Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC: Kituo cha Amani chakabili habari potofu na za uongo

Afisa Habari wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO ofisi ya Beni jimboni Kivu Kaskazini akipatia mafunzo wanahabari, wanaharakati na wanafunzi wa Vyuo Vikuu kuhusu habari potofu na habari za uongo mjini Beni.
UN./George Musubao
Afisa Habari wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO ofisi ya Beni jimboni Kivu Kaskazini akipatia mafunzo wanahabari, wanaharakati na wanafunzi wa Vyuo Vikuu kuhusu habari potofu na habari za uongo mjini Beni.

DRC: Kituo cha Amani chakabili habari potofu na za uongo

Amani na Usalama

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, kituo kilichojengwa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO kimesaidia vijana kukabiliana na habari potofu na za uongo ambazo huchochea ukosefu wa amani kwenye taifa hilo la Maziwa Makuu barani Afrika. 

Jean Claude Batumike, ambaye ni Mkuu wa kituo cha vijana cha Amani, kilichoko eneo la Kamanyola huko jimboni Kivu Kusini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC akizungumza kupitia video ya MONUSCO iliyochapishwa kwenye mtandao wa Instagram anasema kituo hicho kilipojengwa watu walijihisi wako na amani zaidi.

Anasema kituo cha amani kilijengwa kwa ajili ya amani ili kuondoa migogoro kwa vijana na jamii kwa ujumla. Kituo kina kompyuta, mtandao wa intaneti wakati wote na skrini kubwa ambapo katika video hiyo wanaonekana vijana wakipita hapa na pale huku wakipatiwa maelezo na Bwana Batumike.

Akilinganisha hali kabla na baada ya kujengwa kwa kituo hicho, Bwana Batumike anasema, “mara nyingi wakati tulikuwa na mizozo hapa kwenye eneo letu, hakukuweko na mahali ambapo watu wanaweza kwenda na kutatua mizozo, lakini tangu wamejenga hiki kituo cha Amani, kushikakuweko na mzozo wa vijana au jamii, wanakimbilia kituo cha Amani, wanakaa pamoja na kutatua mizozo na hatimaye mambo yanakuwa mazuri zaidi.”

Bwana Batumike akaelezea kuwa kituo cha Amani kinasaidia kukabili habari za uongo na potofu kwa kuwa kituo kina mtandao wa uhakika wa intaneti, kompyuta na skrini na wanaweza kupata habar iza ukweli.

“Mara nyingi vijana wanapokuwa na habari za wasiwasi ambazo hawana uhakika nazo ni rahisi kufika kituo cha Amani, wanajiunganisha kwenye intaneti, wanarambaza na kusogoa na wengine kwa mtandao na kupata habari za ukweli. Na katika sehemu yenye mzozo, unahitaji kupata habari za uhakika,” anasema Bwana Batumike.