na kuzindua wito wa kuchukua hatua ili kuharakisha utekelezaji wa SDG 7 kuhusu nishati nafuu na safi.

Nchi za Visiwa vidogo zinazoendelea zinakabiliwa na changamoto ya utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu SDGs
© IOM/Abraham Diaz
Nchi za Visiwa vidogo zinazoendelea zinakabiliwa na changamoto ya utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu SDGs

Zaidi ya ajenda ya 2030

Rais huyo wa Baraza Kuu Francis pia ameangazia mipango zaidi ya Ajenda ya 2030, ikijumuisha kampeni ya Chagua Uendelevu, ambayo inawahimiza washikadau kupitisha ahadi na mazoea endelevu.

"Ninahimiza wawakilishi wote wa kudumu wa Umoja wa Mataifa, wadau na vyombo vya habari kupitisha ahadi za kuchagiza uendelevu na kutangaza uungaji mkono wao kwenye mitandao ya kijamii huku wakifuata mazoea endelevu," 

Kwa upande wake, ofisi yake, pamoja na mambo mengine, inafanya kazi ya kukomesha matumizi ya mabango wakati wa mkutano wa Baraza Kuu na badala yake kuweka skrini za kisasa za TV zinazotumia nishati kidogo lakini zinazodumu kwa muda mrefu.