Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC: Mapigano yameshamiri tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu Desemba- Keita

Bintou Keita (kwenye skrini) Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa UN nchini DRC na pia Mkuu wa MONUSCO akihutubia Baraza la Usalama la UN hii leo kutoka Kinshasa, mji mkuu wa DRC.
UN /Eskinder Debebe
Bintou Keita (kwenye skrini) Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa UN nchini DRC na pia Mkuu wa MONUSCO akihutubia Baraza la Usalama la UN hii leo kutoka Kinshasa, mji mkuu wa DRC.

DRC: Mapigano yameshamiri tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu Desemba- Keita

Amani na Usalama

Hali  ya usalama mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC imezorota tangu kukamilika kwa uchaguzi mkuu nchini humo mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka jana, amesema Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa nchini humo, Bintou Keita wakati akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo.

Tweet URL

Alikuwa akiwasilisha ripoti mpya zaidi ya Katibu Mkuu wa UN kuhusu DRC, kutokea Kinshasa mji mkuu wa DRC ambapo amesema waasi wa M23 wanazidi kusonga mbele na kupanua eneo lao la kwa kiwango kikubwa.

Kwa mujibu wa WFP, asilimia 25 ya wananchi wote zaidi ya milioni 90 nchini DRC wanakabiliwa na njaa.

Hali  ya kibinadamu imezidi kuzorota

Bi. Keita ambaye pia ni Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani, DRC, MONUSCO amesema hali mbaya ya usalama imefanya hali ya kibinadamu kuwa mbaya huku idadi ya wakimbizi wa ndani ikifika viwango vya juu.

“MONUSCO tayari inasaidia serikali katika juhudi zake za kutekeleza marekebisho ya sekta ya ulinzi na usalama na marekebisho mengine muhimu ya utendaji wa serikali ili iweze kunufaika kwa mapana zaidi kwa mujibu wa maridhiano yaliyomo kwenye azimio la majukumu ya MONUSCO,” amesema Bi. Keita.

Hata hivyo amesema operesheni za kijeshi dhidi ya waasi, ziende sambamba na uwekezaji kwenye michakato ya amani kikanda, kitaifa na kimajimbo bila kusahau programu za kina za upokonyaji silaha, uvunjaji wa makundi na ujumuishaji kwenye jamii, P-DDRCS kwa waasi, mpango ambao Umoja wa Mataifa umepanga kutekeleza kupitia programu ya pamoja na serikali.

Rwanda haikanushi uweko wake ndani ya DRC – Balozi Mukongo

Mwakilishi wa Kudumu wa DRC kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Zenon Ngay Mukongo akihutubia Baraza amesema “kwanza kabisa, Rwanda haikanushi tena uweko wa jeshi lake kwenye ardhi ya DRC. Pili, wanajeshi wa Rwanda wanashiriki kwenye mapigano wakitumia zana za kisasa za vita zilizowekwa kwenye ardhi ya DRC. Tatu, jeshi la Rwanda, katika matukio kadhaa, kwa majivuno, limejaribu utendaji wa makombora yake mapya ya kutoka ardhini kwenda angani, kwa kulenga helikopta za MONUSCO na kwa ndege za kiraia zilizokuwa zimeegeshwa uwanja wa ndege wa Goma.”

Waasi wa FDLR wanaambatana na jeshi la serikali la DRC – Balozi Rwamucyo

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kudumu wa Rwanda kwenye Umoja wa Mataifa Ernest Rwamucyo amewaeleza wajumbe kuwa shaka na shuku za Rwanda bado hazijapatiwa majibu. Shaka na shuku hizo ni pande mbili. Mosi, uweko na kinga dhidi ya vikosi vinavyosababisha mauaji ya halaiki, na pili, matangazo ya umma ya hivi karibuni kutoka kwa viongozi wa ukanda wetu.

Bwana Rwamucyo amesema, “Rwanda ina wasiwasi na usaidizi wanaopatiwa waasi wa FDLR kutoka jeshi la serikali la DRC, FARDC. Waasi hao wanapatiwa ufadhili, wanapatiwa silaha na wanapigana pamoja na makundi mengine ya wanamgambo wa kikundi cha Wazalengo wakiambatana na FARDC. Usaidizi huu lazima ukome na wafuasi wa FDLR lazima wapokonywe silaha, makundi  yao yavunjwe na warejeshwe Rwanda.”

FDLR ni miongoni mwa makundi ya waasi yanayofanya mashambulizi mashariki mwa DRC.