Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita inayoendelea Gaza kwa miezi sasa ni usaliti dhidi ya ubinadamu: Griffiths

Picha za uharibifu wa hospitali ya Al-Shifa huko Gaza, kufuatia kumalizika kwa mashambulizi wa hivi karibuni ya Israel. Shirika la Afya Duniani (WHO) lilikariri kuwa hospitali lazima ziheshimiwe na kulindwa; lazima zisitumike kama uwanja wa vita.
UN News
Picha za uharibifu wa hospitali ya Al-Shifa huko Gaza, kufuatia kumalizika kwa mashambulizi wa hivi karibuni ya Israel. Shirika la Afya Duniani (WHO) lilikariri kuwa hospitali lazima ziheshimiwe na kulindwa; lazima zisitumike kama uwanja wa vita.

Vita inayoendelea Gaza kwa miezi sasa ni usaliti dhidi ya ubinadamu: Griffiths

Amani na Usalama

Mratibu mkuu wa misaada na masuala ya dharura wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths amesema vita inayoendelea Gaza imefikia harua ya kutisha. 

tarifa yake iliyotolewa leo mjini New York Marekani kwa ajili ya miezi sita ya vita hiyo Griffiths amesema “Kwa watu wa Gaza, miezi sita iliyopita ya vita imeleta vifo, uharibifu na sasa matarajio ya aibu ya njaa iliyosababishwa na mwanadamu.”

 Ameendelea kusema kwmba kwa watu walioathiriwa na hofu ya kudumu ya mashambulizi ya Oktoba 7, imekuwa miezi sita ya malalamiko na mateso.

“Kila siku, vita hivi vinaongeza idadi ya waathirika waliopoteza Maisha miongoni mwa raia. Kila sekunde vita inapoendelea inapanda mbegu za mustakbali ulioghubikwa na vita hiyo isiyokoma.” Amesema Griffith ambaye pia ni mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kibinadamu na masuala ya dharira OCHA.

Bwana Griffiths amesema “Kama mimi na wengine wengi tumesema mara kwa mara, mwisho wa vita hivi umechelewa sana sasa ni wakati wa kuvikomesha.”

 Badala yake, amesema “tunakabiliwa na matarajio ya sinto fahamu yanayoongezeka zaidi huko Gaza, ambapo hakuna mtu aliye salama na hakuna mahali popote salama pa kwenda.”

Operesheni ambayo tayari ni tete inaendelea kudhoofishwa na milipuko ya mabomu, ukosefu wa usalama na kunyimwa fursa ya kufikiwa na misaada ameongeza afisa huyo wa Umoja wa Mataifa

Martin Griffiths, Mratibu wa Msaada wa Dharura wa Umoja wa Mataifa
UN News/Daniel Johnson
Martin Griffiths, Mratibu wa Msaada wa Dharura wa Umoja wa Mataifa

Juhudi za kukomesha mzozo wa Gaza haziridhishi 

Kwa mujibu wa Bwana Griffiths ni mara chache sana kumekuwa na ghadhabu ya kimataifa juu ya athari ya migogoro, huku inaonekana kuwa na juhudi kidogo sana za kuikomesha na badala yake ukwepaji sheria umefurutu ada.

 Amesema “Katika siku hii, moyo wangu unaenda kwa familia za waliouawa, kujeruhiwa au kuchukuliwa mateka, na wale ambao wanakabiliwa na mateso ya kutojua masaibu ya wapendwa wao.”

Amehitimisha tarifa yake kwa kusema kwamba “Haitoshi kwa miezi sita ya vita kuwa wakati wa ukumbusho na maombolezo, lazima pia kuchochea azimio la pamoja kwamba kuwe na uwajibikaji kwa usaliti huu wa ubinadamu.”

Miezi sita kamili ya vita Gaza itakuwa kesho Jumapili Aprili 7.