Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

220,000 wanahitaji msaada wa kibinadamu haraka Madagascar baada ya kimbunga Gamane: IOM

Mchanga unasukumwa ndani ya nchi na upepo wakati wa msimu wa upepo kusini mwa Madagascar.
UN News/Daniel Dickinson
Mchanga unasukumwa ndani ya nchi na upepo wakati wa msimu wa upepo kusini mwa Madagascar.

220,000 wanahitaji msaada wa kibinadamu haraka Madagascar baada ya kimbunga Gamane: IOM

Msaada wa Kibinadamu

Takriban watu 220,000 wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu kutokana na athari mbaya ya kimbunga cha kitropiki cha Gamane Kaskazini-Mashariki mwa Madagascar limesema shirika la Umoja wa Mataifa uhamiaji IOM

Katika tarifa yake iliyotolewa leo mjini Antananarivi IOM inasema kimbunga hicho cha kitropiki kilitua Machi 27 kaskazini-mashariki mwa Madagascar, na kusababisha uharibifu mkubwa katika maeneo ya Analanjirofo, Diana, Atsinanana, na Sava.

Roger Charles Evina, mkuu wa ujumbe wa IOM nchini Madagascar amesema "Kimbunga hicho kinazidisha ugumu wa maisha ya watu ambao tayari wameelemewa na migogoro mingi ukame. Wakati dhoruba ya Tropiki Alvaro ilitopiga mwezi Januari na mvua nyingi za El niño mnamo mwezi wa Februari zimesababisha mafuriko makubwa katika mikoa ya kaskazini na kusini magharibi, na kuathiri karibu watu 52,000.”

Ili kukabiliana na uharibifu huo uliosababishwa na kimbunga cha kitropiki, IOM lilishiriki katika tathmini ya pamoja ya anga iliyofanywa tarehe 30 Machi na washirika wa kibinadamu na Ofisi ya Kitaifa ya Hatari na Usimamizi wa Majanga (BNGRC).

Taarifa za awali ainaonyesha kwamba watu zaidi ya 535,0000 wameathirika katika jamii 33 zilizokumbwa na mafuriko huku watu 18 wakiuawa na 22,000 kutawanywa.

Pia nyumba hadi 19,000 zilifurika na kuharibiwa vibaya na uharibifu mkubwa kuripotiwa Kwenye miundombinu kama Barabara na miundombinu mingine ya msingi ikijumuisha vituo vya afya 22 na shule 135. Pia ekari zaidi ya 2,200 za mashamba yam punga ziko katika hatihati ya kusambaratishwa na hivyo kuhatarisha maisha ya maelfu ya watu katika maeneo yaliyoathirika.
Serikali yatangaza hali ya dharura

Serikali ya Madagascar imetangaza hali ya dharura ya kitaifa ili kukabiliana na athari za kimbunga hicho.

Washirika wa kibinadamu wanafanya kazi kwa uratibu wa karibu na mamlaka za kitaifa na za mitaa na wanataka kusaidia mara moja watu 165,000 kwa usaidizi wa dharura, ikiwa ni pamoja na malazi, chakula, maji na usafi wa mazingira, huduma za afya, elimu na msaada wa ulinzi. 

Wengi wa familia zilizolazimika kukimbia makwao ambazo hapo awali zilitafuta makazi katika vituo 87 vya uokoaji sasa zinahifadhiwa na jamaa kwa muda na wachache wamesalia katika vituo vya uokozi wengi bado wanahitaji msaada wa haraka, ikiwa ni pamoja na kuwa na uwezo wa kurejea nyumbani.

Vifaa vya dharura vinavyopatikana nchini vinakaribia kuisha, kwani akiba zimetumika kusaidia watu walioathiriwa na majanga tangu mwanzoni mwa mwaka. 

Hali ya ufikiaji waathirika katika maeneo yaliyoathiriwa na kimbunga cha kitropiki bado ni changamoto, pamoja na unafuu unaotolewa kwa njia ya anga au baharini kutokana na uharibifu wa barabara na madaraja. 

Kwa mujibu wa IOM ufadhili wa ziada unahitajika kwa haraka ili kuendeleza juhudi za msaada huku kukiwa na rasilimali chache zinazopatikana.

Madagascar iko katika hatari ya majanga ya asili

Madagascar inakabiliwa sana na hatari za majanga ya asili na iko kati ya nchi 10 zilizo hatarini zaidi na mabadiliko ya tabianchi duniani. 

Katika miaka ya hivi karibuni, nchi hiyo imekuwa ikikabiliwa na mfululizo wa majanga yanayotokana na ukame, mafuriko na vimbunga, na kusababisha vifo, uharibifu mkubwa wa nyumba, miundombinu muhimu na rasilimali za uzalishaji, na kusababisha watu wengi kuhama makazi yao. 

Madhara ya hatari za majanga ya asili yanazidishwa na uharibifu mkubwa wa mazingira, na sasa theluthi moja ya rasilimali za ardhi za kisiwa hicho zimeathiriwa na mmomonyoko wa ardhi, na kusababisha madhara makubwa kwa uwezo wa watu wa kukabiliana na kushughulikia matatizo kwa njia endelevu.

IOM inataka msaada wa haraka ili kukabiliana na janga la kibinadamu nchini Madagascar. 

Kabla ya kimbunga hicho, Umoja wa Mataifa ulikadiria kuwa watu milioni 2.3 wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu nchini Madagascar. 

Jumla ya dola milioni 90 zimeombwa chini ya ombi la mwaka huu wa  2024, ambalo kwa sasa linafadhiliwa chini ya asilimia 20, na chini ya dola milioni 15 zimepokelewa hadi sasa.

Shirika hilo linasema bila msaada wa kifedha juhudi za msaada wa kibinadamu zitakuwa hatarini na kuwaacha maelfu ya watu katika hali mbaya.