Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yashikamana na watu wa Madagascar baada ya kimbunga Gamane

Watu wa kusini mwa Madagascar wanajifunza kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
UN News/Daniel Dickinson
Watu wa kusini mwa Madagascar wanajifunza kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

UN yashikamana na watu wa Madagascar baada ya kimbunga Gamane

Tabianchi na mazingira

Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na washirika wake nchini Madagascar wanaisaidia serikali ya kisiwa hicho kukabiliana na athari za kimbunga Gamane.

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo mjini New York Marekani msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema “Kulingana na serikali kimbunga hiki cha kitropiki kilichoikumba Madagascar  siku ya Jumatano kimeua watu 19, kujeruhi wengine watatu, na kuwaacha takriban watu 22,000 bila makazi.”

Ameongeza kuwa washirika wa kibinadamu wanatazamia kuwafikia watu 165,000 kati ya watu 230,000 wanaohitaji msaada.

Kwa mujibu wa msemaji huyo wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric jumuiya ya kimataifa ya misaada ya kibinadamu inaonya kwamba hifadhi ya misaada ya dharura iko chini sana, mingi ikiwa imetumika wakati wa dhoruba ya Alvaro iliyopiga nchini humo Januari na hatua za kukabiliana na mafuriko mwezi Februari. 

Msemaji huyo ameongeza kuwa “Ombi letu kwa ajili ya Madagascar ambalo litahitaji takriban dola milioni 90 mwaka huu limefadhiliwa chini ya asilimia 20, na chini ya dola milioni 15 ndizo zimepokelewa hadi sasa.