Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtindo ya maisha miongoni mwa sababu za ugonjwa wa Homa ya ini

Hospitali ya Bugando iliyoko jijini Mwanza Tanzania
UN News
Hospitali ya Bugando iliyoko jijini Mwanza Tanzania

Mtindo ya maisha miongoni mwa sababu za ugonjwa wa Homa ya ini

Afya

Leo dunia inaadhimisha siku ya Homa ya ini ulimwenguni, ambayo imewekwa kwa lengo la kujenga uelewa kwa jamii juu ya ugonjwa huu unaoshambulia ini kwa kasi na kushindwa kufanya kazi yake vizuri.

Nchi mbalimbali duniani zinaungana kwa pamoja kuazimisha siku hii inayobebwa na Kauli mbiu inayosema kufikia utokomezaji wa homa ya ini ndani ya mifumo ya afya inayoendelea
Kwa mujibu wa takwimu za shirika la afya duniani WHO zinaonesha kuwa asilimia 90 ya watu ulimwenguni huishi na ugonjwa huu bila kujitambua, huku takribani watu 3000 hufariki dunia kila siku kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya homa ya ini aina hepatitis B na C.

Hata hivyo kila baada ya sekunde 30 mtu mmoja duniani hupoteza maisha kutokana na maradhi hayo, hatua mbayo mashiika ya afya ulimwenguni,serikali na taasisi zisizo za kiserikali kuanza kutoa elimu kwa jamii wakihamasisha wapime ili kupata chanjo  na matibabu ya homa ya Ini.

Hata hivyo WHO inalenga kutokomeza ugonjwa wa homa ya ini ifikapo mwaka 2030 na kunatoa wito kwa nchi kufikia malengo mahususi ili Kupunguza maambukizi mapya ya hepatitis B na C kwa 90%,Kupunguza vifo vinavyohusiana na homa ya ini na saratani kwa 65%,Hakikisha kuwa angalau 90% ya watu walio na virusi vya hepatitis B na C wametambuliwa.

Unawezaje kuambukizwa homa ya ini?

Kwa mujibu wa Daktari mbobezi wa magonjwa ya mfumo wa chakula na Ini kutoka hospital ya Rufaa ya Kanda Bugando Dr. David Majinge katika mahojiano na Evarist Mapesa wa Redio SAUT FM iliyoko jijini Mwanza Tanzania amesema homa ya ini ni ugonjwa unaoletwa na virusi wanaoitwa Hipatisis ambao wamegawanyika katika makundi matano ambayo ni hepatitis A,B,C,D,na E.
“ A na E huambukiza zaidi kwa njia ya chakula, kama umekula chakula ambacho kina contamination (uchafu), au vinywaji ambavyo vina contamination, mara nyingi tunapozingatia usafi wa chakula, utakuwa umeweza kujikinga usipate maambukizi ya homa ya ini ambayo ni A na E”, alisema Dk. Majinge.

Aina nyingine za B,C, na D huambukizwa kwa njia ya maji maji ya mwilini ( body fluids) kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine.

“changamoto ya homa ya ini nayenyewe kama ilivyo kwa ugonjwa kama Ukimwi, ukishika damu ambayo ina maambukizo, majimaji ya njia ya uko, kwa njia ya kujamiiana,na yenyewe pia inaweza kukuambukiza” alisema Dk. Majinge.

Tumeiona  pia changamoto kwa wale wanaotumia madawa ya kulevya kwenye kujidunga, kuchangia vitu vyenye ncha, mswaki,nyembe,au unapoenda kupata huduma katika sehemu ambazo hazizingatii usafi unakuwa uko katika hatari ya kuambukizwa” aliongeza Dk. Majinge.

Daktari David Majinge kutoka hospitali ya Bugando Mwanza Tanzania
UN News
Daktari David Majinge kutoka hospitali ya Bugando Mwanza Tanzania

Mtindo wa maisha unaweza kuwa chanzo cha homa ya ini

Mtindo wa maisha ni miongoni mwa sababu zinazopelekea uwepo wa homa ya ini na inatajwa kuwa iwapo jamii haitobadilika basi ugonjwa huo utaendelea kuenea kwa kasi katika maeneo mbalimbali duniani.

Dk. Majinge anasema mtindo wa maisha huchangia kwa kiasi kikubwa uwepo wa homa ya ini kwa mtu binafsi kutokana na kutofuata kanuni na taratibu za afya ambazo zimekuwazikishauriwa na matabibu kote ulimwenguni.

“Mtindo wa maisha ni moja kati ya vitu vinavyoweza kuchangia mtu kupata changamoto ya homa ya ini,mfano tumekuwa tukiwaambia watu kuacha ngono zembe, matumizi ya pombe kwa mtu ambaye anaumwa ugonjwa huu kwa kuharibu ini kwa uharaka zaidi” aliongeza Dk. Majinge.

Baadhi ya vijana wa kiume na wakike wamekuwa wakichora michoro katika miili yao maarufu kwa jina la tatoo na wakati mwingine kutoboa maskio ili kuleta mvuto fulani katika miili yao, Dk. Majinge anashauri kuwa makini na vifaa ambavyo hutumiwa katika shughuli hizo ili kuzuia katika maambukizi ya homa ya ini.

Mitindo ya maisha huenda mbali zaidi hata aina ya vyakula ambavyo binadamu huvitumia katika milo ya kila siku pia imekuwa ni chanzo cha mtu kupata ugonjwa huu.

“ulaji sahihi unaweza kusaidia kulinda ini lisipatwe na hiyo changamoto,kama lishe ikizingatiwa na mwili ukawa na kinga nzuri basi huenda usipate changamoto ya ugonjwa wa ini, kwahiyo kama chakula tunachokula kinakuwa hakizingatii matakwa labda kuna pombe inazidi,kuna vyakula vyenye mafuta vimezidi, na chumvi nyingi ikazidi, vinaweza kuleta changamoto kwenye ini na kushindwa kufanya kazi yake ya kutengeneza kinga kwa ajili ya kulinda mwili”, alisema Dk. Majinge.

Chanjo hii ya pentavalent, inayotumiwa katika kituo cha afya nchini Mali, ni chanjo iliyounganishwa na chanjo tano za kibinafsi zilizounganishwa na kuwa moja, inayokusudiwa kuwalinda watu kutokana na magonjwa mengi, ikiwa ni pamoja na hepatitis B. (9 Mach
UNICEF/Ilvy Njiokiktjien
Chanjo hii ya pentavalent, inayotumiwa katika kituo cha afya nchini Mali, ni chanjo iliyounganishwa na chanjo tano za kibinafsi zilizounganishwa na kuwa moja, inayokusudiwa kuwalinda watu kutokana na magonjwa mengi, ikiwa ni pamoja na hepatitis B. (9 Mach

Utajuaje kama una homa ya ini?

Dalili za mwanzo hutokea ndani na miezi 6 baada kuambukizwa virusi vya homa ya ini, hutokea kwa baadhi ya watu na sio kwa kila mtu, mgonjwa mwenye maambukizi ya virusi vya homa ya ini hujiskia kuumwa, upoteza hamu ya kula ,  Kupata manjano kwenye macho, vinganja vya mikono/kucha au mwili mzima.

Lakini watu wameshauriwa kupima ili kujua iwapo wanamaambukizo ya homa ya ini ili wataalam waweze kumpa chanjo, ushauri na hata kuanza matibabu iwapo atabainika kuwa na ugonjwa huo.
“kujua kama mtu amepata maambukizo ya homa y aini kitu muhimu ni kupima, vipimo ni rahisi na vinafanyika kwenye hospital mbalimbali, na kwa bahati nzuri kwa Hepatitis B kama mtu akipimwa na akagundulika kuwa hana maambukizo basi anaweza akapata chanjo ambayo itamkinga asiendelee kupata mambukizo”,amesema Dk. Majinge.

Kwa Nini Ni Muhimu Kupima

Homa ya ini ni tatizo la kiafya ulimwenguni linalohitaji kuzingatia kupima na kufuata maelekezo ya wataalam wa afya katika hatua za kujikinga na ugonjwa huo unaoshambulia ini.