Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Najivunia kuirejesha FAO katika msingi wa jukumu lake:Graziano da Silva

Mkurugenzi Mkuu wa FAO Jose Graziano da Silva akihutubia kikao cha ufunguzi cha mkutano wa kikanda kuhusu vijana na kilimo mjini Kigali Rwanda.
FAO/Luis Tato
Mkurugenzi Mkuu wa FAO Jose Graziano da Silva akihutubia kikao cha ufunguzi cha mkutano wa kikanda kuhusu vijana na kilimo mjini Kigali Rwanda.

Najivunia kuirejesha FAO katika msingi wa jukumu lake:Graziano da Silva

Masuala ya UM

Kuzalisha chakula cha kutosha sio tatizo, tatizo ni fursa ya watu kupata chakula kilichopo ili kupambana na njaa na utapiamlo.  

Kauli hiyo imetolewa na Jose Graziano da Silva mkurugenzi mkuu wa shirika la chakula na kilimo FAO  katika mahojiano maalum ya kumaliza muda wake. Da silva amesema njaa ni tatizo mtambuka na hivi sasa watu wanazalisha chakula kingi kinachoweza kulisha dunia nzima lakini bado kuna watu zaidi ya milioni 820 wanaokabiliwa na njaa duniani, hivyo anachojivunia zaidi kwa kipindi cha miaka 8 aliyokuwa mkuu FAO ni kubadili mtazamo wa kukabiliana na upande wa pili wa shilingi kuhusu njaa

Bwana da Silva amesema, “tulitambua kwamba tunahitaji kuliangalia pia suala la fursa , wakati mwingine watu hawana fecha za kununua chakula wanachokihitaji , FAO ikaanza sasa kushughulikia suala la walaji kufanya watu waweze kumudu gharama za chakula, kufanya chakula kipatikane zaidi kwa watu, nadhani hayo yalikuwa mabadiliko muhimu sana tuliyoyatekeleza”

 Halikadhalika amesema licha ya kuwa mstari wa mbele katika kampeni na miradi mbalimbali ya Umoja wa Mataifa yenye lengo la kutokomeza njaa anasema mtihani ni mgumu hasa katika kutimiza lengo hilo namba 2  la maendeleo ifikapo 2030 kwani sasa linakwenda kombo akisema kuwa, “kwa bahati mbaya ndivyo ilivyo na miongoni mwa malengo 17 ya SDGs, namba mbili la kutokomeza njaa na mifumo yote ya utapiamlo ndilo linafanya vibaya zaidi ya malengo yote, tunahitaji kufanya jitihada zaidi kurejea katika mstari unaopaswa”

Pamoja na kwamba anaondoka madarakani bwana da Silva amesisitiza kupewa kipaumbele tatizo lingine kubwa linalohusiana na chakula akifafanua kuwa, “utipwatipwa unaathiri wote nchi zilizoendelea, zinazoendelea, watu tajiri na masikini, ni suala gumu zaidi , itakuwa vigumu kukabiliana na changamoto ya kukomesha tatizo la utipwatipwa endapo hatutobadilli kabisa mifumo yetu ya chakula.”

 Graziano Da Sila mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 30 kama mtaalam wa masuala ya usalama, chakula na maendeleo vijijini leo Julai 31 anaachia ngazi rasmi kama mkurugenzi mkuu wa FAO baada ya kuliongoza shirika hilo tangu mwaka 2012.